0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

http://www.serenahotels.com/serenadaressalaam/default-en.html

Oct 24, 2009

NIKAONA MAITI ZAO!

Ø Kumbe ni mtu na mkewe walionipa shilingi 90 punde tu!
Ø Nikasau kwamba nilikuwa na deni , nikaendelea na maisha
Ø Miaka 17 baadae nikiwa ofisini nikapata mgeni wa ajabu
Ni siku nyingi kidogo, mwaka 1979, lakini ni tukio ambalo liliniuma sana. Ilikuwa vigumu sana kulisahau na lilinifanya nijiulize, inakuwaje Mungu anakuwa mkatili kiasi kile. Lakini bila shaka ilikuwa ni wakati ule wa ufahamu mdogo. Hivi sasa ninafahamu mengi na hasa baada ya kujifunza maarifa haya ya utambuzi.

Ilikuwa ni mwaka 1979 nikiwa nasafiri kutokea Dar es salaam kwenda Arusha. Sijui ilikuwaje, lakini ilitokea. Tuliondoka Dar es salaam saa 12.30 jioni. Wakati ule mabasi yalikuwa yalikuwa yakisafiri jioni na usiku, sio kakma siku hizi.

Nilikuwa ninakwenda Arusha kwenye usaili kwa ajili ya ajira, nikiwa ndio kwanza nimemaliza kidato cha nne. Niliajiriwa moja kwa moja serikalini, kwani siku zile ajira zilikuwa ni za kumwaga. Hata hivyo sikuridhishwa na kazi niliyokuwa nafanya, hivyo niliomba kazi kwenye kampuni moja kule Arusha na niliitwa kwa usaili.

Tulifika mji unaoitwa Korogwe ambao wakati ule ulikuwa ndio mji maarufu kwa hoteli zake katika barabara yote ya Segera hadi Moshi na Arusha. Tulipofika Korogwe basi letu lilisimama kwa ajili ya abiria kupata chakula. Niliingia kwenye hoteli moja ambayo nakumbuka hadi leo kwamba ilikuwa ikiitwa Bamboo. Niliagiza chakula na kula haraka kutokana na muda mfupi wa kula uliotolewa na wenye basi la TTBS ambalo ndilo nililosafiri nalo.

Wakati wa kulipa ndipo niliposhangaa na kuogopa. Niliingiza mkono mifukoni na kukuta kwamba sikuwa na hela. Nilianza kubabaika na mwenye hoteli alisema hawezi kukubali ujinga huo, "Abiria wengine wahuni bwana, anakula na kujifanya kaibiwa, ukikubaliana nao kila siku hasara tu" Mwenye hoteli alisema kwa kudhamiria hasa.

Kulizuka zogo kubwa, huku mwenye hoteli akisema ni lazima anipeleke polisi. Ni kweli alimtuma mmoja wa watumishi wake kwenda kituo cha polisi ili nishughulikiwe……

Hapo Hotelini kulikuwa na bwana mmoja naliyekuwa amekaa pembeni na mkewe na watoto wao wakila. Yule bwana alipoona vile alimtuma mhudumu mmoja aniite. Niliondoka pale kaunta nilipokuwa nabembeleza na kuja kwa yule bwana.

Alikuwa ni kijana mtu mzima kidogo, mwenye miaka kama 50 hivi. Nilimsalimia na aliitikia, nilimsalimia mkewe pia. Yule bwana aliniuliza kisa cha vurugu ile na nilimsimulia. Aliniuliza sasa huko Arusha ningeishi vipi wakati wa usaili wakati nimeibiwa fedha zote na ningerudi vipi Dar. Nilimwambia nilikuwa napanga namna ya kurudi Dar, kama huko polisi ningeaminika.

Kama mzaha vile yule bwana aliniambia kuwa angenipa fedha za kutumia huko Arusha na nikirudi Dar nimrudishie fedha zake. Nakumbuka alinipa shilingi 90 kwa ahadi kwamba nikirudi Dar nimpelekee fedha zake ofisini kwake. Alinielekeza ofisini kwake, mtaa wa Nkuruma na kuniambia kuwa ameamua kunisaidia kwa sababu kila binadamu anahitaji msaada wa mwingine na maisha haya ni mzunguko. Nilimshukuru na kuondoka kukimbilia basini. Basi lilikuwa linanisubiri mimi tu. Nilipanda ndani ya basi na abiria wengine walinipa pole. Tuliondoka Korogwe, lakini haikuchukua muda basi letu lilipata tatizo la pancha ya gurudumu moja la mbele. Ilibidi tuegeshe pembeni ili litengenezwe.
Baada ya matengenezo, tuliondoka kuendelea na safari yetu.

Karibu na mji wa Same kwenye saa saba usiku, basi letu lilisimama ghafla. Abiria walisimama ndani ya basi na kulizuka aina ya kusukumana. Huko nje kulikuwa na ajali. Abiria tulishuka haraka na wengine huko chini walishaanza kupiga mayowe, hasa wanawake. Niliposhuka niliona gari ndogo nyeusi ikiwa imebondeka sana na hapo kando kulikuwa na maiti wawili.

Nilijua ni maiti kwa sababu walikuwa wamefunikwa gubigubi. Halafu kulikuwa na katoto kalikokuwa kanalia sana kakiwa kamefungwa kanga kichwani. Tumwahishe huyu mtoto hapo Same hospitali ameumia, ingawa sio sana. Nilikatazama kale katoto ka kiume kenye umri wa miaka kama mitatu. Kalikuwa kameumie kwenye paji la uso, lakini kalikuwa hai. Bila shaka wale walikuwa ni wazazi wake, kalikuwa yatima tayari. Machozi yalinitoka.

Baada ya kupata msaada na askari wa usalama barabarani kuchukua maiti wale tulipanda basini kuendelea na safari yetu. Kale katoto kalichukuliwa na jamaa fulani waliokuwa na Land Rover ya serikali kukimbizwa hospitalini. Ndani ya Basi mazungumzo yalikuwa ni kuhusu ajali ile tu, hadi tunafika Arusha. Tulichelewa sana kufika Arusha kwani tulifika kwenye saa tano asubuhi, badala ya saa mbili .

Nililala kwenye hoteli rahisi na kufanya usaili kesho yake. Ni hiyu kesho, baada ya usaili niliponunua gazeti ambapo nilipata mshtuko mkubwa ajabu. Kumbe wale watu wawili waliokufa kwenye ajali ile ya Same walikuwa ni yule bwana aliyenisaidia hela na mkewe. Yule mtoto wao ndiye aliyeokoka. Niligundua hilo baada ya kusoma jina lake na jina la kampuni aliponiambia nimpelekee fedha zake nikirudi Dar, pamoja na picha yake, mke na mtoto. Nililia sana, kama mtoto.

Nillishindwa kujua ni kwa nini afe. Nilijiuliza ni nani sasa angemlea mtoto yule? Yalikuwa ni maswali yasiyo na majibu na pengine maswali ya kijinga pia.
Nilijua kwamba nilikuwa na deni, deni la shilingi tisini. Kwa wakati ule shilingi tisini zilikuwa ni sawa na shilingi laki moja za sasa.
Kwa mara ya kwanza sasa nilijiuliza ni kwa nini marehemu yule aliniamini nakuamua kunipa fedha zile. Sikupata jibu.

Nilikata kipande kile cha gazeti la kingereza kilichokuwa na habari ile. Nilichukuwa kipande hicho na kukiweka kwenye Diary yangu. Deni, Ningelipa vipi deni la watu? Nilijikuta nikipiga magoti na kuomba mungu anipe uwezo wa kuja kulilipa deni la mtu yule mwema kwa njia yoyote. 'Mungu naomba uje uniwezeshe kulilipa deni la marehemu kwa sura na namna ujuavyo wewe. Nataka kulilipa deni hili ili nami niwe nimemfanyia jambo marehemu,' niliomba. Nilirejea Dar siku hiyo hiyo.

FUATILIA MKASA HUU WA KUHUZUNISHA..............

3 comments:
Andika Maoni Maoni
  1. Mimi ni mmoja wapo wa watakaoufuatilia mkasa huu hatua kwa hatua.

    Hujambo lakini kaka? Naona majukumu yamechukua nafasi yake sio?

    ReplyDelete
  2. naomba uweke hadithi kila siku katika blog yako.mimi nimdau kutoka kenya

    ReplyDelete
  3. Ni mkasa wa kusikitisha na wenye mengi ya kujifunza nitaendelea kufuatilia!

    ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi