0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Feb 24, 2009

MAHOJIANO YANGU NA RAHMA, MWEZESHAJI WA UTAMBUZI

Tunaishi kama familia
Hivi karibuni nilifanya mazungumzo na mmoja wa wawezeshaji wa utambuzi katika kituo chetu cha FAJI pale Kimara Rombo, naye si mwingine bali ni Rahma Nsekela.
Rahma Nsekela ni mmoja kati ya wawezeshaji wanaotuwezesha sisi tunaojifunza maarifa haya ya utambuzi tujivunie kile tunachokipata kutoka kwao.
Lengo kubwa la kufanya mahojiano na yeye ni ili kupata uzoefu wake tangu alipoanza kujifunza maarifa ya utambuzi mpaka sasa ambapo ni mmoja kati ya wawezeshaji katika kituo chetu cha FAJI waliojititolea muda wao kuwafundisha wengine.

MWANDISHI: Hebu nipe uzoefu wako juu ya maarifa haya ya utambuzi Kwa nini uliamua kujifunza haya maarifa?

RAHMA: Tangu mdogo nilikuwa na mambo mengi ambayo ambayo yalikuwa yananitanza na kusema ukweli sikuwa nayafurahia. Baadaye nilivyokuwa mkubwa nikaanza kujiuliza “hivi hakuna namna ambayo naweza kubadilisha maisha yangu yakawa bora?” basi kuanzia hapo nikaanza kubadilika taratibu mimi mwenyewe

MWANDISH: Je ni changamoto gani unazopata tangu ulipobadilika kutoka vile watu walivyokuzoea na unavyoishi sasa kama mtu uliyejitambua?

RAHMA: Kwangu mimi hakuna changamoto za kuniumiza kichwa, kwa sasa hakuna linalonishangaza. Mimi nimejifunza kuwachukulia watu jinsi vile walivyo bila ya mimi kufuata matakwa yao, kwa hiyo sioni changamoto zozote zinazohusiana na jinsi watu walivyonizoea na nilivyo sasa. Wana uhuru wa kufikiria chochote.

MWANDISHI: Je wazazi, ndugu na marafiki zako wanakuonaje sasa?

RAHMA: Kuna siku nilimsikia mdogo wangu anamwambia mama yangu, hivi unajua fulani siku hizi yuko chanya sana hakuna asiloliweza na siku nyingine rafiki yangu aliniambia anatamani kuwa kama mimi yaani mtu asiye na wasiwasi. Kwa hiyo najua wanaona mabadiliko.

MWANDISHI: Wewe ni mwezeshaji wa utambuzi katika kituo cha FAJI [Familia ya Jitambue]. Je unalipwa?

RAHMA: Ndiyo ninalipwa, lakini si mshahara. Kwetu sisi wawezeshaji kipaumbele kipo kwenye kusambaza haya maarifa tu na kuona mabadiliko ya kweli kwenye jamii. Of course tunatumia hela kuendesha kituo.

MWANDISHI: Je imekuwaje umejitolea kufundisha, kusambaza maarifa haya?

RAHMA: Kwa sababu tunataka watu wajue ukweli mkubwa zaidi ya vile wanavyofikiria. Watu inabidi wajue kuwa kuna mizigo mingi ya kimaisha tunajitwisha na kuna uongo mwingi tunaolishwa ambao unawaletea wengi kero na matatizo ya maisha.

MWANDISHI: Je kuna malengo gani juu ya kituo hiki?

RAHMA: Tunataka kiwe zaidi ya kituo, tunataka kiwe ni chuo chenye kutoa maarifa tofauti na yale ya darasani. Watu wanafundishwa maarifa mengi lakini hayawasaidii maishani mwao. Hakuna haja ya kufuata ule mlolongo tuliouzoea: unazaliwa , unaenda shule, unaanza kazi, unaoa au kuolewa/ unapata watoto, unaanza kuboreka na mwenzi wako, mnazeeka, kisha mnakufa

MWANDISHI: Je kufundisha kuna utaratibu gani, yaani kama mtu anafika hapa na anataka kujifunza haya marifa anaanzia wapi?

RAHMA: Utaratibu pekee unaweza ukawa ni mtu kuwa na azma ya kubadilika kuwa bora, basi atakuja hapa FAJI atajitambulisha na atapewa fomu ya kujiunga madarasa. Madarasa haya ni ya tofauti na ufundishaji wetu ni wa tofauti kabisa,

· Kwani hakuna haja ya mwanafunzi kuandika notes

· Mwanafunzi anaruhusiwa kuchangia maoni na hata kuhoji bila ya aibu baadhi ya hoja au mada zinazotolewa pale darasani.

· Hakuna mwalimu maalumu, wote ni wanafunzi na wote ni walimu, yaani hata mimi kama mwezeshaji siwezi nikasema najua yote yaliyomo kuhusu masomo haya. Hata mtu ambaye ni mgeni amekuja hivi karibuni na ana jambo la kunifundisha, nitamsikiliza, kwani kimsingi kila mtu ana jambo la kumuelimisha mwenzake.

· Kikubwa zaidi tunachosisitiza wakati wa kujifunza maarifa haya ni kutenda kila kinachofundishwa, kwani kutakuwa hakuna maana ya kujifunza kitu ambacho hukitendi, kutenda ndio msingi mkuu wa kumuwezesha mwanafunzi kubadilika kutoka katika kuishi kwa mazoea na kuwa mtu tofauti kabisa na jinsi watu walivyomzoea.

MWANDISHI: Itamchukua mwanafunzi muda gani kuhitimu?

RAHMA: Maarifa haya hayana mwisho, kwa sababu sisi ni wanadamu na kila siku tunaendelea kukua, kubadilika na kujifunza. Maarifa haya hayana hatima kwa sababu kujifunza maarifa haya hayakufanyi wewe kuwa mtaalamu/ bingwa wa maisha kwamba hautakosea, hautaumia, hautaumiza; hapana, Hakuna kuhitimu kwa sababu haya tunayojifunza ndiyo maisha yenyewe, sasa ukitaka kuhitimu si ina maana uache kuishi.

MWANDISHI: Kuna kutunukiwa cheti?

RAHMA: Cheti cha nini? Kutenda kwako na kubadilisha maisha yako yawe bora zaidi ni ushahidi tosha kuwa umeelewa na unatenda kwa dhati. Na sisi hatutaki ubadilike kwa ajili ya mtu, yote haya ni kwa ajili yako. Ina maana basi hakuna haja sana ya sisi kuelezwa kuwa fulani anafanya vizuri, yeye binafsi anajua kutoka moyoni mwake kama anatenda au la. Zaidi ya yote, kilichopo akilini mwake kitajidhihirisha tu katika matendo yake na kauli zake.

MWANDISHI: Unashauri nini Watanzania?

RAHMA: Kwa yeyote atakayesoma mahojiano haya, nataka kusema kwamba haujasoma kwa bahati mbaya, kuna sababu maalumu kwani sio watu wote watakaosoma mahojiano haya. Basi ujue hujapotea njia ni vyema ukachukuwa uamuzi ili uweze kujitambua, kubadilisha maisha yako. Sisi tunamkaribisha mtu yeyote bila kujali dini, kabila, cheo chako na vitu vinginevyo visivyo na msingi. Fikeni Kimara Rombo , kama unatokea njia ya mjini basi vuka barabara utaona kibao kimeandikwa kwa maandishi ya bluu FAJI ELIMU YA UTAMBUZI
INAPATIKANA HAPA, wote mnakaribishwa.

MWANDISHI: Ahsante sana Rahma kwa mahojiano haya, nakutakia siku njema.

RAHMA: Ahsante sana ndugu mwandishi.

4 comments:
Andika Maoni Maoni
 1. Nimefurahishwa sana na mahojiano haya kwani ni ukweli mtupu. Hongera sana bwana Kaluse, kwa kusambaza maarifa ya utambuzi. Napendekeza ufanye mahojiano na watu mbali mbali wanaohudhuria madarasa hayo watoe uzoefu wao kwani kuna mambo mengi yakujifunza kupitia kwa uzoefu.

  ReplyDelete
 2. kama alivyosema mbeyele, hii nimbonge la ubuni.
  kuna swali moja muhimu, labda eti Rahma kaolewa, anatafuta, au anatafutwa?

  wengine wako singo au hilo halikubaliki kiutambuzi?

  pweeeeeeeeeeeeeeeenye

  ReplyDelete
 3. Ni muhimu sana kupata walau mahojiano ya watu mbalimbali kwa mwezi mara moja,kama walivyotangulia kusema wenzangu.
  Kamala hilo swali naona labda Kaluse alilisahau.

  ReplyDelete
 4. Huyu mama katika picha ni Chimamanda Ngozi Adichie, mwandishi kutoka Nigeria. Hapo pembeni kulia kuna nakala za riwaya yake iitwayo "Half of a Yellow Sun."

  ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi