0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Nov 29, 2008

HOFU ZA MAISHA, SAWA, LAKINI........


Kuwa na hofu hutuwezesha kuchukuwa tahadhari, iwapo tutatafsiri matukio yanayotutokea bila kuongeza chumvi.Nilipozungumzia kuhusu hofu na kuwataka watu wasihofie matukio ya kimaisha na kujitahidi kuyapokea kama yanavyokuja na kutulia kabla hawajiuliza wafanye nini, sikuwa na maana kwamba binadamu hatakiwi kuwa na hofu.

Ukweli ni kwamba hofu ni kama kitu cha kimaumbile ambacho humfanya Binadamu aweze kuishi.
Bila kuwa na hofu kabisa , kuna uwezekano hapo kuna tatizo la kiakili. Hii ni kwa sababu hofu kama hofu humsaidia binadamu kuweza kukwepa maafa na kusonga mbele.

Kuna zile hofu ,ambazo hizo tunaweza kusema ni kama lazima ziwepo, Kwa maisha haya na maumbile yetu binadamu, hizi hatuwezi kuzikwepa. Lakini hofu ambazo tunasema ni tatizo, ni zile zinazotokana na kuongeza chumvi mambo au kutafsiri mambo ndivyo sivyo. Kwa nini nasema hofu ni lazima kwa binadamu?

Hebu jaribu kuzunguka ukiwauliza watu kama wako tayari kuondolewa hisia za maumivu. Iwapo atatokea mtu na kukwambia kwamba angependa aondolewe hisia za maumivu kwenye mwili wake , yaani asihisi maumivu. Bila shaka jibu hilo litakuwa limetokana na ujinga, kwa nini?

Kwa sababu bila kuwa na hisia za maumivu ni vigumu kwako na kwangu kuishi. Maumivu ni muhimu kwa binadamu ili tuishi. Hofu ni kama hisia za maumivu, pia nayo ni muhimu. Kwa kuhofia jambo halisi tunaweza kujilinda na madhara au uharibufu wake.

Mtu anaweza kutamani kuingia baa na kunywa pombe na kula kuku, lakini akipata hofu kuwa atapunguza fedha za ada za watoto, itamfanya aachane na wazo hilo.
Mtu anaweza kumtamani sana mwanamke, lakini hofu kuwa anaweza kuwa mke wa mtu, (Je watu wanajali kuhusu hilo kweli?) au hofu kwamba ameathirika kwa ukimwi, huweza kumzuia kufanya jambo hilo ambalo matokeo yake ingekuwa ni maumivu.

Hali inapotafsiriwa vibaya huleta hofu isiyo na maana. Kwa mfano mtu anaweza kuwa na kijipu usoni, lakini kwa hofu zake kuhusu kansa akadhani amepata kansa, anaweza kuingia kwenye hofu na kuwatisha wengine walio karibu yake na kusababisha madhara mengi na makubwa..

Kuna watu ambao wakifukzwa kazi hufanya familia ione kama vile dunia imesimama na kila kitu kimepoteza maana. Ukweli ni kwamba mtu akipoteza kazi anaweza kuingia kwenye hofu ili aweze kurekebisha hali hiyo. Hii ni hali ya kawaida, lakini anapoanza kuwafanya wengine waamini kwamba, huo ni mwisho wa maisha , hapa tunasema hofu hiyo ni ya ujinga.

Tunapoingia kwenye hofu kimaumbile tunajiandaa kupambaana na kile kinachotuhofisha au tunajiandaa kukikimbia. Wakati mwingine tunatulia na kukusanya nguvu zetu zote ili kukikabili kile kinachotutisha.

Haiwezekeni hata hivyo katika hali halisi ya maisha kukimbia vile vitu vinavyotutisha. inabidi tupambane navyo, kama ni kufuzwa kazi inabidi tupambane na kufukuzwa huko kwa kukubali halafu tuamue kukusanya nguvu na kuanza kutafuta kazi mahali pengine au kufanya kitu kingine kitachotuwezesha kujikimu, badala ya kukaa na kujilaumu, ni kupoteza muda bure.

Kujaribu kukimbia ukweli huo ni kujidanganya bure. Kuna watu ambao hukimbia hali halisi kwa kunywa pombe, kuwa malaya, kugombana na kila mtu, na pengine hata kuamua kuachana na miili yao ( kufa). Bila shaka hawa ndio ambao ni dhaifu zaidi. Kujiuwa ni kutafuta suluhu ya kudumu kwa tatizo la muda mfupi.

Kumbuka jambo moja. Hata kama jambo litakuwa kubwa kiasi kwa gani, hatimaye ni lazima litafikia tamati. Kulikubali na kulikabili bila hofu ndio njia pekee ya kulifikisha kwenye tamati kimafanikio.

Kwa hiyo usiogope kuonekana kuwa una hofu, kwa sababu hofu ni suala la kimaumbile. Unachotakiwa ni kujichunga nacho ni kutafsiri vibaya matukio kwa kuongeza chumvi matukio na kujaribu kukimbia hali halisi.

Bado nasisitiza kuwa hofu zetu zisiwe ni dubwana la kutisha, kwa sababu ya kutafsiri kwetu vibaya matukio yanayotutokea katika maisha yetu, tukiweza kuratibu hisia zetu, basi tutaweza kukabiliana na hofu zetu kwa njia bora zaidi.


3 comments:
Andika Maoni Maoni
 1. Kaka,
  Awali ya yote, napenda kukupongeza sana kwa kuwa mwanablog. Blog yako, pamoja na uchanga wake ni nzito, imesheheni fikra makini juu ya maisha.
  Nilipoyasoma maoni yako kwenye blog ya dada Yasinta nilisukumwa kuzuru kijijini mwako. Kama nilivyohisi kabla sijafika, blog yako ni babkubwa. Kaza uzi kaka.
  Napenda kukukaribisha kijijini kwangu, usome mashairi, ili nawe ufikiri.
  Ni hayo tu!
  Kazi njema.

  ReplyDelete
 2. Ahsante kaka Mtanga kwa kunitembelea.
  Ukweli ni kwamba nilivutiwa sana na maoni yako uliyoyatoa kwenye blog ya Yasinta Ngonyani.
  Nilipoyasoma niliishiwa na maneno.
  Nakukaribisha tena na tena uje tujitambue.

  ReplyDelete
 3. Kaka,
  nitakuwa mgeni wako mara kwa mara kwa sababu napenda kupanua uelewa wangu.
  Nakushukuru sana nawe kwa kuwa mtembeleaji wa blog yangu.
  Nakutakia kila la kheri katika shughuli zako za kila siku, afya njema na furaha.
  Wanasema "success doesn't bring happiness, but happiness is a key to success."
  Kazi njema kaka.

  ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi