0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

http://www.serenahotels.com/serenadaressalaam/default-en.html

Jan 27, 2013

KWANGU MIMI ILIKUWA NI KAMA NDOTO....!

Hadi leo naona kama ndoto.............!
(Picha haihusiani na habari hii.)

Nakumbuka ilikuwa ni mwaka 1991 wakati huo nikiwa nafanya kazi kwa mtu binafsi, Muasia mmoja. Nakumbuka katika mojawapo ya majukumu yangu, nililazimika kwenda Nairobi nchini Kenya. Nilikwenda huko kikazi na nililazimika kukaa kwa mwezi mmoja. Nilipomaliza kazi ile, niliamua kukaa kama siku tatu zaidi ili kujionea hali ya Kenya ilivyo. Nilizunguka jijini Nairobi na kwenda maeneo ya karibu kama vile Thika, Kinangop na miji mingine iliyo karibu na jiji hilo maarufu katika ukanda huu wa Afrika Mashariki.


Siku moja wakati natoka kwenye matembezi yangu nje ya jiji hilo la Nairobi, nilikutana na mtu mmoja. Huyu bwana alikuwa anaonekana kuchoka sana, ama kwa kuumwa au kwa njaa. Nilikaa naye kiti kimoja kwenye Matatu, yaani daladala za Kenya. Huyu bwana alikuwa ananitazama mara kwa mara na kujitahidi kutaka kama kutabasamu, ingawa hakumudu sana.

Niliingiwa na huruma na kulazimika kumuuliza kama alikuwa yu mzima wa afya. Alisema anaumwa na hana hata senti tano ya kulipia matibabu yake. Nilimuuliza kama anao ndugu. Alisema hana na familia yake iko mashambani, ambapo haina kitu kabisa. “Nina watoto watatu mmoja amemaliza shule hana kazi na wawili wanasoma, lakini ni kwa mashaka sana, kwani mara nyingi hurudishwa nyumbani kutokana na kukosekana ada.” Aliniambia.

Ilibidi nimchukue yule bwana hadi hospitalini ambapo alichukuliwa vipimo. Aliambiwa arudi kesho yake kuchukua majibu yake. Tuliagana tukutane pale hospitalini kesho yake. Kwa kweli hakuamini kwamba, nilimfikisha hospitalini na kumlipia matibabu. Hakuweza hata kushukuru na nilielewa ni kwa sababu gani. Mshangao ulikuwa ni mkubwa sana kwa upande wake.

Kesho yake alipata majibu yake ambayo yalionyesha kwamba alikuwa na maji kwenye pafu moja pamoja na kifua kikuu. Ilibidi aandikiwe dawa. Hakuwa na fedha kabisa. Ilibidi nitoe fedha zote za matibabu yake. Ilikuwa kama silimia 20 ya pesa zote nilizozipata pale Nairobi kama posho. Lakini hiyo haikunisumbua. Nilikuwa najisikia vizuri kuona angeweza kupona.

Ilibidi niombe ruhusa ya siku saba zaidi ili nikae Nairobi kukagua hali ya yule jamaa. Wakati huo huo nilimwambia kwamba, kama anaweza kumwita mkewe akae naye pale mjini wakati anatibiwa ingekuwa vizuri. Nilimwambia ningemsaidia pesa kidogo za kumwezesha mkewe kukaa naye angalau kwa siku kadhaa. Alikubali na kumwita mkewe. Mkewe alipofika hakuamini kwamba niliweza kumsaidia mumewe vile. Yule mama alilia sana na aliniombea sana kwa kikwao, yaani Kikikuyu kwa majina ya mizimu yote. Nilijisikia furaha kwa namna mke wa jamaa alivyojisikia vizuri kuona mumewe amepata matibabu.

Niliondoka Nairobi siku ya tatu tangu mkewe kuja. Niliwaachia hela kiasi cha shilingi 14,000 za Kenya, ambazo nilimwambia yule mama zingemsaidia kufanyia shughuli yoyote ambayo ageona inafaa. Niliondoka bila hata kuwaachia anuani yangu wala simu yangu. Labda wao walitegemea ningewapa anuani yangu, lakini sikufanya hivyo. Mimi sikuona sababu ya kuwapa kwani, niliwasaidia kama binadamu ambao wanahitaji msaada wangu, siyo ili wanijue au tuwe marafiki. 

Hivyo ndivyo nilivyo hata leo. Sijisifu kwa sababu sioni kuwa ni sifa, bali naona kila binadamu angetakiwa kuwa hivyo, ila basi tunazuiwa na choyo ya kufundishwa. Sikuwahi kusoma kuhusu masuala ya kusaidia na kupata furaha wala kumsikia mtu. Tabia hii nilitoka nayo kwetu, niliitoa kwa baba yangu ambaye, alikuwa mtu wa kusaidia sana bila kujali malipo. Hilo nalijua.

Mambo yangu yalienda vizuri hadi mwaka 1994. Mwaka huo nilipoteza kibarua change na hata shughuli zangu zikawa zimepoteza umaarufu kutokana na mabadiliko ya teknolojia. Ilibidi nianze kuhangaika. Kufikia mwaka 1996, nilikuwa hoi bin taabani kiuchumi. Watoto wangu watatu wakawa hawaendi tena shule, hakuna ada. Tulishindwa kulipa kodi ya nyumba, ambapo ilibidi tufukuzwe na kwenda kuishi kwa ndugu wa mke wangu. Huyu naye hatukukaa hata mwezi masimango yakaanza. Siwezi kumlaumu, kwani kusaidia siyo jambo rahisi, ingawa naamini ndipo mahali furaha ya binadamu ilipo.

Tulilazimika kuhama na kwenda kuishi Mtoni Kijichi. Huko hatukuwa tumepanga. Jamaa yangu mmoja alikuwa anajenga kule na alikuwa anataka mlinzi, ambapo nilimwambia ningefanya kazi hiyo. Hivyo tukawa tunaishi kwenye kibanda cha mtumishi. Lakini tulihisi nafuu. Hata hivyo watoto wote walisimama shule, kwani hata nauli ya kuwapa ili waende shule ilikuwa ni vigumu. 

Mwaka huo huo wa 1996 mwezi Novemba likazuka tatizo lingine. Mke wangu alianza kuumwa. Ilikuwa kama ghafla tu, alianza kulalamika tumbo na akaanza kuwa anatoka majimaji sehemu za siri. Nilijitahidi kumtafutia dawa za miti shamba kwa wenyeji bila mafanikiao. Jirani yangu mmoja aliona hali inazidi kuwa ngumu na alijua tatizo langu ni ukata. Huyu alijitolea kunipa 3,000 nilimpeleka mke wangu hospitalini. Nilimpeleka pale Temeke ambapo nao walisema labda nimpeleke Ocean Road, kwani wana wasiwasi kwamba, huenda alikuwa na kansa.

Nilimpeleka Ocean Road na matokeo yakawa ya kuumiza kuliko maradhi yenyewe. Ni kweli alikuwa na kansa, tena ilikuwa imefikia hatua ya nne. Kwenye hatua kama hii, kupona ni miujiza. Ilibidi aanze huduma ya matibabu palepale. Alipomaliza huduma ya matibabu hakuchukua miezi mitatu akafariki. Lazima niseme kweli kwamba, nilipoteza sehemu yangu kwa kumpoteza mke wangu.

Tunaambiwa kila mtu ni kamili kama alivyo, lakini kuna wakati tunaweza kumpoteza mtu, tukahisi kama nasi wenyewe tumepotea nusu. Msiba huu ulikuwa mkubwa kwa namna mbalimbali, kwani hata mazishi yenyewe yalikuwa na kero zake. Kutokana na ugeni pale Kijichi, ilionekana hakuna aliyekuwa akitujua na ilionekana kwa maana hiyo kwamba, hatuhudhurii mazishi. Kwa hiyo waliohudhuria mazishi ya mke wangu walikuwa ni watu wachache sana.

Lakini tulizika na mambo yakaisha. Nilibaki na wanangu watatu ambao nao hawakuwa na mwelekeo. Mmoja alikuwa amekomea darasa la sita, mwingine la nne na wa mwisho wa kike darasa la pili. Huyu ndiye aliniumiza sana, kwani alikuwa karibu sana na mama yake. Mambo hayakubadilika na katika kujihami na shinikizola ukata nililazimika kuanza kunywa pombe. Nilitaka kupoteza mawazo, kwani sikuwa namudu tena kuishi nikiwa mzima wa akili. Nadhani ndilo kosa ambalo wengi huwa tunalifanya tunapokabiliwa na matatizo.

Mwaka 1998 nilikuwa na watoto wawili pale nyumbani. Yule mkubwa wa kiume alihama nyumbani na nikasikia kwamba anafanya kibarua cha kupiga debe. Sikujali kuhusu taarifa hiyo. Yule wa pili alikuwa tu nyumbani akiishi kwa kufanya vibarua vya kubeba mchanga au vya aina nyingine. Yule mdogo wa kike, alikuwa anasoma kwa msaada wa jirani ambaye alitokea tu kumpenda, kwani alikuwa ameelewana sana na marehemu mke wangu, wakati tuliphamia pale. Hiyo pia haikunisumbua na wala sikwenda hata kumshukuru. 


Septemba mwaka 1998, nikiwa ninatoka kwenye ‘kubangaiza’ mjini nilipita eneo la karibu na Hoteli ya Peacock. Wakati napita jamaa mmoja alinismamisha na kunisalimia. Huyu jamaa tulikuwa naye zamani kwenye ile kampuni ya Waasia. Tulisalimiana na alinipa pole ya msiba wa mke wangu. Halafu tulianza kujadili kuhusu maisha kwa ujumla.


Wakati tukiwa tunaongea, alitokea jamaa mmoja na kusimama akitutazama. Huyu jamaa alikuwa mnene, mrefu na mwenye rangi ya maji ya kunde. Sikuwa namjua na nilihisi alikuwa anajuana na mwenzangu, hivyo alikuwa anasubiri tumalize kuzungumza ili wazungumze. Hivyo ilibidi nimuage yule jamaa ili niwape nafasi.

Wakati najiandaa kuondoka, yule mtu aliniita kwa jina langu. “Nadhani ni wewe bila shaka, kama siyo wewe utanisamehe.” Alisema. 

Nikiwa nimeshikwa na butwaa nilimjibu. “Ni mimi, samahani, nimekusahau kidogo, labda unikumbushe.” Halafu lilikuja jambo ambalo hata kama ingekuwa ni wewe usingelitarajia. “Tulikutana Nairobi, ulinisaidia, uliokoa maisha yangu…….” Kuna wakati mtu unapata mshangao ambao unakuwa kama vile ni maumivu yasiyovumilika. Ndivyo ilivyokuwa kwangu. Nilitulia kwa muda mrefu sana, kabla sijasema, “nakukumbuka, nakukumbuka sasa vizuri.”

Unaweza ukadhani najua kujifaragua, lakini hapana. Ninapomsaidia mtu huwa nimemsaidia na tumemalizana, sihitaji kumjua tena kama siyo lazima. Kwa hiyo hata huyu bwana sikuweza kumkumbuka kirahisi. Mabadiliko ya mwili aliyokuwa nayo, pia yasingeniwezesha kumkumbuka hata kama ingekuwaje. Aliniambia kuwa anakuja hapa nchini kibiashara na amekuwa akitamani kuniona. “Nikija Dar huwa natembea sana kujaribu kukutafuta. Niliuliza ile kampuni uliyosema unafanya nikaambiwa uliondoka.” Aliniambia na kuniomba twende chumbani kwake pale Hotelini.

Alikuwa amefurahi zaidi kuniona mimi bila shaka, na alianza kunisimulia kuhusu namna mkewe alivyoweza kufanya biashara kwa zile fedha nilizompa na yeye kuungana naye baada ya kupona. “Tuliweza kufanya kitu kikubwa sana. Fedha zako zilikuwa na baraka na kuna wakati tulikuwa tunaambiana na mke wangu kwamba, hatuwezi kukuona kwani tuliamini wewe ni malaika kiongozi (Guardian Angel).” Alisema. Ulipokuja upande wangu kusimilia maswahibu yangu, yule bwana furaha yote ilimwishia na alilia kwa muda mefu sana. Baadaye aliingia bafuni na alimpigia mkewe simu kumweleza hali yangu. 

Alikuwa anazungumza kwa Kikikuyu, lakini kwa sababu ni kibantu niliweza kuokota maneno mawili-matatu. Halafu aliniomba kama ningeweza kufuatana naye kwenda Nairobi kesho yake. Nilimkubali. Tulikula chakula cha mchana pamoja huku akinisifu kwa namna nilivyo na ukarimu. Tumbo langu bila shaka lilipata mshangao, kwani kwa miaka mingi nilikuwa sijala chakula cha utulivu.

Niliagana naye huku akiniachia shilingi 50,000. Ilikuwa kama vile nimepata shilingi milioni tano. Jioni ile nilikwenda kwa yule jirani yetu anayemsomesha mwanangu, ambapo nilimpa shilingi 20,000 na kumwomba radhi kwa kutoona anachofanya. Halafu nilimwita mwanangu mwingine na kumwambia asikate tamaa, kwani mambo yatakuja kubadilika. Huyu nilimpa shilingi 10,000 na kumwomba aache kwa muda kufanya vibarua.


Kwa mara ya kwanza tangu kufiwa nilitembelea kaburi la mke wangu. Nililia sana hapo kaburini kwa kushindwa wajibu wangu kama baba. Nilirejea nyumbani na kulala baada ya kuandaa nguo ambazo ningesafiri nazo.


Naona nisiwachoshe kwa kuwasimulia kila kitu. Ni kwamba, nilifika Nairobi na kushangaa kukuta yule jamaa yangu akiwa na biashara kubwa ya jumla ya vifaa mbalimbali.

Alikuwa akinunua vifaa mbalimbali ambavyo kwa Kenya ni adimu, na ambavyo vinapatikana Tanzania. Ilikuwa ni biashara kubwa. Nilipokewa vizuri kiasi kwamba, niliona kama sistahili. Nilitambulishwa kwa kila ndugu na jamaa wa familia ile kwamba, mimi ndiye niliyewapa mtaji wa biashara. Hawakuficha wala kuona aibu. Walikuwa ni watu wanaojiamini. Hao jamaa na ndugu zao walinitazama kwa woga mkubwa wakijua kwamba, mimi ni tajiri wa ajabu. 


Nilikaa Nairobi kwa wiki moja. Unajua walifanya nini watu wale? Walinipa shilingi 300,000 za Kenya ambazo zilikuwa kama shilingi milioni 3.5 za hapa kwetu kwaq wakati ule. Waliniambia hawana njia nyingine ya kuonyesha shukurani yao kwangu kwani hicho walichonipa ni kidogo sana. Kwangu ilikuwa kama ndoto.

Nilirudi Dar nikiwa mtu tofauti kabisa. Yule bwana na mkewe walinipa uwakala wa kuwapelekea bidhaa kule Nairobi, badala ya yule jamaa kuja kila wakati. Shughuli hiyo nilimpa mwanangu mkubwa ambaye nilimsaka na kumpata baada ya kurejea.

Hakuwa anataka kusoma hivyo niliona nimpe yeye biashara ile. Nashukuru hakuwa ameingia ulevini wala kwenye kuvuta bangi na alikuwa amefungua akaunti benki ya posta, jambo ambalo lilinionyesha kwamba, alikuwa na ufahamu mkubwa.

Hadi leo anafanya biashara za Nairobi-Kampala-Dar es Salaam. Ile familia imekuwa ni ndugu zetu. Watoto wangu wale wawili waliendelelea na elimu hadi elimu ya juu na sasa wamemudu kusimama wenyewe. Miaka miwili baadae tangu niliporudi kutoka Nairobi nilioa na sasa nimepanuka kibiashara, nikiwa nimejikita katika maeneo ya Manzese, Magomeni na Kinondoni B. 

Usione mtu ana biashara fulani au mafanikio fulani ukadhani yalikuja tu, kuna habari pana nyuma yake wakati mwingine. 

Kuna jambo naomba sana nikusaidie kulifahamu. Hili ni jambo ambalo linaonekana halina maana, lakini ndio ubinadamu wenyewe. Jitahidi sana popote ulipo kuwasaidia watu, bila kujali kama watakukumbuka au kukulipa ama hapana.

5 comments:
Andika Maoni Maoni
  1. habari hii imenigusa sana kweli. Wengi tunasahau ubinadamu yaani kusaidiana jhata kama una kidogo kwa mwingine kitakuwa kingi na kitamsaidia.Tusijali kulipwa..

    ReplyDelete
  2. Habari ya huzuni, mshangao, utu na maajabu yake Mungu muumba. This is what I call "divine human connections". Hadithi imenigusa hasa na jambo la kusaidiana bila ubagusi wo wote. Asante, hadithi yenye mafundisho makuu ya binadamu na kusaidiana.

    John Fisher Kanene,
    Nairobi

    ReplyDelete
  3. Kwa kweli,kisa hiki kimenigusa sana.Tujifunze kusaidia,na malipo yake ni mungu pekee anajua.

    ReplyDelete
  4. Hakuna mtu chini ya jua ajuaye ni lini atapata tatizo lililo juu ya uwezo wake, hivyo basi kujitoa kwa ajili ya kusaidia tena bila ya kujitangaza ni mbegu ambayo tunda lake siku zote huonekana siku utakayokuwa na shida iliyo nzito kuliko uwezo wako hata kama utasaidiwa na mtu tofauti na yule uliyewahi kumpa msaada.

    ReplyDelete
  5. Nimesoma kisa hiki nimejikuta machozi yananitoka tu kwa mshangao, huzuni na furaha! kweli binadamu hujafa hujaumbika, tunapitia mengi sana ambayo mwishowe ndio yanatufanya tusimame imara.Kutoa ni moyo, si utajiri.

    ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi