Ni Kitu gani unachotaka kufanya katika maisha yako? Je unaota ndoto gani juu ya maisha yako? Je wewe ni mzuri katika eneo gani? Yaani unacho kipaji gani?
Katika umri wa utoto kila mmoja wetu aliwahi kuigiza kuhusu jambo fulani, wapo waliowahi kuigiza kuwa ni madaktari, madereva, wanasiasa, wasanii waigizaji katika filamu na kadhalika na kadhalika.
Wengi wetu pia tuna ndoto fulani juu ya maisha yetu, ndoto ambazo wakati mwingine huziona kana kwamba ndivyo maisha yetu yatakavyo kuwa huko mbele ya safari.
Hapa ningeomba kutahadharisha kwamba kama ndoto zako zilikuwa hasi na zilikuwa zimejaa maumivu na kukatishwa tamaa au hofu za kushindwa katika kufikia malengo yako hayo, basi ujue kwamba hayo ndiyo mavuno ya aidha ulichokuwa nacho leo au utakachovuna kesho ukubwani.
Mara nyingi inashauriwa na wataalamu wa elimu hii ya utambuzi kuwa ndoto zetu zinatakiwa ziwe ni chanya na za kutupa nafuu.
Kwani ndoto ulizokuwa nazo utotoni au ulizonazo leo inawezekana ikawa ndio matokeo ya shughuli unayofanya leo.
Kama ulikuwa na malengo tofauti na unachokifanya leo, kwa maana ya kwamba unachokifanya leo si kile ulichokuwa umekusudia kuwa ndio malengo yako ya kuwepo hapa duniani basi huajachelewa, unao uwezo wa kuibadilisha hali hiyo kwa jinsi utakavyopenda.
Kimsingi haitakiwi maisha yakuendeshe, bali uyaendeshe, kwani wewe ndio mwenye mamlaka ya kujichagulia maisha uyatakayo na sio maisha yakuchagulie yanavyotaka.
Hebu chunguza mawazo yako ya kina ujue ni kitu gani unachowaza ndani yako, najua sio jambo rahisi sana kutokana na mazoea, lakini ukiamua unaweza kabisa ukajua mawazo yaliyo ndani yako na hapo ndipo utakapo gundua siri kubwa iliyoko katika maisha yako.
Kwa sababu, naamini utagundua kwamba maisha uliyonayo sasa ni matoeo ya kile unachokiwaza na unachokiamini.
Kama ukigundua kuwa mawazo yako yamejaa majuto na maumivu ya matukio ya jana na hofu za kesho, basi yakupasa ubadilishe mfumo wako wa kufikiri, na kuanza kuwaza yale yanayokupa furaha na amani.
Kataa kabisa mawazo ya kukatisha tamaa na jaribu kuwaepuka marafiki wenye mawazo yenye kukatisha tamaa kwani hao ndio maadui wakubwa wa kukukwamisha kufikia malengo yako.
Katika miongoni mwa makala zake kwenye Gazeti la Jitambue, hayati Munga Tehenan, Mtaaluma wa Elimu hii ya utambuzi aliwahi kuandika kuhusiana na nguvu ya mawazo pamoja na subira, aliandika hivi:
“Wakati inawezekana ukawa na hamu ya kuona malengo yako yanatimia mara moja, ukweli ni kwamba hamu yako ya kuleta mabadiliko ya haraka yaweza kukuletea madhara zaidi kuliko faida.
Kwa nini? Kwa sababu unakosa subira na hivyo unafanya mambo yako kinyume na utaratibu wa maumbile. Ukosefu wa subira hutuma ujumbe hasi kwenye mawazo yako ya kina na wakati huohuo unakuwa unafanya mambo kwa kupingana na kanuni ya maumbile. Kwa kufanya hivyo hutumii kile kinachofahamika kama nguvu ya subira. Hii nguvu ya subira yaweza kupatikana kwa hatua mbali mbali zikiongozwa na kufikiri kwako.
Wakati unapokosa subira katika kupata mafanikio, unachofanya ni kuisukuma nafsi yako mbali zaidi kutoka kwenye mafanikio. Wengi wetu hutaka vitu tunavyoamua kuvipata tuvipate hapo hapo, na pale tunapoamua kubadilika ama kuboresha hali zetu, tunataka mabadiliko hayo yatokee mara moja ili mtu aweze kufurahia maisha yetu mapya na kuanza kufurahiya mafanikio.
Lakini sisi ni sehemu ya maumbile na maumbile hayabadili vitu mara moja. Mchakato unaweza kuanza mara moja lakini mabadiliko kamili hayawezi kutokea mara moja.
Kwa vile sisi ni sehemu ya maumbile, ni lazima tufanye kazi kama maumbile yanavyotaka na kwa kufuata taratibu zake.
Linapokuja suala la kufikia malengo yako, mawazo yako ya kina kama yalivyo maumbile yanatakiwa kufanya kazi kwa kupitia mchakato na kukuruhusu kwenda kwa hatua kuelekea kwenye mafanikio ya malengo yako.”
Kwa maelezo hayo tumeona kuwa maisha ni malengo na malengo ndio mafanikio, lakini la msingi tusije tukajiumiza kwa kutaka malengo hayo yatokee mara moja, kuwaza hivyo ni kujiumiza kihisia na kuisababishia miili yetu maumivu na hivyo kuwa mibovu kiafya.
Nov 2, 2008
JE NI NINI MALENGO YAKO?
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Andika Maoni Maoni