Ninapozungumzia mawazo, ninamaanisha kile ambacho kinapita kichwani mwetu kila nukta. Kwa kawaida mawazo yamegawanywa katika makundi mawili.
Mawazo ya kawaida
Mawazo ya kina
Kuna tofauti kubwa kati ya mawazo ya kawaida na yale ya kina. Mawazo ya kawaida ndiyo unayotumia sasa hivi. Haya ndiyo yanayotuwezesha kuwa na utashi wa kuchagua, kwa mfano mavazi ya kuvaa, vyakula tunavyokula, vitabu tunavyosoma na kadhalika na kadhalika. Kwa kawaida maamuzi yote tunayofanya yanaratibiwa na mawazo haya ya kawaida. Pia ndiyo yanayoratibu hii milango mitano ya fahamu, yaani kugusa, kunusa, kuona, kusikia na kuonja.
Mawazo haya yanafanya kazi unapokuwa macho. Unapolala yanapumzika. Huna uwezo wa kuyazuia mawazo haya. Inakadiriwa kwamba, kwa siku moja binadamu huwaza au hupitiwa na mawazo 50,000 mpaka 60,000.
Kwa upande wa mawazo ya kina huwa hayapumziki, hata kama umelala yanaendelea kufanya kazi (hayajawahi kupumzika).
Yalianza kuhifadhi kumbukumbu tangu ulipokuwa tumboni. Wataalamu wanasema kwamba, mawazo haya huanza kuhifadhi kumbukumbu mimba inapofikisha miezi minane na nusu (hupokea sauti kwa njia ya mawimbi) na kuzihifadhi kwa ajili ya matumizi (rejea) ya baadaye.
Mawazo ya kina yana nguvu kubwa sana. Wataalamu wanasema kwamba, zaidi ya miaka kumi iliyopita, kompyuta iliyokuwa na nguvu kupita zote, ilikuwa na uwezo wa kufanya mikokotoo milioni 400 kwa sekunde moja. Ili kompyuta hii iweze kufikia uwezo wa mawazo ya kina ya dakika moja, inabidi ifanye mikokotoo ya hii kwa miaka 100.
Mawazo ya kina hufanyia kazi kile ambacho kimeombwa na mawazo ya kawaida (imani zetu). Imani ni mambo anayokubali mtu kuwa ni ya kweli na anapaswa kuyaheshimu, au ni maoni ya moyo yanayomfanya mtu awe na mkabala fulani juu ya jambo au kitu. Kanuni ya ufanyaji kazi wa mawazo yetu ya kina ni imani zetu (kanuni hii haivunjwi kwani ni ya kimaumbile).
Kwa kawaida, matukio, hali zetu za hisia na matendo yetu ni majibu ya mawazo yetu ya kina kwa mawazo yetu ya kawaida. Mfano: unapoamini katika ushirikina au hofu, matokeo yake yanakuwa ni kulogwa, kuugua, hofu na kukata tamaa. Lakini chenye kupelekea hali hizo siyo ushirikina au hofu, bali imani yako kwenye hofu hizo.
Mawazo haya hayana akili, hayachagui kibaya au kizuri, hayana huruma, yanafanyia kazi chochote yalichopewa na mawazo ya kawaida. Wale wenye uwezo wa kutumia vizuri mawazo yao ya kina, wamefanikiwa sana maishani, ingawa siyo kwa mali bali kwa kuwa na furaha au vyote viwili (fikra zao ni nzuri na wamemudu kufuta fikra mbaya kwenye mawazo yao).
Mawazo ya kina ndiyo yanayobainisha aina ya maisha tunayoishi. Nikikuambia kwamba maisha unayoishi umechagua mwenyewe usikasirike, huo ndiyo ukweli usio na doa.
makala hii imeandaliwa kwa msaada wa Dr. John Simbile
No comments:
Andika Maoni Maoni