0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

http://www.serenahotels.com/serenadaressalaam/default-en.html

Jan 11, 2009

JE MAISHA YANA MAANA GANI KWETU?

Kwanza naomba nikwambie kwamba, tofauti na unavyoweza kuamini, maisha tunayoishi hakika siyo yetu, siyo maisha tunayoyapenda. Tunaishi maisha ya kimazoea zaidi na hivyo, amani na utulivu hutuponyoka sana. Hata hivyo, lengo langu leo ni kuzungumzia kidogo matumizi ya nguvu na tafsiri yake katika maisha halisi ya watu wenye ukomavu.

Hakuna kati yetu ambaye ni kitovu cha ulimwengu, isipokuwa ni kwamba kila mmoja wetu ni sehemu muhimu ya ulimwengu.
Maisha ni magumu na yanaumiza wakati unapokosea namna ya kuyatafsiri, lakini, ukweli ni kwamba, maisha ni mazuri kwa kiasi cha kutosha.

Watu, mara kwa mara hushtushwa na maovu yaliyotapakaa katika jamii. Hakuna mtu ambaye anaweza kujigamba kwamba, hawezi kuja kukumbwa na mikasa, hatari na wala kutofautiana na watu wengine.
Matendo na maneno yetu vinaweza kuwa tofauti. Lakini, kumbuka tu kwamba, sisi binadamu tu zaidi ya miili yetu hii tuliyonayo.
Chuki na ujinga haviwezi kuondolewa kwa chuki na ujinga zaidi.

Uvumilivu na heshima hutakiwa kufundishwa mapema katika maisha, kuwa jambo muhimu katika maisha ya kawaida ya kifamilia, makazini, mashuleni na kadhalika.
Vitendo huongea zaidi kuliko maneno, na watoto wetu wanapotusikia tunaongea jambo halafu tunatenda tofauti, tunakuwa tunawachanganya. Mafunzo muhimu yanakuwa yamepotelea hewani.
Matatizo mengi ya kijamii siku hizi yanatokana na chuki, ujinga na upeo mdogo. Sasa ni muda mwafaka wa kuitokomeza chuki, ujinga na kuyatazama mambo kimazoea!

Kuondoa chuki ni jukumu la kila mmoja wetu. Tufanyeje ili kutimiza haya? Hatuna budi kuwa macho na kila tulifanyalo. Hatupaswi kulalamika tupatapo matatizo, badala yake tunatakiwa kuyatatua kwa kufanya matendo ya kujenga na si ya kubomoa.

Tunatafuta suluhisho la matatizo katikati ya maumivu. Tukiwa katika mchakato huo tunaweza kujiponya na pia kuwaponya wengine.
Tunakuwa mashujaa kiasi cha kupambana na mauti na kujiuliza ni kitu gani kilicho muhimu kwetu, ni kitu gani hasa tunataka kukitimiza kabla hatujafa.

Hatutakiwi kuhubiri wema tu bali hatuna budi kuwa wema.
Tuweze kuiweka hofu pembeni, na kuwaendea wengine ambao wanateseka. Hatupaswi kufumba macho tuyaonapo majanga yakiikodolea macho jamii. Hatuna budi kutafuta njia za kuwasaidia wengine.

Wanasema mpende mwenzio au mtoto wako bila masharti, kwa sababu huo ndiyo upendo wa kweli.
Lakini sisi sote tunajua kwamba si rahisi kutimiza hivyo.
Hatuna budi kuheshimu tofauti zilizopo kati yetu, na kumsikiliza mtu mwingine anasemaje.
Tusingetegemea tupate watu tunaofanana nao kabisa, binadamu tumeumbwa tofauti.

Huwa najiuliza, kama dunia hii ingekuwa na upendo tungeshuhudia kweli hivi vita vinavyoendelea kule Palestina, Iraq, Somalia, Sudan na kwingineko?
Haya magomvi tunayoyashuhudia ya vita vya wenyewe kwa wenyewe, vita baina ya nchi na nchi, chuki, dhulma, fitna, usengenyaji, na mengine yanayofanana na hayo, yanatokana na kukosekana kwa upendo miongoni mwa jamii.

Changamoto tulionayo binadamu, ni kuishi katika dunia ambayo ina watu tulio tofauti mno, tamaduni tofauti, ladha tofauti, na hisia tofauti.
Pia linafuata suala la heshima. Mtu anayejiheshimu, kamwe hawezi kupata mawazo ya kuwaumiza wengine; akiwaumiza kinakuwa ni kioja.

Hatuna uwezo wa kudhibiti mwenendo wa kila binadamu, ila sisi wenyewe tunaweza kudhibiti mienendo yetu mibaya dhidi ya binadamu wengine.

Marekani kwa mfano, nchi ya watu wanaodaiwa kuwa huru kwa kile kinachoitwa demokrasia, na nchi ya mashujaa, haina budi kuanza kutafuta suluhisho la muda mrefu la matatizo ya jamii hiyo.
Pamoja na demokrasia na maguvu, watu wengi nchini humo wanaishi katika hofu na mshaka, katika kushindwa kujua kwamba, maisha ya kila mtu yatabadilishwa na mtu mwenyewe na siyo utajiri na mabavu ya jamii.

Mtu uliyemcheka leo, atachukua hasira zake na kwenda nazo kwa mnyonge wake kuzimiminia huko.
Kumbuka kwa kufanya hivyo, wewe unakuwa ni sehemu ya tatizo hilo, sehemu ya nguvu za maumivu zinazotembea ulimwenguni kote zikipokezanwa.

Jicho kwa jicho. Zima moto kwa moto. Jibu ukatili kwa ukatili. Mkifanya hivi, kila mmoja anakosa, inakuwa ni sandakalawe.
Na ndivyo dunia inavyoendeshwa leo, jamii zote ziko hivyo. Nchi inapotangaza vita na nchi nyingine inafanya hivyo kama sifa, ujinga na choyo.

Mtu mwenye mafanikio si yule mwenye nyumba nzuri au kazi nzuri.
Mafanikio huja kutoka ndani.
Huja kutokana na kuishi. Kuwa na mafanikio maana yake ni kuishi katika dunia ambayo mema na mabaya yamejaa tele, na bado tunapambana ili kuwa washindi, bila kujali matatizo yanayotuzingira.

Kamwe washindi hawakati tamaa. Hujaribu mikakati tofauti tofauti.
Mara kwa mara wanapenda kuthubutu na kujaribu.
Inahitaji imani kubwa. Inahitaji upendo mkubwa.
Inahitaji kufikiri kwa makini kwa kutumia akili nyingi.
Si kufuata mkumbo wa watu wengi wanavyotaka kwa kuogopa kuchekwa.
Hofu huturudisha sana nyuma, na ukweli hutuweka huru.

Ndio tumeuanza mwaka mpya wa 2009, Je unategemea kufanya nini ili kuifanya dunia hii iwe ni mahali pazuri zaidi? Ni lazima ujiulize swali hilo kama kweli unataka kuwa na haki ya kusema uliwahi kutumia mwili huu hapa duniani.
Dunia imebadilishwa na watu wachache wenye mioyo mikubwa na ndoto kubwa. Kamwe usiudharau uwezo wako, fanya tena na tena.

Hata wewe una uwezo wa kuongeza kitu hapa duniani!


5 comments:
Andika Maoni Maoni
  1. "Lucky Dube aliimba katika wimbo wake wa RESPECT akisema "respect me for who i am and not what i am" Ukiusikiliza huo wimbo anazungumzia kumheshimu mtu kwa kuwa ni BINADAMU na si kwa kuwa ana hiki ama kile ama anatokea huku ama anaweza kufanya hivi. Na hilo ndilo tunalopungukiwa sasa. Hakuna heshima na bila heshima hakutakuwa na upendo wa dhati na maana ya maisha ya mtu mwingine kwako itakuwa finyu na hapo ndipo utakapoona kama hana thamani na kitakachofuata hapo ni kulingana na uwezo wako. Tumekosa heshima na hilo latugharimu saana. Kama ulivyosema kuhusu Marekani, gharama ya hofu hapa ni kubwa na thamani ya maisha ya wananchi wake sasa ni ndogo mno. Unaposafiri unapekuliwa kama vile kila msafiri ni gaidi, unapoingia sehemu mbalimbali huna thamani na heshima maana utachambuliwa na kupitishwa kwenye scanners kama wewe ni gaidi. Hapo hakuna heshima na thamani ya maisha maana huonekani kuyathamini maisha yako na ya mwenzako na ndio maana unapekuliwa. Hakuna imani na hilo latupeleka pabaya.
    Pengine UPENDO ukirejeshwa patakuwa mahala pema zaidi kuishi. Ziggy Marley alisema LOVE IS MY RELIGION na akamalizia kusema "you can take it or leave it, you don't have to beleive it"
    Nami nimesema yale niaminiyo, waweza kuamini ama kutoamini maana ni sauala la mtazamo.
    Blessings

    ReplyDelete
  2. "Lucky Dube aliimba katika wimbo wake wa RESPECT akisema "respect me for who i am and not what i am" Ukiusikiliza huo wimbo anazungumzia kumheshimu mtu kwa kuwa ni BINADAMU na si kwa kuwa ana hiki ama kile ama anatokea huku ama anaweza kufanya hivi. Na hilo ndilo tunalopungukiwa sasa. Hakuna heshima na bila heshima hakutakuwa na upendo wa dhati na maana ya maisha ya mtu mwingine kwako itakuwa finyu na hapo ndipo utakapoona kama hana thamani na kitakachofuata hapo ni kulingana na uwezo wako. Tumekosa heshima na hilo latugharimu saana. Kama ulivyosema kuhusu Marekani, gharama ya hofu hapa ni kubwa na thamani ya maisha ya wananchi wake sasa ni ndogo mno. Unaposafiri unapekuliwa kama vile kila msafiri ni gaidi, unapoingia sehemu mbalimbali huna thamani na heshima maana utachambuliwa na kupitishwa kwenye scanners kama wewe ni gaidi. Hapo hakuna heshima na thamani ya maisha maana huonekani kuyathamini maisha yako na ya mwenzako na ndio maana unapekuliwa. Hakuna imani na hilo latupeleka pabaya.
    Pengine UPENDO ukirejeshwa patakuwa mahala pema zaidi kuishi. Ziggy Marley alisema LOVE IS MY RELIGION na akamalizia kusema "you can take it or leave it, you don't have to beleive it"
    Nami nimesema yale niaminiyo, waweza kuamini ama kutoamini maana ni sauala la mtazamo.
    Blessings

    ReplyDelete
  3. Ni kweli maisha ni mazuri ukiamua hivyo. Haijalishi unatenda nini au unatendewa nini. Wewe pekee ndiyo maisha. Matukio yote yanayotokea ukiatazama kwa milango ya fahamu yatakuwa na pande mbili, lakini ukitoka nje ya miili yako hutaona kitu choche. Changamoto tuliyo nayo ni "kukua"

    ReplyDelete
  4. haya maoni ya mtua asiyejulikana, yamenichanganya kidogo, naomba ufafanuzi tafadhali.

    Umesema, ngoja ninukuu, "matukio yote yanayotokea ukiyatazama kwa milango ya fahamu yatakuwa na pande mbili, lakini ukitoka nje ya MIILI yako hutaona kitu chochote"

    Mwisho wa kunukuu.

    Hebu mwenzetu tujuze hiyo miili ni ipi? maana mimi nafahamu kwamba ninao mwili mmoja.

    Hiyo mingine ni ipi na iko mingapi kwa idadi?

    Ombi: wakati mwingine ukichangia kwenye hivi vibaraza vyetu ni bora ukijitambulisha ili tufahamiane!

    ReplyDelete
  5. Makala nzuri sana katika kujielimisha. Asante ndugu yangu Kaluse. Nisiongeze neno.

    ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi