Je unaweza kuhisi kuwa hawa wanafikiri kuhusu nini?
Jana nilikuwa na mtambuzi mwenzangu, Dr. John, tulizungumza mambo mengi sana juu ya maarifa haya ya utambuzi. Na kutokana na mazungumzo yetu ndio nikapata wazo la kuandika makala hii, ili kuweka sawa ile makala ya kwanza iliyozungumzia nguvu ya mawazo yanayopita vichwani mwetu,
Leo nimeona nizungumzie kuhusu kufikiri kwetu na jinsi kunavyoakisi kwa kiasi kikubwa maisha tunayoishi. Kwa kawaida binadamu huwa anafikiri. Huwezi kuzuia milango yako ya fahamu isifanye kazi (ukiweza kufanya hivyo unakufa). Kufikiri kwetu huwa ni tofauti kutegemea malezi na mazingira tuliyokulia.
Ukweli huwa hatujui kama tunafikiri mpaka tuambiwe au tukumbushwe. Thamani yetu iko ndani mwetu, ni jinsi tunavyofikiri. Lakini kwa kutokujua kwetu, tunafikiri thamani yetu iko nje ( vitu, mali au umaarufu). Mfano: waziri, mkurugenzi, hatusemi ukatae kuitwa waziri, la hasha. Bali jiulize, unakitumiaje hicho kibandiko? Kuumiza au kuwaumiza wengine? Kumbuka, kibandiko kibaya kuliko vyote ni ndoa.
Jikubali kimwili, kiakili na kihisia kwamba umekamilika na unastahili na thamani yako ni sawa na mtu mwingine yoyote bila kujali kigezo chochote cha mali, utajiri au umaarufu. Tunapaswa kumsikiliza kila mtu bila kujali alivyo. Ukiwa na kijicho, visasi, majivuno, kero, huwezi kuibaini thamani yako. Hakuna mtu au vitu vinavyoweza kuiongeza au kuipunguza thamani yetu hadi pale sisi tutakapotaka iwe hivyo (hii itatokana tu na jinsi tunavyofikiri). Mfumo wa kufikiri una uwezo wa kuhifadhi kila kitu kinachokupitia kwenye maisha yako.
Mfumo wa kufikiri upo mmoja ila umegawanyika katika sehemu mbili:
( i )Mfumo wa kufikiri vibaya
hebu tutajie mambo au matukio uliyokuwa unayafikiria siku mbili au tatu zilizopita. Bila shaka yote ni mabaya na yenye kuumiza. Ni mfumo ambao mtu anawaza au kufikiri mambo ambayo yanamuumiza yeye au mtu mwingine. Katika mfumo huu, mtu anazijaza fikra zake na picha (taswira) zenye matarajio na matukio ya kuumiza, maanguko, wasiwasi, hofu, hasira, kukata tamaa, visasi, majuto, kinyongo, chuki, fitina, kujishusha, kujikosoa n.k.
Mfumo huu ndiyo unaoongoza maisha ya mwanadamu. Anafikiri vibaya kwa sababu anaongozwa na mwili. Ndiyo maana majuto na hofu haviishi. Amefundishwa na kuzoeshwa kupokea, kutafsiri na kusema au kuona kirahisi zaidi yale yaliyo mabaya tu. Ni bahati sana kumkuta anafikria mambo mazuri kwa muda mrefu wa siku. Anapenda kutazama upande mbaya wa tukio au binadamu mwingine. Mfano: mtu anaweza kufanya yaliyo sahihi kumi. Ikitokea akakosea moja, kwa mujibu wa mfumo wetu wa kufikri, hili moja baya ndiyo litatamalaki na kupewa nguvu. Yale kumi yatafutwa haraka sana kwenye kumbukumbu.
Kwa kutokujua sisi ni nani, matokeo yake miili hii badala ya kuimiliki, yenyewe ndiyo hutumiliki na kuwa mali yake. Kumbuka miili hii haitumii akili yetu, inatumia akili tuliyopewa. Baada ya kufanya yale yanayotokana na kufikiri vibaya (kwa matakwa ya mwili), ndipo sisi hujitokeza nyuma ya miili hiyo na kuanza kujuta na kulaumu. Lakini baada ya muda, miili hututhibiti tena na kuturudisha kwenye mazoea yetu na hivyo kurejea kwenye mateso ya maisha. Kwa mfano: unapoachwa na mume au mke unaumia sana. Kinachokuumiza siyo kuachwa, kinachokuumiza ni ile tafsiri uliyofundishwa kwamba kuachwa ni kubaya. Tukio siyo tatizo, tatizo ni tafsiri yako. Kila tatizo (changamoto) unayoipata, fahamu kwamba ufumbuzi wake unao, kama huna, haliwezi kukutokea, na kama utalikataa, ujue unatafuta tatizo jingine jipya na lazima utaumia tu. Ukweli ni kwamba, furaha, amani na utulivu haviwezi kustawi katika mfumo huu wa kufikiri vibaya.
( ii ) Mfumo wa kufikiri vizuri:
ni ule mfumo ambao mtu anawaza au kufikiri mambo ambayo hayamuumizi yeye wala mtu mwingine. Ni kuzijaza fikra zetu na masuala, matukio, matarajio na picha/taswira zenye kutupa moyo, matumaini na faraja. Tunapaswa kuishi kwa wakati na mahali tulipo tu, sasa hivi, hapa ulipo. Hakuna kitu kinachoitwa mambo mengi ( bize), timiza kila jambo kwa wakati wake. Mfumo huu ni mgeni kwetu au hatuufahamu.
Huna uwezo wa kuzuia mawazo yasiingie kwenye mfumo wako wa kufikiri. Mawazo yote mabaya kwa mazuri yataingia kwenye mfumo wako wa kufikiri ( mfano: mawazo ya kuiba, kusaidia, kuzini, kufukuzwa kazi, kudhulumiwa, kudhulumu, kupigana, kusali/kuswali, kujiua, kupata kazi, kufanikiwa n.k.). Swali kubwa la kujiuliza ni hili: Mawazo hayo yanapoingia kwenye mfumo wako wa kufikiri, wewe unatoa nafasi na muda kwa mawazo yapi?
Kwa kawaida, huwa tunatoa nafasi na muda kwa mawazo mabaya (yale ambayo hatuyataki, yale yanayotuumiza, yale yanayowaumiza watu wengine). Kwa kutoa nafasiI na muda kwa mawazo hayo, tunayavuta yaje kwetu, na hivyo yanatutokea kweli. Lakini pia, usitoe nafasi na muda kwa kukataa jambo usilolitaka. Mfano, sitaki kuolewa na askari. Ukweli ni kwamba, utaolewa na askari. Kwa nini usitoe nafasi na muda kwa mtu unayetaka akuoe?
Huna budi kubadili mfumo wako wa kufikiri. Toa nafasi na muda kwa yale tu unayoyataka, kwa yale tu yanayokupa nafuu, kwa yale tu ambayo hayakuumizi na kwa yale tu ambayo hayamuumizi mtu mwingine. Kumbuka kila jambo lina pande mbili, upande mzuri na upande mbaya. Pande zote hizi mbili ziko sawa. Mfano, bila utajiri kusingekuwa na umaskini, bila kupoteza kazi kusingekuwa na kupata kazi, bila kuzaliwa kusingekuwa na kufa. Hakuna jambo hata moja hapa duniani ambalo lina upande mmoja tu. Kama lipo, binadamu halijui. Hivyo, hakuna jambo baya wala zuri ila wewe unasemaje!!!
Katika kila jambo au tukio, kinachoanza ni kufikiri, tunapofikiri tunapata hisia ambazo zinatupelekea kutenda jambo fulani (mawazo – hisia – kitendo). Baada ya kutenda jambo hilo tunakuwa sisi, sisi akina nani? (Sisi wapole, sisi wakorofi, sisi wakatili, sisi waungwana, sisi wagomvi n.k.). kila wakati, hakikisha unachofikiri, unachowaza, unachosema au unachotenda hakikuumizi wewe au mtu mwingine. kumbuka, maumbile hayajui samahani, hasira au kulewa, yanachojua ni kile ulichotenda. Jitahidi kuwa taa kila unapokuwa ila hakikisha miili yako iko sawa. Kuna uhusiano mkubwa kati ya mwili wa akili, wa hisia na huu unaoonekana. (Mada hii nitaizungumzia baadae kwajinsi ninavyoendelea kuandika makala juu ya maarifa haya) Linaanza wazo au fikra kwenye mwili wa akili, wazo hili linazaa hisia fulani. Mwili unaoonekana unajibu kwa kutoa vichocheo ili kuulinda mwili. Kwa kuwa vichocheo hivi hutolewa wakati wa dharula tu, hivyo kuendelea kuchokozeka kihisia kutokana na kufikiri vibaya, huudhuru/kuumiza mwili huu unaoonekana na hivyo kusababisha magonjwa kama vidonda vya tumbo na shinikizo la damu.
Jiulize, kutokana na kufikiri kwako, maisha yako ni kero kwako kwa kiasi gani? Lakini pia ni kero kwa wengine kwa kiasi gani? Huoni kwamba kufikiri kwako ni muhimu sana, huoni kwamba ndiyo njia muhimu ya kukupa amani, furaha na ridhiko katika maisha yako? Ukiweza kuratibu mwili wako wa akili, ni rahisi zaidi kuratibu miili mingine. Ukiamka huna furaha, jiulize ni mwili gani unakunyima furaha. Kufikiri vizuri ndiyo hatua ya kwanza ya kuelekea kupata furaha ya kweli. Ili uipate furaha ni lazima usafiri pia, na ukiwa njiani utaipata, na ukiipata inapoteza maana (kinakuwa kitu cha kawaida). Furaha unayo ndani, usiitafutie nje. Kumbuka tumekuja duniani kutafuta furaha kwa kufanya jambo tunalolipenda zaidi (lengo).
Ili umudu kuutumia mwili wako wa akili vizuri, unapaswa:
(I) Kujua kwamba, unafikiri. lakini siyo kufikiri tu, bali kufikiri vizuri. kufikiri vizuri maana yake ni kuruhusu fikra zenye kukupa furaha na kuwapa wengine furaha, kuingia kwenye mfumo wako mkuu wa kufikiri.
(II) Kujua kwamba, mazingira na watu wengine hawapaswi kukupangia ufikirie kitu gani, bali wewe ndiye mwamuzi wa unachotaka kufikiri.
(III) Kujua kwamba, unapaswa kufikiria kuhusu yale unayotaka, na siyo usiyoyataka. Kama jambo hulitaki, unalitafutia nini?
(IV) Jua kwamba, kuna mambo ambayo yamewekwa kichwani mwako kupitia mawazo yako ya kina. Yalianza kuwekwa tangu ukiwa tumboni mwa mama yako, mengine yaliwekwa wakati wa makuzi yako, ambayo ndiyo leo unayaita akili yako. Kama yanakukera au kuwakera wengine, jua kwamba hayakufai.
Yatoe. Utayatoaje? Tukutane wakati mwingine.
No comments:
Andika Maoni Maoni