0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Aug 2, 2009

KUFANIKIWA AU KUTOFANIKIWA NI UCHAGUZI WETU WENYEWE

Ukiamini utafanikiwa

Ili kufanikiwa kwenye lengo lolote katika maisha, ni lazima uamini kwamba utafanikiwa. Kama usipofanya hivyo, una nafasi kubwa ya kushindwa.
Unaweza kuwa na malengo mapya uliyoyapanga na ambayo unaanza kujaribu kuyatekeleza. Lakini ni lazima ufanye hivyo ukiwa na imani kubwa kwamba utafanikiwa.
Waweza kuona kazi uliyo nayo hivi sasa haikusaidii sana na hivyo kuamua ghafla kuiacha.
Waweza kufanya hivyo huku ukiwa hujaamua kitu gani cha kufanya, na hivyo kulazimika kutumia kipindi cha pengine miezi sita ama hata zaidi inayofuata kujaribu kufikiria nini cha kufanya.


Huwezi kufanikiwa katika kile unachokitaka kufanya ikiwa hutaamua kuyafanya mawazo yako hayo uliyonayo kuwa vitendo. Hata ukiwa na kiu na hamu kubwa kiasi gani ya kufanikiwa, bila kuhamasisha nafsi yako na kuanza kufuatilia lile unalotaka kulifanya, kufanikiwa itakuwa ndoto kwako. Hilo litashusha ari yako na kujikuta unarudi kulekule ulikotoka, kwenye kazi ya kuajiriwa.
Lakini wakati wote huu, vyanzo vya mafanikio huwepo karibu nawe tayari kutumiwa nawe kwa ajili ya kukuletea mafanikio unayoyataka. Lakini bila kuiamini nafsi yako kwamba unaweza kufanikiwa, huwezi kufanikiwa.


Hivyo ni lazima ujifikirie katika mambo unayoyafanya, unafanya mambo yako yanayokuelekeza kwenye malengo yako ukiwa na imani kwamba utafanikiwa. Je, unayo picha ya mafanikio yako akilini mwako na hisia kwamba hivi ndivyo inavyotakiwa kuwa?
Hebu kaa chini na ufikirie kuhusu mambo uliyowahi kuyafanya na ukashindwa katika kipindi cha miaka michache iliyopita. Jiulize ikiwa kweli ulijiamini kwa dhati kwamba utafanikiwa.
Mara nyingi utakuta katika matukio hayo ulikuwa na mashaka ndani yako kuhusiana na uwezo wako wa kufanikiwa na hivyo iko haja ya kujihamasisha kabla ya kuanza kupiga hatua kuelekea kwenye lengo lako. Unatakiwa kuamini kwamba utafanikiwa.


Ni kwa nini imani hiyo ni muhimu kiasi hicho? Kwa kawaida huwa tunaanza kujenga imani tangu tukiwa wadogo. Mara baada ya kuzaliwa kwetu, huanza kujenga au kujengewa imani.
Na baadaye tunaendelea kujijengea imani wakati tukiendelea kukua na huwa tunabadili imani kutoka za zamani na kujenga mpya, kutegemea vitu vingi. Tunahitaji kufanya haya ili kuyafanya maisha yetu hapa duniani yawe rahisi na ya kweli.


Siku zote tunaamini kwamba tunapoamka vitandani mwetu asubuhi, tunahitajika kuweka miguu yetu chini ili kuweza kusimama ardhini kabla ya kuendelea na shughuli zetu nyingine na si kuruka hewani hadi kwenye dari ili kuweza kutoka vyumbani mwetu kwa shughuli zetu za kawaida.


Tumejifunza hili tangu tukiwa wadogo kabisa na sasa hatuna haja hata ya kufikiria kila siku kwamba hivyo ndivyo tunavyotakiwa kufanya. Vivyo hivyo, pia hatuna haja ya kufikiria ni kwa kiasi gani nguvu ya uvutano ina mchango gani katika kusimama kwetu kila asubuhi tangu tunapoamka vitandani mwetu.


Wakati unapofungua mlango wa nyumba yako, unageuza ufunguo wako kuelekea upande uliko ubao wa kufungia mlango ama upande wa tofauti na mwenendo wa mikono ya saa.
Hiyo ni imani tunayojijengea tangu tukiwa watoto wadogo kabisa, tunapoanza kujifunza kufungua na kufunga milango.


Kila unapokutana na mlango mpya hatuwi na wasiwasi kwamba tunajua vile mlango unavyofunguka kwani tunakuwa na hakika (akilini mwetu) na namna mlango huo utakavyofunguka. Tunazunguusha funguo kuelekea upande uliko mlango tu! Ni rahisi. Hiyo ndiyo imani tuliyonayo.


Huoni sababu ya kufikiria uwezekano wa kukutana na mlango unaofunguka vinginevyo. Lakini hakuna atakayekataa kwamba wengi tumewahi kukutana na milango inayofunguka kwa mwelekeo tofauti na ule tunaoamini ndio utaratibu ‘unaokubalika.’ Inaudhi sana unapokutana nao kwa mara ya kwanza.


Hata baada ya mwaka mzima wa kufungua mlango kwa mwelekeo huo, bado imani uliyojijengea kutokana na uzoefu wako kwamba mlango haufunguki kwa mwelekeo huo, utakuwa nayo, na hivyo utakuwa ukikasirika kila mara utakapofungua mlango huo. Imani unayojijengea moja kwa moja huathiri tabia yako, hata kama imani hiyo si sahihi kama unavyofikiria.
Hebu tufikirie kitu kingine! Dunia ni duara ama si duara? Umelijuaje hili? Si kwamba umeambiwa na watu tu? Una uhakika gani? Wapo wanaoamini kwamba dunia ni ya ubapa kutokana na wanavyoiona kila wanapochungulia madirishani.


Kama ungeamini kwamba dunia ni ya ubapa, ni wazi ungepatwa na wasiwasi mkubwa wakati unaposafiri kwenye mashua kwamba huenda mngefika mwisho na kuangukia nje ya dunia. Lakini hivi ndivyo watu walivyokuwa wakifikiria. Kilikuwa ni kikwazo kikubwa kwa ugunduzi kwa miaka mingi ya mwanzoni. Imani waliyokuwa nayo watu moja kwa moja iliathiri vitendo vyao, na hilo lilikwaza matokeo yao. Fahamu tena kwamba imani si lazima zioneshe ukweli uliopo duniani. Si kila siku milango hufunguliwa kuelekea mwelekeo uliko mlango.
Imani kuhusu dunia kuwa ubapa ilibadilishwa mara wagunduzi walipoanza kuzunguuka dunia. Imani huathiri moja kwa moja matendo yetu hata hivyo. Wakati mwingine, tunachukua hatua hata imani zetu zinapokuwa si sahihi, na hii yaweza kutukwaza. Hii ni kweli kuhusiana na imani tulizonazo kuhusu nafsi zetu na uwezo wetu.


Vipi kuhusu nafsi zetu? Kama tufanyavyo mambo tuliyoyazoea bila kufikiria kutokana na imani tunazojijengea kama vile kufungua mlango, tunafanya hivyo hivyo kutokana na imani tunazojijengea kuhusu nafsi zetu. Ikiwa tutajenga imani za kutukwaza kuhusiana na nini kinawezekana kufanikisha, jibu letu litakuwa kukwamisha matokeo ya vitendo vyetu tunavyochukua. Matokeo yake tunakwaza pia matokeo tunayoyapata.


Ikiwa tunaamini kwamba kuna kila uwezekano wa kushindwa katika kile tunachofanya mawazo yetu ya kina (subconscious mind), itafanya kazi ya kujenga mazingira yatakayounga mkono imani yetu hii. Wakati mambo yanapokuwa magumu, hatutakuwa na haja ya kufanya jitihada zaidi iliyo muhimu katika kufanikiwa; kushindwa kwa mara ya kwanza kutaunga mkono imani yetu hiyo na hivyo kutufanya tukate tamaa na kuachana na kile tunachofanya.

3 comments:
Andika Maoni Maoni
 1. Kaka Kaluse hii post imesimama. Ni wazi wengi huwa tunajiangusha wenyewe. Unaweza kuweka malengo, lakini usiyatekeleze na wala usione hatari kushindwa huko.

  ReplyDelete
 2. Wengi tunakata tamaa mapema. Kwa sababu kubwa ni hii nitanukuu "Huwezi kufanikiwa katika kile unachokitaka kufanya ikiwa hutaamua kuyafanya mawazo yako hayo uliyonayo kuwa vitendo. Hata ukiwa na kiu na hamu kubwa kiasi gani ya kufanikiwa, bila kuhamasisha nafsi yako na kuanza kufuatilia lile unalotaka kulifanya, kufanikiwa itakuwa ndoto kwako. Hilo litashusha ari yako na kujikuta unarudi kulekule ulikotoka, kwenye kazi ya kuajiriwa.
  Lakini wakati wote huu, vyanzo vya mafanikio huwepo karibu nawe tayari kutumiwa nawe kwa ajili ya kukuletea mafanikio unayoyataka. Lakini bila kuiamini nafsi yako kwamba unaweza kufanikiwa, huwezi kufanikiwa." mwisho wa kunukuu. Ahsante Kaka Shabani kwani kila siku unatuletea masomo mahimu sana katika maisha.

  ReplyDelete
 3. Hapa nimejifunza kuliko ninavyoweza kufunza.
  Shukrani saana Kaka

  ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi