0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Feb 27, 2009

KWENYE NDOA MWANAMKE KAPEWA KISU KWA UPANDE WA MAKALI

Wanawake ni viumbe wa hisia, ni vyema wakasikilizwa

Je umeshawahi kujiuliza ni kwa nini wanawake ndiyo wanao lalamika sana kuhusu ugumu au matatizo ya ndoa kuliko wanaume? Inawezekana ni kwa sababu wanawake ni wakosoaji na wanaotaka zaidi kwenye uhusiano kuliko wanaume, wakati wanaume ni wagumu kutoa?

Hakuna anayeweza kusema hasa ni kwa nini wanawake ndiyo wanaolalamika na pengine hata kuomba talaka katika ndoa ukilinganisha na wanaume. Lakini kwa kuangalia sababu kuu ambayo mara nyingi ndizo zenye kutajwa sana kama chanzo cha kuvunjika kwa ndoa tunaweza kupata “ati-ati” ya jambo lenyewe.

Kabla ya ndoa wanandoa huwa na ndoto tamutamu ambazo siyo rahisi katika ndoa. Kwa kuwa tuna hizi ndoto tamu kuhusu ndoa tunapokuja ingia kwenye ndoa na kugundua kwamba tulichokifikiri hakipo ndipo tunapoanza kuvunjika moyo na kujiuliza kwamba ndoa ina maana. Kwa kawaida tunachotarajia kukipata kabla ya ndoa, tunapoingia kwenye ndoa hatukipati na hili huvuruga kila kitu.

Inaonekana kama matarajio ya wanaume huwa siyo makubwa sana kama yale ya wanawake kabla ya ndoa. Huenda hili huchangia katika kufanya wanaume wasishangazwe sana na kile wanachopambana nacho baada ya ndoa. Inawezekana pia ni kwa sababu wanaume wameshika “mpini” kwenye masuala mengi ya kiuhusiano wakati wanawake wameshika kwenye “makali”.

Hata hivyo badala ya wanandoa kukwaruzana kutokana na kukutana na hali ambayo hawakuwa wanaiota kabla ya ndoa inabidi wajifunze maana ya ndoa wakiwa ndani ya ndoa yenyewe. Inabidi wakubaliane na yale ambayo hawakuwa wameyatarajia na kujifunza kupitia kwayo. Badala ya kukimbia hali halisi ya ndoa ni vema kujifunza na kuikubali ili kwenda nayo na siyo kutegemea hali hiyo ibadilike.

Kwenye ndoa tatizo la fedha hukera sana. Kila ndoa ina tatizo linalo husiana na fedha au kipato. Ama hakuna fedha za kutosha au kuna fedha nyingi zinazo sababisha kisirani cha aina moja au nyingine. Kama ilivyo kwa matarajio suala la fedha au kipato pia lina sura ileile ya mwanamke kushika “makali” na mwanamume kushika “mpini”. Mwanamke hajaweza kumiliki au kumilikishwa kipato na hili humfanya kuwa mwathirika wa migogoro yote ya kifedha au kipato katika ndoa.

Inabidi wanandoa kujua kwamba ndoa yao haiunganishwi kwa fedha na wala kuwa au kutokuwa na fedha hakuna maana ya kuwa ya furaha au kukosa furaha. Wanachotakiwa kukijua wanandoa ni kwamba wao wameoana ili kuunda familia kwa njia ambayo kipato hakitakuwa na nafasi ya kuwaathiri. Inabidi wajue kwamba hawakuoa wala kuolewa na kipato bali wapenzi wao na kuwepo kwa fedha hakuwezi kubadili mpenzi kuwa “mbaya” au “mzuri”. Kushindwa kuelewa tofauti iliyopo kati ya upendo na kipato kunaweza kuwa chanzo cha mgogoro katika ndoa yoyote.

Karibu wanando sita katika kumi wanaolalamika kuhusu ubovu wa ndoa zao huwa wanalalamikia kukosekana kwa mawasiliano kati ya wanandoa. Ni vigumu kama wanandoa hawana mawasiliano ya mara kwa mara ya wazi kuishi katika ndoa imara. Wanawake ni viumbe wa hisia kwa hiyo wao hupenda sana mawasiliano, wakati wanaume ni viumbe wa kutenda na suluhu, hivyo hawajali sana mawasiliano.

Mwanaume anaweza kudhani kuacha shilingi laki moja nyumbani kila siku kunatosha kuimarisha uhusiano. Ndiyo maana wanaume wengi huwa wanasema “nampa kila kitu lakini wapi….” Hiyo “kila kitu” kwao ina maana ya fedha na siyo kauli na kusikiliza au kujali. Katika hali kama hii mwanamke ndiye anayeshika kwenye “makali” wakati mwanaume ameshika kwenye “mpini”.

Matatizo ya ndugu au wazazi kuingilia ndoa ni suala lingine linalotajwa sana katika kuvunjika kwa ndoa nyingi. Bila shaka wengi wetu tunajua kwamba mila na desturi zetu (ni potofu, hata hivyo) ndoa inakuwa ni ya ndugu na wazazi pia, siyo wanandoa peke yao. Lakini kwa bahati mbaya sana katika ndoa nyingi ndugu wa mwanaume ndiyo ambao huingilia ndoa kwa kuwasakama wake katika ndoa hizo wanaume wengi hujikuta wakiwaunga mkono wazazi au ndugu zao dhidi ya wake zao.

Bila shaka haihitaji ufafanuzi mrefu au mkubwa ili mtu kujua kwamba matatizo ya kiunyumba yana mchango mkubwa sana katika kuvuruga ndoa nyingi. Ukitazama sana malalamiko mengi ya kindoa ingawa yamepewa sababu nyingi chimbuko lake ni kwenye unyumba.kwa sababu ni mwiko, tumelelewa na kukulia katika mazingira ambapo tumeambiwa na kuamini kwamba kujadili masuala ya kiunyumba ni mwiko wanandoa wengi hawako tayari kujadili matatizo ya kiunyumba.

Mwanaume anaweza kuzungumzia matatizo ya kinyumba, lakini mwanamke kamwe hana nafasi hiyo. Mwanamke anapojaribu kuzungumzia matatizo hasa kama chanzo ni mwanaume, tafrani kubwa huzuka. Mwanamke yuko tayari kufanya subira kama mume ndiye mwenye matatizo hayo, lakini kama mwenye matatizo ni mke, mume haoni ajabu kutoka nje kwa kisingizio hicho. Hapa mila na desturi zinampa mwanamke “kisu” kwa upande wa makali na mwanaume kwa upande wa “mpini”

Katika hali hii ni wazi mara nyingi mwanamke atakuwa anaonekana kuwa ndiye mwenye kulalamika sana kuhusu matatizo ya kindoa ukilinganisha na mwanaume . lakini kwa ndani zaidi mwanaume ndiye anaonekana kuwa ndiyo sababu ya matatizo hayo kwa sehemu kubwa.

9 comments:
Andika Maoni Maoni
 1. Naweza kukubaliana nawe kuwa ndoa nyingi huvunjika kwa sababu kunakuwa na ukosekanaji wa kutoongea/kutojadiliana kutopeana mawazo. Kama ulivyosema wengi wanaume huzani pesa hutibu kila kitu kumbe ni kinyume kabisa.sijui nimechemsha au?

  ReplyDelete
 2. siku za mwanzo dada na kaka wanapokutana kila mmoja huonyesha kumjali mwenzie hasa mwanamume.Siku zinakwenda hatimaye ndoa inatangazwa na kufungwa.
  Mwanzoni mwa ndoa kila mwanandoa huonyesha kutojali tofauti zao kwa kuwa tu wamefunikwa na blanketi zito liitwalo "UPENDO"
  Blanketi huanza kuchakaa,kasi ya kuchakaa hutegemea matumizi ya wanandoa.Wakilitumia vibaya huchakaa mapema zaidi.Wengine ujaribu kuweka viraka lkn baada ya muda blanketi linakuwa halifai,linatupwa.
  Wanaochangia zaidi kuchakaza blanketi ni majirani na ndugu hasa wa kiume wanaoruhusiwa na wanandoa kuingia chumbani na kulitumia blanketi watakavyo.
  Mwanamke ndiye mwathirika mkuu kwa kuwa jamii inaamini kuwa ndiye anayepaswa kutunza na kufua hilo blanketi.Jamii inamuona mwanamke ndiye chanzo cha matatizo ndani ya ndoa.
  Ukweli niuonao mimi ni kuwa wanaume wengi ndo chanzo cha mfarakano ktk ndoa nyingi.Mwanamke ni rahisi kubadilika na kukubali mapungufu ya mwanaume kwa sababu wao hutumia mwiliwa hisia zaidi kuliko mwili wa Akili.
  Ushauri wangu ni huu,Mwanandoa yeyote yeye na mwenzake ni kama wametoka ktk sayari tofauti kwa hiyo kila mwanandoa ana tabia zake ambazo hazifanani kabisa na za mwenzake.Ni jukumu la kila mwanandoa kuzikubali tofauti za mwenzake na kujadiliana mambo yao wao wawili tu kwa ukweli na uwazi.Mwanandoa yeyote asijaribu kumlazimisha mwenzie afanane naye kitabia au matendo,ninaamini kufanya hivyo kutaleta migogoro na hatimaye kuvunjika kwa ndoa.

  ReplyDelete
 3. jambo jingine ni kuhusu Yasinta,nimesoma maoni yako lkn nimeshangazwa na maneno haya"au nimechemsha?.Inaonekana kama vile haujiamini na maoni yako na unahitaji mtu akukamilishe kuwa "haujachemsha'
  MAMA MAONI YAKO NI MAZURI NA YAMEJITOSHELEZA,KWANINI HAUJIAMINI AU NIMEKUELEWA TOFAUTI?

  ReplyDelete
 4. Hahahahaaaa. Nianze na Kaka Fred hapo. Umenikumbusha jirani yetu aliyekuwa akimchapa mtoto huku akimtusi na tulipomuuliza kaiba nini? Akasema amemtukana mtu. Nikamwambia mbona wewe tayari ushamtukana matusi yote niyajuayo? Yaani anatatua tatizo kwa kutumia njia iliyoleteleza tatizo. Sasa Kaka Fred umesema kweli kuwa maoni ya Da Yasinta yamejitosheleza na umeshangazwa na yeye kuuliza kama amechemka, kisha nawe pamoja na kuonesha kuwa umemuelewa na uko sahihi ukamalizia na swali kuwa "au nimekuelewa tofauti"? Ndio raha ya blogs hizi.
  Nikirejea kwenye mada, kaka Fred na Da Yasinta wamechangia vema. Mfano wa "blanketi upendo" alilosema Kaka Fred ni mwema na naamini wengi wanauona kwa kuwa ukweli umo ndani mwake.
  Blessings

  ReplyDelete
 5. Asante mzee wa changamoto ndo raha ya kuandika unachokijua na ukikosea unajifunza kutoka kwa mtu mwingine.Umenifundisha kitu kikubwa sana mzee.

  ReplyDelete
 6. Sikujua kuwa ninatumia njia ile ile aliyoikosea Yasinta.Big up mzee wa changmoto nimejifunza kitu kikubwa sana leo.

  ReplyDelete
 7. Sasa itabidi nioe ili kuitumia elimu hii kwa vitendo.

  ReplyDelete
 8. Kaka Bwaya unanirudisha kwenye swali lako kuwa ndoa ni nini?

  ReplyDelete
 9. Kaka Bwaya na Mzee wa changamoto.
  Kiutambuzi, yaani mtu akishajitambua anao uwezo wa kuishi bila kuoa kabisa kwani atakuwa na uwezo mkubwa wa kudhibiti mihemko ya hisia za kimapenzi au tamaa ya kufanya ngono.
  Tatizo liko hapa, ni hivi, wakati mwingine kijana kuonekana uko single au mseja inaleta mushkeli katika jamii na pia wale dada zetu wenye kutaka kuolewa hawatasita kujisogeza karibu yako na kuleta usumbufu kidogo, kwa hiyo nadhani ili kuepuka yote mawili ni vyema kuoa kwani kidogo itajenga heshma.
  Ingawa si lazima kama utakuwa na uwezo wa kupuuza kero na vijineno vidogo vidogo.
  Lakini ki ukweli ndoa haiwezi kumpa shida mtu aliyejitambua.

  Kaka Katawa mfano wako wa kufananisha ndoa na blanketi nimeupenda sana, jana kuna jamaa yangu mmoja nilikuwa nae kwenye mghahawa wa internet akaamua a-print maoni yako ili ampelekee mkewe, nadhani ule ujumbe umemgusa.
  Kwa kweli umenifikirisha sana.
  Ahsante sana.

  Dada Yasinta, Karibu sana, hapa huwa tunaibua hoja zenye kuleta changamoto, nilimiss sana kibaraza chako, nadhani umetuandalia vitu vizuri kutoka Ruhuwiko

  ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi