0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Dec 7, 2009

MITIHANI YA MAISHA INAPOKITHIRI


Alikuwa akisafiri kwenye barabara kuu akiwa juu ya pikipiki yake. Alikuwa akiendesha kwa wastani wa kilimeta 65 kwa saa. Jambo lenyewe lilitokea ghafla sana. Aligeuka kutazama pembeni mwa barabara na aliporudisha macho barabarani, gari kubwa la mizigo lililokuwa mbele yake lilikuwa limesimama ghafla.

Ilikuwa ni ghafla mno kiasi kwamba hata akili kufikiri ilikuwa ngumu sana. Kwa kutaka tu kuokoa maisha yake mawazo ya nguvu za mwisho yalimjia ambapo aliangusha pikipiki na kuburuzika chini ya gari hilo. Wakati akiburuzika, kifuniko cha tangi la mafuta la pikipiki yake kilifunuka na jambo baya lilitokea.

Moto ulilipuka akiwa bado anaburuzika chini ya gari hilo. Anachokumbuka baada ya hapo ni kupata fahamu wakati akiwa hospitalini. Alikuwa ameungua karibu mwili wote kwa kiwango ambacho hata kupona ilionekana ni suala la Mungu mwenyewe. Lakini yeye hakukata tamaa katu. Alisema kwamba anataka kupona na kwamba ni lazima angepona.

Alipona na kuanza shughuli zake za biashara kama vile hakuwa amepatikana na ajali ile mbaya. Lakini haikuchukua muda kabla hajapambana na kisirani kingine cha maisha. Ilikuwa ni wakati wa safari zake za kibiashara, ambapo ndege aliyokuwa akisafiri nayo ilianguka naye akaponea chupuchupu. Lakini akalemaa kuanzia kiuno kwenda chini.

Hakukata tamaa. Alisema anataka kuishi na siyo kuishi tu bali kuishi kwa mafanikio. Alipopona alirudi katika biashara zake kama vile hakukuwa kumetokea jambo lolote baya au la kuvunja nguvu.

Huyu siye mwingine bali ni mfanyabiashara maarufu sana kule Colorado nchini Marekani, William Mitchel, ambaye baada ya mitihani hii mikubwa ya kimaisha alipata ari mpya ya kutafuta mafanikio maishani. Aliendelea kufanya biashara huku akiwa na makovu na ulemavu hadi akafanikiwa kuingia kwenye orodha ya mamilionea wa Marekani.

Bila shaka unafahamu kwamba kwenye maisha huwa tunapitia hatua mbalimbali za mabadiliko kutoka mafanikio kwenda maanguko au kinyume chake na kutoka faraja kwenda visirani au kinyume chake. Kila mmoja wetu ana njia ambayo huchukulia mabadiliko haya.

Kuna wakati ambapo huwa tunasema tunajaribiwa, tunapewa mitihani na mungu. Hali hii iko duniani kote na kwa kila binadamu kutegemea tu mazingira ya mitihani hiyo. Wakati huu ni ule ambapo kila tulicho nacho kama ulinzi wetu hujaribiwa. Huu ni wakati ambapo huwa tunayatazama maisha kama yasiyo na haki na yanayoonea au kutazama upande mmoja.

Hiki ni kipindi ambapo imani zetu, thamani ya utu wetu, viwango vya subira zetu na uwezo wa kujizatiti hufikishwa kwenye ukomo, ambao tunadhani hatuwezi tena kuwa na vitu hivyo.

Kwa baadhi ya watu, hutumia vipindi kama hivi vya mitihani ya maisha kuwa watu bora zaidi, wakati wengine hutumia vipindi hivi kukata tamaa na kuharibu kabisa maisha yao. Je umeshawahi kujiuliza maishani mwako ni kwa nini baadhi ya watu hutumia mitihani ya maisha kufanikiwa na wengine huitumia kwa kuanguka kabisa maishani?

Ukweli ni kwamba siyo kuwa watu walifanikiwa hawana au hawakupitia mitihani katika maisha, tena huenda wamepitia mitihani mizito kuliko wale ambao hawana mafanikio maishani mwao. Mahali ambapo hakuna matatizo ni kaburini tu, lakini kwenye maisha matatizo ni lazima kwa yeyote.

Watu wanaofanikiwa kupitia mitihani ya maisha na wale wanaoanguka kabisa kufuatia mitihani hiyo hutofautiana katika jambo moja tu, jinsi wanavyoichukulia mitihani hiyo na wanachokifanya baada ya kukumbwa nayo. Kinachowatofautisha siyo kile kilichotokea, yaani mitihani bali wanavyotazama na kuchukulia kile kilichotokea na matendo yao baada ya mitihani hiyo kutokea.

Kama Mitchel alivyoungua mwili mzima, ilikuwa ni juu yake kuamua kuhusu tukio hilo. Kama angeamua kwamba kuungua kule ulikuwa mwisho wa maisha , mwisho wa kutafuta mafanikio, bila shaka angefia hospitalini au hata kama angepona, angebaki mtaani kuombaomba. Lakini kwake kuungua kule kulikuwa ni changamoto katika kutafuta maana halisi ya maisha. Alijiambia kwamba, mtihani ule wa kuungua haukuwa umempata tu kwa sababu ya kumpata, bali kulikuwa na maana kubwa, kusudi maalum kubwa. Kusudi ambalo linalenga kwenye kubadili maisha yake kwa mafanikio makubwa zaidi.

Ni wangapi kati yetu ambao wanapopambana na mitihani ya maisha huchukulia mitihani hiyo kama mwisho wa maisha yao. Huanza kuchanganyikiwa na hata kuamua kujiuwa? Ni wangapi ambao wanapopambana na mitihani ya maisha huanza kuwanyooshea kidole wengine kwamba ndio wamewasababishia matatizo hayo kwa kuwaloga au kwa njia nyingine? Ni wangapi ambao wanapopambana na mitihani ya maisha huamua kuingia katika ulevi ili kupoteza mawazo? Bila shaka ni wengi, wengi, wengi sana, pengine ukiwemo na wewe.

Hebu jiulize kama leo hii utapoteza kazi yako, utapoteza biashara yako, kuunguliwa na nyumba na kufiwa na mpendwa wako katika kipindi kisichozidi miezi mitatu, utafanyaje? Wengi wetu kwa kujifurahisha tunaweza kusema tutamshukuru mungu, lakini ukweli ni kwamba hatutakumbuka kama kuna Mungu na kama tutakumbuka, tutaishi kumtukana.

Lakini hii yote itatokana na ukweli kwamba tutakuwa tumeiweka akilini mitihani hii ya maisha vibaya. Kama ambavyo tumesema , ni kwamba mitihani yenyewe kama mitihani haina maana bali maamuzi yetu ndiyo yanayoipa maana. Badala ya kusema kwamba sasa hatuwezi kuinuka tena baada ya kufilisika kwetu kama tukio muhimu la kutufundisha njia bora zaidi za kutazama mali zetu. Kama tumepoteza kazi inabidi tutazame tukio hilo kama njia mpya ya kutupeleka kwenye shughuli nyingine ambayo itatufaa zaidi na kutupa nafasi kubwa zaidi ya kuwasaidia wengine.

Wale wanaoamini katika Uislamu au Ukristo watakubaliana nami kwamba, vitabu vitakatifu vya dini hizo vinahimiza kuwa tukubali kwamba yote mema na mabaya yametoka kwa mungu na yameletwa kwetu kwa sababu ya wema a siyo ubaya. Hili siyo suala la dini tu bali ndiyo ukweli wenyewe, kwamba hakuna tukio baya katika maisha.

Bila shaka kama umeshakumbana na mambo mengi au watu wengi ambao wameshawahi kukumbana na matatizo ya kimaisha, utakubaliana nami kwamba umewshawahi kukutana na watu ambao wanasema mafanikio yao yalikuwa ni matokeo ya mitihani fulani maishani. Mtu anafukuzwa kazi katika mazingira magumu sana, lakini anakuja kufanikiwa kupata kazi au shughuli nyingine ya maana zaidi na pengine kubadili kabisa maisha yake. Wakati kuna mwingine hupoteza kazi katika mazingira sawa kabisa na huyo, lakini yeye akaishia kuchanganyikiwa na kuokota makopo.

Kwa nini basi tusiamini kwamba matukio yote yanayotutokea huwa hayana nguvu ya kutuathiri hadi pale tunapoyapa tafsiri tuitakayo. Kama tukifukuzwa kazi, kwa nini tusilichukulia tukio hilo kama lile la kupata kazi. Huwa tunasema, “lakini hiyo ni vigumu” kwa sababu tumeshazoea kuyatafsiri matukio kwa mazoea tuliyolelewa au kukulia.

Nakuomba kuanzia sasa ujaribu, kama uko kwenye mitihani ya maisha, jiambie kutoka ndani kabisa ya moyo, kwa kuamini kwamba utainuka tena, utaweza kusonga mbele, halafu uone matokeo yake. Kama utajiambia kwamba tukio hilo ni changamoto na linakusaidia kujirekebisha na maisha, ni wazi utashangazwa na matokeo yake. Wewe hutakuwa mtu wa awali kushangazwa na matokeo yake bila shaka.

Naamini kwamba wengi wetu tunapopata matatizo ya kimaisha au mitihani, huwa tunadhani kwamba tuna mikosi, tumefanya makosa na tunaadhibiwa au kuna mkono wa mtu. Lakini ukweli ni kwamba, mitihani ya maisha ni mabadiliko kutoka tukio la aina moja kwenda lingine na matukio yote kwenye maisha yetu yana maana sana kwetu kama tutayatafsiri vizuri akilini mwetu.

Hebu tufikirie…….Kuna idadi kubwa ya watu tunaowafahamu ambao hawana viungo, hawana uwezo na majaaliwa ya elimu, ndugu na jamaa kama tulivyo sisi, lakini watu hawa wamechukulia upungufu wao huo kama sehemu muhimu ya maisha yao, wameukubali na tunaona jinsi wanavyosonga mbele kimaisha.

Sisi ambao tuna viungo vyote, tuna elimu, ndugu na jamaa tele, tena wakiwa wanatupenda na kutujali, bado tunapopatwa na mitihani kidogo tu ya kimaisha tunakata tamaa na kuanza kufanya mambo ambayo hatukutarajiwa hata mara moja kwamba tungekuja kuyafanya.


Kwa nini tusione kwamba kuwa kwetu wakamilifu peke yake ingekuwa ni fundisho kwamba hatupaswi kulalamikia tukio lolote tunaloliona baya linalotukuta kwa sababu tungeweza kupatwa na tukio baya zaidi kama wale ambao tunawaona wanateseka kila siku.

Tujiulize pia, pale tunapopata mafanikio ambayo huwa tunayafurahia sana, huwa tunajiuliza mbona tumepewa sisi tu na wengine hawakupewa? Bila shaka huwa hatujiulizi kwa kudhani kwamba hiyo ni stahili au haki yetu, lakini tunasahau kwamba huwa hatujui anayetupa au kutushushia hayo mema ambaye bila shaka ndiye huyo ambaye kesho atatushushia tunayoyaona mabaya na hapo tutamuuliza, “Inakuwaje mimi tu?”

4 comments:
Andika Maoni Maoni
 1. Kukata tamaa ni kitu ambacho kinatawala sana katika sisi binadamu na wapo wengi ambao wamekata tamaa na sasa wapo tu. Ningependa wengi wangesoma post hii labda wangejifunza kitu. Binafsi nimejifunza kitu. Asante.

  ReplyDelete
 2. Chacha o'Wambura a.k.a Ng'wanambiti!Saturday, December 12, 2009

  somo tosha!

  ReplyDelete
 3. Ni kweli hatutakiwi kukata tamaa, juhudi na maarifa ni msingi wa maendeleo mtu unatakiwa ujitume katika majukumu yako na mara zote usisite kujaribu kitu kipya

  ReplyDelete
 4. ndiyo maana Chachage alikuwa akisisitiza kuwa elimu ni maisha yenyewe siyo ufunguo wa maisha

  ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi