0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Nov 26, 2008

JE MWILI WA HISIA NI UPI?


Sema hisia zako, katika njia ambayo haitakuumiza au kuwaumiza wengine kihisia.


Mwili wa hisia:

Mwili wa hisia ni jumla ya hisia na mihemko yote. Hiyo ni kama, hasira, furaha, huzuni, sononeko, kero, kijicho, wivu n.k. Kila binadamu ana hisia kwani humsaidia kuishi. Mfano: bila hasira, utakufa baada ya muda mfupi kwani hutaweza kujilinda. Tunapaswa kutumia vizuri hisia zetu ili ziwe msaada kwetu na kwa wengine badala ya kuwa maumivu kwetu na kwa wengine.

Maumivu mengi ya kimaisha yanatokana na kushindwa kwetu kuzipeleka mahali bora hisia zetu ili zisitupe maumivu na badala yake ziwe na msaada kwetu. Kwa mfano: upande wa pili wa kijicho ni wa kujenga. Badala ya kuwa na hasira na kulaani na kumshusha aliyefanikiwa, mtu anaweza kujiambia kumbe inawezekana, na mimi nitajitahidi. Hapa ni kijicho kilekile ila kimegeuzwa kuwa wivu wa maendeleo (kutoa nafasi na muda kwenye kijicho katika mkabala wenye kujenga).

Watu ambao wanaweza kuitumia miili yao ya hisia vizuri, ni wale ambao wana utambuzi kuhusu mawazo yao, hisia zao na tabia zao. Wamejifunza namna ya kukabiliana na vema na matatizo ya kila siku ya kimaisha, ambayo hakuna anayeweza kuyazuia. Watu hawa hujihisi vizuri kuhusu wao wenyewe na hivyo wana uhusiano mzuri na watu wengine.

Kuna mambo mengi ambayo huwafanya watu kushindwa kuwa na afya njema kwenye miili yao ya hisia. Hebu fikiria kuhusu kupoteza kazi, kuanguka mtihani, kufiwa na mtu wa karibu, kuachwa na mpenzi, kuugua kwa muda mrefu au kuugua magonjwa hatari, kuwa na matatizo ya kifedha na mengine. Unaweza vipi kuyakabili haya, bila kuwa mwerevu kihisia? Ni vigumu.

Ukumbuke kwamba, mabadiliko mabaya au mazuri kwenye maisha yanaweza kuwa na athari mbaya kwenye miili yetu ya hisia. Mfano: kuhama, kupanda cheo, kuoa au kuolewa vinaweza kuvuruga miili yetu ya hisia. Tutaona ni kwa vipi kupanda cheo kunaweza kutuathiri vibaya wakati tutakapofika kwenye kipengele cha hasira na msongo. Hivyo bila kujali tuko katika hali gani, tunapaswa kujua namna ya kuratibu hisia zetu. Miili yetu hujibu mambo au kuwa katika hali fulani kutegemea na jinsi au namna tunavyofikiri, kuhisi na kutenda.

Uhusiano huu hufahamika kama uhusiano wa akili na mwili ( mind/body connection). Hivyo, unapoingia kwenye mashaka, wasiwasi na hofu, mwili wako hujaribu kukuambia kwamba, kuna jambo ambalo siyo sahihi (haliko sawa). Unapopata tukio au unapofikiria jambo ambalo litakuweka kwenye huzuni, kusongeka na kusononeka kwa muda mfupi au mrefu, unaweza kupata maradhi au matatizo ya kimwili kama vile: maumivu ya mgongo, kuumwa/ kubanwa kifua, kukosa choo, kuharisha, kinywa kukauka, kuchoka kupita kiasi, maumivu ya jumla ya mwili, kuumwa kichwa kisicho na maelezo rahisi, shinikizo la juu la damu, kukosa usingizi, kuhisi aina ya kizunguzungu kwa mbali, moyo kwenda mbio, matatizo ya tendo la ndoa, kukosa pumzi, shingo kukakamaa, kutoka jasho hovyo, usumbufu wa tumbo usioeleweka, kupungua uzito na vidonda vya tumbo.

Unaposhindwa kuuratibu vyema mwili wako wa hisia, huwa na afya duni na hivyo huuathiri mwili unaoonekana kwa kuuondolea kinga yake, ambapo maradhi hupata mahali pa kukimbilia. Maradhi yanapotupata, kama pia hatuwezi kuratibu mwili wetu wa akili, athari huja kwenye mwili huu unaoonekana na hivyo kuathiri mwili wa hisia tena, halafu huathiri mwili unaoonekana. Huu ni mzunguko thakili (vicious cycle). Mfano, mtu akifiwa na mkewe na akajaribu kushindana na hali hiyo (kuikataa) kwa kufikiri vibaya, na kuamua kutoa nafasi na muda kwa matatizo yaliyotokana au yatakayotokana na kifo cha mkewe kwa kujiuliza, kwa nini mkewe amekufa au amekufa kwa utata. Hali hii itasababisha hisia zake kukereka na hivyo zitaathiri kinga ya mwili. Mwili ukiathirika, ataanza kufikiri vibaya kuhusu mwili wake ( yaani ndiyo mimi kweli?). kwa kufanya hivyo, atachokoza hisia tena na hivyo kuumiza zaidi mwili huu unaoonekana. Ni mduara usio na mwanzo wala mwisho. Tunaposhindwa kufikiri vizuri, tunaishi kwenye mduara wa aina hiyo.

Jinsi ya kuwa na afya bora ya mwili wa hisia:

( i ) Kila wakati, tambua au fahamu upo kwenye hisia gani kwa kujenga urazini ( kujua kila wakati uko kwenye hisia gani na kwa nini?).
mfano, ukiwa na huzuni, jiulize ni kwa nini uwe na huzuni. Ukiwa na simanzi hivyohivyo. Usikubali kubeba hisia usizozipenda bila kufahamu ni kwa nini umezibeba.

( ii ) Sema hisia zako wazi na kwa njia nzuri. Usifiche hisia zinazoumiza kwani zitasababisha maumivu zaidi. Ni vyema mtu unayemwambia akawa mtu wa nje ya familia, inaonekana watu wa familia wameshindwa kumudu kuwasaidia jamaa zao kutoka kwenye maumivu ya kihisia. Kama unajisikia kulia, lia sana, kama ni kucheka, cheka sana. Usijaribu kukandamiza hisia kwani utaumia. Wanaume waliambiwa kulia ni tabia ya kike. Huu ni ujinga mwingine wa ukweli wa kimapokeo, ukatae.

( iii ) Ishi maisha yenye uwiano bora. Usiwaze sana kuhusu matatizo ya kazini, nyumbani au popote ambayo yatakufanya usifikiri vizuri. Hii haina maana ujifanye kwamba umefurahi, wakati umejaa mashaka na hofu tele. Fahamu kwamba, kufikiri vizuri ndiko kunakoweza kukusaidia kukabiliana na matatizo na siyo kufikiri vibaya. Weka nguvu kwenye mambo au vitu ambavyo vitakupa nguvu na ahueni. Kumbuka, hisia kama hisia hazina tatizo, kama ambavyo hakuna kitu au jambo lenye tatizo, bali wewe. Kama ukishindwa kuzipeleka hisia zako namna na mahali panapostahili, zitakuumiza.

Werevu wa kihisia (emotional intelligence):

Ukweli ni kwamba, kila siku huwa tunakabiliwa na hisia nzuri au mbaya.
Je, tuwazuri kiasi gani katika kuzisimamia? Huwa unakabiliana vipi na hasira? Hofu? Kuvunjika moyo? N.k. Je, ni nani alikufundisha kuchukulia hisia kama ufanyavyo? Je, unaweza vipi kupokea, kuonesha, kuelewa na kuratibu hisia zako na za wengine kwa njia isiyoumiza.

Werevu wa kihisia ni ule uwezo wa kudhibiti hisia zako na za wengine ili zisikuumize wewe au wengine. Kila binadamu anaweza kuratibu hisia zake akitaka. Hisia hizi ni kama kucheka, kukasirika, kuhisi kijicho, hofu, kuvunjika nguvu, wivu, huzuni, furaha n.k. karibu hisia zote ni miito ya kibaologia. Hakuna binadamu anayeweza kupinga kutokewa nazo. Lakini pale zinapozidi au zinaposhindwa kupatikana kwa mazingira muafaka huweza kusababisha matatizo.

Kwa sehemu kubwa tumejifunza kuhusu hisia kutoka kwa watu wa karibu yetu tangu tukiwa wadogo kwa kuona na kusikia. Hatufundishwi shuleni namna ya kuratibu hisia zetu, bali wazazi na walezi wetu walitufundisha. Lakini tukiwa wakubwa (ukubwani) ni muhimu sana kujifunza namna ya kuratibu hisia zetu ili zisituumize au kuwaumiza wengine. Watu ambao wanamudu kuratibu hisia zao na kuwawezesha kutowaumiza huwa na uhusiano mzuri na watu. Tunasema, watu hawa ‘wana werevu wa kihisia’

Vyanzo vya migogoro ya hisia:

i. kuchukulia mambo kibinafsi (personal).

ii. kutosikiliza.

iii. kutojua lugha nzuri katika kujieleza.

iv. kutozingatia hali ya hisia ya mzungumzaji.

v. hisia za watu wengine ni zao, usichukulie kuwa ni wewe umewakera.

vi. usijali matokeo, jieleze au wasikilize watu wengine kwa kadri ya uwezo wako wa utulivu, waache waamue.

Sifa zinazobainisha werevu wa kihisia:

(i) Mtu mwenye werevu wa kihisia anajua hisia zake na kuweza kutambua ni nini anafikiri katika muda mwingi. Kumbuka, baada ya kufikiri hufuata hisia. Ukijua unachokifikiri, utajua kirahisi ni kwa nini unahisi kwa namna unavyohisi.

(ii) Mtu mwenye werevu wa kihisia ana uwezo wa kuzidhibiti hisia zake na kujua namna ya kuzifanyia kazi. Kama ni hasira anajua kuzidhibiti na kujua zitamfaidisha vipi badala ya kumpa hasara. Kama amekasirika kwa sababu amedharauliwa, badala ya kutukana na kutaka vita, ataamua kurekebisha au kuboresha eneo lililomfanya achekwe, bila kinyongo kwa aliye mcheka.

(iii) Mwenye werevu wa hisia ni mtu ambaye hakati tama hata pale panapoonekana kwamba kuna vikwazo vikubwa. Kumbuka jambo moja, kukata tama hutokea akilini, ambapo huzifanya hisia za mtu kuingia kwenye kukasirika, kukosa matumaini au chochote.

(iv) Mtu mwenye werevu wa kihisia ana uwezo wa kusoma mawazo ya wengine na kuyaelewa. Kusoma mawazo yaw engine maana yake ni kumudu kujua wengine watajihisi au wanajihisi vipi kwenye mazingira fulani. Kuna watu ambao hawajui nikisema au kufanya nini kwa mtu au watu gani watajihisi vipi. Huongozwa na hisia tu. Wakifurahi au kukasirika wanaweza kusema au kufanya kwa njia yenye kuwaumiza sana wengine. Huu ni udhaifu.

(v) Mwenye werevu wa kihisia ana uwezo wa kujenga na kudumisha uhusiano bora kazini, na marafiki, wapenzi, na watu walio katika familia yake. Hii inatokana na ukweli kwamba, kwa kumudu kuziratibu hisia zake vizuri, hawakeri watu kirahisi.


Njia zitakazokuwezesha kuratibu hisia zako:

(i) Unatakiwa kujua kwamba unazo hisia na huwa zinajitokeza kwako. Mfano_ jua kwamba, sasa umekasirika, sasa umefurahi au sasa umehuzunika. Watu wengi huwa hawajui kwamba wako kwenye hisia fulani, hivyo wanapokuwa kwenye hisia hizo, wanafanya mambo kimazoea (wanarudia makosa).

(ii) Ukishagundua kwamba upo kwenye hisia fulani unatakiwa ‘utulie’ usifanye kitu chochote. Hii inakupa nafasi nzuri zaidi ya kudhibiti hisia zako, siyo hisia zikudhibiti wewe.

(iii) Kubali kwamba upo kwenye hisia fulani. Kuna wakati mtu anakasirika lakini anapingana na ukweli huo. Kuna wakati mtu anahisi kijicho dhidi ya mafanikio ya mtu mwingine, lakini anajitahidi kupingana nayo kwa kujiambia “simwonei kijicho” bali anaringa ndiyo maana namchukia. Jaribu kukiri, kukubali kwamba uko kwenye hisia fulani kwani hisia siyo dhambi.

(iv) Unapokuwa kwenye hisia fulani usijaribu kufikiri au kufanya jambo lolote kwani hutamudu. Hisia zinapokuwa juu mantiki haifanyi kazi. Matumizi ya akili na hisia za juu au kuhemkwa haviwiani. Kama umekasirika sana usifanye jambo kwani utakachokifanya kitakuwa ni upuuzi. Ndani ya hisia kali hakuna matumizi ya akili, subiri hisia au furaha yako iwe katika hali ya kawaida ndiyo ufikiri na kutenda.
Kumbuka kwamba si vyema kujaribu kuwasiliana na mtu mwingine kwa kufuata hisia zake. Usivutwe na ndoano ya mtu mwingine. mfano: uko na rafiki yako ghafla akakasirika, wewe usikubali kukasirika, ukikubali ina maana umekubali kunaswa kwenye ndoano au mtego wake.

Hivyo mtu anapokasirika, unachotakiwa kufanya ni wewe kutulia, badala ya kuambukizwa na hasira zake. Unachotakiwa kufanya, ni kumwambia kwamba, ‘naona umekasirika, basi tutajadili au tutaongea baadaye’. Ukivutwa na hasira zake na ukajikuta na wewe
umekasirika hujitendei haki na hivyo umeshindwa kuwa na werevu wa hisia. Lakini pia, kubali hisia za mwingine. Aliyehemkwa hajui asemacho wala atendacho.

(v) Usimeze hisia zako, badala yake ziseme. Kama umekasirika mwambie mtu kwa upole, lakini kwa dhati kuwa umekasirika.
Ukimeza hisia, zitakuja kulipuliwa na jambo dogo sana. Lakini pia, ukimeza hisia zako watu hawatajua kwamba jambo fulani hulitaki, hivyo watakukera bila kujua. Waambie watu kama wanakukera jambo fulani au kama wanapaswa kukufanyia au kutokukufanyia jambo fulani. Weka mipaka ili usiingiliwe hovyo. Hupaswi kuogopa kusema hisia zako, bali ziseme kwa njia ambayo haitakuumiza au kuwaumiza wengine. Ukitulia, yaani ukiwa haupo kwenye mhemko, ndipo unapopaswa kusema hisia zako.

(vi) kwa kadri jinsi unavyokuwa na werevu wa kihisia zaidi, ndivyo unavyoweza kuwa na uhusiano mzuri na watu wengine na kuweka mipaka. Kwa kwawaida, sisi wote tuna mipaka ya kimwili (hii inayoonekana). Mipaka ya kihisia, ya kiakili na ya kiroho. Hii huwa hatuioni (haionekani). Hivyo, tunapaswa kuheshimu mipaka yetu.


Kwa Makala hii naamini sasa wasomaji wataelewa ni kwa jinsi gani maarifa haya ya utambuzi yamelenga kuwasaidia watu kwa kiasi gani, kwani kimsingi ukifahamu miili hii mitatu jinsi inavyofanya kazi na ukaweza kuidhibiti na kuiendesha na sio ikuendeshe wewe, basi maisha kwako yatakuwa ni rahisi sana.
Bado nitakuwa najadili mada tofauti tofauti kulingana na jinsi nitakavyoona, na kama kutakuwa na hoja mbalimbali kutoka kwa wasomaji wa blog hii, nitaziweka hapa barazani ili tusaidiane kujadili na kupata mawazo tofauti tofauti kutoka kwa wasomaji wengine.

Naomba kuwasilisha.

4 comments:
Andika Maoni Maoni
 1. Nakubali kabisa Mkuu!Lakini ngumu kweli kuwa makini na hisia kila wakati!Ingawa si busara kuusingizia udhaifu wa kibinadamu kwa kushindwa kuwa dereva mzuri wa hisia.

  ReplyDelete
 2. Nakubaliana na wewe kaka Kitururu,
  Lakini kama unakumbuka katika makala zangu niliweka bayana kwamba mtu kuweza kudhibiti hisia zako inahitaji mazoezi ya kutosha kwa sababu tangu kuzaliwa kwetu tumelishwa hisia hasi nyingi sana, kwa hiyo hilo sio jambo la kuliondoa mara moja kama vile kuweka chumvi kwenye mboga au kuweka sukari kwenye kinywaji na kuonja halafu ukapata majibu wakati ule ule. Itategemea na namna utakavyoweza kucheza na hisia zako.
  Kimsingi hili litawezekana iwapo utaifahamu miili hii mitatu niliyoizungumzia, ambayo ni mwili huu tulionao, mwili wa akili na mwili wa hisia. ukimudu kuifahamu vizuri kabisa na kuitofautisha, basi utakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuweza kucheza na hisia zako kwa jinsi unavyotaka.
  nakukaribisha uendelee kupita katika baraza hili la utambuzi ili uweze kujitambua. Pia nakaribisha maoni zaidi kutoka kwako na kwa wengine.

  Shabani Kaluse

  ReplyDelete
 3. @Kaluse:Ni Kweli Ambiere!Lakini nachojaribu kusema ni kwamba katikati ya maisha bize tuishiyo, unaweza kujikuta uko bize na mambo hata ya kijinga na kukosa muda hata wa kuwa peke yako kujaribu kujifunza kujijua au kujua hisia zako.

  ReplyDelete
 4. Ambiere Kitururu, hivi ni nani aliyekuambia kwamba kuna kitu kinaitwa bize?
  Kwanza bize ni nini?
  Nadhani ninahitaji muda zaidi ili niweze kukuweka sawa.
  Kwa kifupi hakuna kitu kinaitwa bize ila sisi wenyewe ndio tumekuwa wabunifu wa vitu vinavyotuumiza wenyewe.
  Hivi nikikwambia kuwa hakuna kitu kinachoitwa muda utakubaliana na mimi?
  Hivi unafahamu kwamba muda uligunduliwa wakati binadamu, akiwa ameshakuwa mjanja?
  Hebu tujiulize mimi na wewe kabla hivi vitu tunavyoita, sekunde, dakika, saa, siku, wiki, mwezi, mwaka, nakadhalika nakadhalika, havijagunduliwa, watu walikuwa wanaratibu vipi shughuli zao?

  Naomba unipe muda, nakuandalia jibu katika makala inayofuata..........

  NI MI AMBIERE KALUSE

  ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi