0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Aug 15, 2009

WAUAJI WADOGO WA KISHETANI!

Familia ya Lillelid
Wasomaji wapendwa, nimekuwa nikipokea maombi ya wasomaji wa gazeti la Jitambue ambalo limesimama kuchapishwa kutokana na sababu za kiufundi wakitaka nirejee makala zangu za Kesi za Utata ambazo nilikuwa nikiandika katika gazeti hilo.

Naheshimu sana maoni ya wasomaji wangu na kwa kuanzia nimeona nianze na mkasa huu ambao ulitokea nchini marekani mwaka 1997.

Kesi hii niliwahi kuiandika katika gazeti la Jitambue, si vibaya nikirejea Kesi hii wakati nikiandaa makala nyingine.

********************************

Ilikuwa ni jumapili majira ya saa 2:20 usiku, April 6, 1997, kitengo cha ulinzi wa jamii katika mji wa Greene County ulioko jimboni Tennessee nchini Marekani, kilipokea simu kupitia namba ya dharura ya kupokelea matuki ya uhalifu au hatari inayotumika nchini humo.

Mpiga simu alitoa taarifa kuwa katika eneo lao imesikika milio ya bunduki. Iliwachukuw dakika 10 askari wawili waliokuwa zamu katika kitengo hicho, Sajenti Frank Waddell na mkuu wa Kitengo hicho msaidizi Jeff Morgan kufika kwenye eneo la tukio.

Walipofika tu kwenye eneo hilo walipokelewa na hali ya kutisha, kwani kulikuwa na miili ya watu wawili iliyokuwa imelala chini huku ikivuja damu na hivyo kufanya eneo lote la tukio kutapakaa damu.

Miili hiyo ilikuwa imelala pembezoni mwa barabara na ilikuwa ni ya mwanaume na mwanamke. Kwa haraka haraka walionekana kama wanakaribia kufikisha umri wa miaka thelathini au ndio wanatimiza miaka thelathini. Wote wawili walikuwa wamepigwa risasi kadhaa mwilini na walikuwa wameshakufa.

Katika mwili wa mwanamke kulikuwa na mtoto mchanga wa kiume ambaye alikuwa amemlalia mwanamke huyo huku akikoroma na pembeni kidogo kulikuwa na binti wa miaka mitano au sita ambaye naye alikuwa amepigwa risasi, lakini aligundulika kuwa bado yuko hai, ingawa alikuja kufariki saa kadhaa baadae akiwa anatibiwa hospitalini.

Hata hivyo, yule mtoto mchanga ambaye alikuwa amepigwa risasi ya jicho , kama miujiza, madaktari walifanikiwa kuokoa maisha yake. Akieleza hali aliyoikuta katika eneo la tukio mbele ya waandishi wa habari, mkuu wa kitengo cha usalama wa jamii katika eneo hilo Terry Jones, huku akitokwa na machozi alisema “Kwa jinsi tulivyokuta watoto wale ilionekana kama vile walikuwa wamekumbatiwa na wazazi wao kabla hawajakata roho, na ukweli kwamba hatufahamu majina yao au kama ni watu wa familia moja au la”

“hakuna Pochi, vitambulisho, fedha au kitu chcochote kilichopatikana kutoka katika eneo la tukio, ambacho kitaweza kurahisisha kuwatambua wahanga hawa” Aliendelea kufafanua mkuu huyo wa kitengo cha jamii Terry Jones.

Mkuu huyo aliendele kuwaambia waandishi wa habari kuwa hata gari walilokuwa wakisafiria wanafamilia wale nalo halikuwepo katika eneo hilo la tukio.
Akijibu mojawapo ya maswali ya waandishi wa habari, Jones alisema kwamba, hata mwonekano wa familia ile uliashiria kuwa ilikuwa ni familia ya watu wanaoheshimika, hivyo mpaka kufikia hapo wanalichukulia tukio lile kama la mauaji ya kihalifu.

Hata hivyo polisi walikuta gari lingine aina ya Chevrolet likiwa limekwama kwenye mtaro umbali wa mita chache kutoka katika eneo la tukio na namba zake pamoja na vielelezo muhimu vinavyohitajika kuwepo kwenye gari vilikuwa vimeng’olewa, na hata taa ya za mbele za gari hilo zilikuwa bado zinawaka.
Jones aliendelea kusema kuwa anaamini kuwa huenda gari lile aina ya Chevrolet lilikuwa likiendeshwa na wauaji, na analazimika kuamini kuwa wauaaji walikuwa ni zaidi ya mtu mmoja, ambapo waliwalazimisha wanafamilia wale kuendesha gari lao mpaka katika eneo la tukio na baada ya kuwauwa waliamua kutoroka na gari la wanafamilia ile.

Uchunguzi wa awali ulionesha kuwa gari lile la aina ya Chevrolet lilikuwa likimilikiwa na na mama mmoja aitwae Mary Castle, karani wa duka anayeishi Paintsville katika jimbo la Kentucky nchini humo.

Akihojiwa na askari wa upelelezi wa Paintsville aitwae Tom Haney alidai kwamba gari lake liliazimwa na mwanae wa kiume aitwae Joseph Risner (21) siku mbili nyuma na tangu alipochukua gari lake hajapata kumuona, si yeye wala gari. Mama huyo alitoa picha ya mwanae huyo na Haney aliituma kwa njia ya fax haraka kwenda Greene County katika kitengo cha ulinzi wa jamii.

Wakati h huo askari wa Tennessee waliitambua miili ya wanafamilia ile kuwa ni ya Vidar Lillelid aliyekuwa na umri wa miaka 34 mhamiaji kutoka nchini Sweden, mkewe Delfina aliyekuwa na miaka 28, binti yao aitwae Tabitha aliyekuwa na umri wa miaka 6 na mtoto wao mdogo wa kiume aitwae Peter aliyekuwa na umri wa miaka 2.

Familia ile ilikuwa inasafiri ikitokea katika mji wa Johnson ulioko katika jimbo la Kentucky, walikokwenda kuhudhuria mkutano mkuu wa kidini wa dhehebu la mashahidi wa Jehova.

Majira ya sa saba na robo za mchana ikiwa ni kabla ya kutimia masaa 24 tangu tukio lile kuripotiwa gari la Lillelid lilikamatwa na askari wa upande wa Mexico, kutokana na nyaraka za umiliki wa gari lile kutiliwa mashaka na askari wa upande huo.

Watu wote sita waliokuwa wakisafiri na gari hilo wakiwa ni wavulana watatu na wasichana watatu na walikamatwa kwa kutuhumiwa kuiba gari na kuhusika na mauaji ya familia ya Lillelid.

Vijana hao walitambuliwa kwa majina ya Joseph L Risner, aliyekuwa na umri wa miaka 21, Dean Mullins na Karen Howel wote wakiwa na umri wa miaka 20, Natasha Cornet na Crystal Renea Sturgil wakiwa na umri wa miaka 18 na Jason Blake Bryant aliyekuwa na umri wa miaka 15, wote wakiwa ni wakazi wa Paintsville katika jimbo la Kentucky.

Vijana hao walikuwana muonekanao wa kihuni kama walivyo watumiaji wa madawa ya kulevya, kwani walikuwa wamejichora katika miili yao picha za kutisha huku wakiwa wamejitoga masikioni puani,kwenye ulimi, kidevuni, midomoni, kwenye nyusi, na kujivika vipuri, pia walikuwa wamekata nywele zao katika mtindo wa ajabu.

Wapelelezi wa Tennesee walipata shida kidogo katika kufuatilia nyendo za vijana wale kutokea Kentucky hadi katika mpaka wa Mexico. Kwa kmujibu wa maelezo ya watuhumiwa ilionesha kwamba, watuhumiwa wote sita walikutana April 6, 1997 na walipanga kusafiri kwenda katika jimbo la New Orleans ambapo wangekutana na marafiki zao.

Risner aliazima gari la mama yake aina ya Chevrolet na wote sita waliondoka na gari hilo hadi kwa afisa mmoja wa kitengo cha uthibiti wa silaha na kuvuja kasha wakaiba bastola aina ya Caliber namba 25 na makasha mawili ya risasi pamoja na fedha kiasi cha dola 500 za Kimarekani.

Baada ya wizi ule, vijana hao wote sita walisafiri kupitia barabara kuu ya kusini kuelekea jimboni Virginia. Majira ya saa 12:20 za jioni wakiwa wanakatisha viunga vya maeneo ya Virginia walisimamishwa na askari wa usalama barabarani na kutozwa faini kwa kuendesha gari kwa mwendo wa kasi. Risiti waliyopewa baada ya kulipa faini ilikutwa kwenye eneo mla tukio.

Kwa kujibu wa askari wa usalama barabarani wa Virginia walikiri kwamba vijana wale hawakuwa wamelewa wala kuonekana kama walikuwa wametumia dawa za kulevya.

Saa moja baadae gari hilo lilionekana likiwa limeegeshwa kando ya barabara kuu iendayo katika mji wa Greene County Tennesee. Kwa mujibu wa shuhuda aliyeliona gari hilo lililokuwana vijana hao sita, waliokuwa na muonekano wa kihuni alidai kwamba gari hilo lilikaa katika eneo hilo kwa takribani dakika 45.

Wakati huo huo familia ya Lillelid ilikuwa ikisafiri kurejea nyumbani kwao matika mji wa Powell jimboni Tennessee wakiwa katika msafara wa mgari kadhaa yaliyokuwa yakiendeshwa na marafiki zao ambao wote walikuwa wakitokea katika mkutano mkuu wa kidini wa mashahidi wa Jehova.

Inasemekana, Lillelid alikuwa amechoka hivyo akaamua kuegesha gari lake pembeni ya barabara ili apate kupumzika, na kuwaacha rafiki zake wakiendelea na safari. Kumbe wakati Lillelid anaegesha gari lake hakujua kama jirani kulikuwa na gari lingine aina ya Chevrolet limeegeshwa likiw na vijana sita ambao wangekuja kumdhuru.

Mmoja wa mashuhuda alidai kwamba waliwaona watuhumiwa wakiongea na Lillelid na kasha waliyaona magari yote mawili yakiondoka kutoka katika eneo lile.

Polisi wanaamini kwamba huenda gari la Lillelid lilitekwa na watuhumiwa na kundeshwa na mmoja na watuhumiwa hadi katika eneo la tukio ambapio waliwapiga risasi wote na kuwauwa lakini wakimuacha mtoto Peter akiwa amejeruhiwa vibaya.

Huku wakiamini kwamba wamewauwa wote, watuhumiwa waliamua kuondoka na magari yote mawili yaani lile la kwao aina ya Chevrolet pamoja na lile la Lillelid, lakini kutokana na wembamba wa barabara waliyoingia, gari lao lilikwama kwenye mtaro.

Ili kuepuka kupoteza muda waliamua kutelekeza gari lao, lakini kabla ya kulitelekeza gari hilo, waling’oa namba za gari pamoja na nyaraka muhimu ambazo zingefanya gari lile kufahamika mmiliki wake kirahisi. Walichukua fedha, vitu vya thamani na vitambulisho vyote walivyokuwa navyofamilia ya Lillelid ili kuchelewesha kutambuliwa kwao.

Baada ya kukamatwa watuhumiwa wote sita walirejeshwa katika mji wa Greene County Tennessee walikotokea katika jimbo la Arizonana kuwekwa katika gereza kuu la mji huo kwa mahojiano zaidi.

Siku chache baada ya watuhumiwa wote kuwekwa rumande, walikiri kwamba Natasha Cornett ndiye aliyekuwa mkuu wa kikundi na pia msemaji mkuu.

Natasha aliwashangaza askari wa upelelezi pale aliposema kwamba yeye ni mtumishi wa shetaninatasha alifafanua kwamba amekuwa akliwasiliana na shetani tangu akiwa na umri mdogo.

Akihijiwa na polisi kuhusiana na maelezo yake hayo, kwa maneno yake mwenyewe Natasha alisema , “Nadhani nilikuwa naitwa na mtu nisiyemwona, na kulikuwa na roho nisiyoiona ambayo ilikuwa ikizungumza na mimi tangu nikiwa na umri wa miaka miwili. Nimekuwa kwa umri na kimo huku nikiandaliwa kuwa mtumishi wa shetani”

Akjibu mojawapo ya maswali ya askari wa upelelezi, Natasha alikiri kuwa yeye ni mpinzani wa Masihi Yesu Kristo na binti wa shetani.
Natasha alizidi kusisitiza kuwa maisha yake yalitawaliwa na nadharia za ajabu kiasi cha kuasi imani ya kikristo aliyokuwa nayo mama yake.

Maelezo ya Natasha yalitoka katika vyombo vya habari nchini marekani na hivyo kutomfurahisha wakili aliyekuwa akimtetea aitwae Eric Conn. Hata hivyo wakili huyo alimuonya Natasha kutoonge na waandishi wa habari au mtu yeyote kuhusiana na kesi hiyo.

Na ili kujenga mazingira mazuri ya kumtetea mteja wake, wakili huyo aliitisha mkutano wa vyombo vya habari na kukanusha madai yaliyokuwa yakitolewa na mamlaka ya kisheria jimboni Tennessee kwamba mauaji yaliyofanywa na watuhumiwa yalikuwa ni utekelezaji wa imani ya dini ya kishetanina badala yake wakili huyo alisisitiza kwamba watuhumiwa walikuwa na matatizo ya kiakili, ambapo wanalindwa kisheria na kifungu kinachowalinda watu wenye matatizo ya kiakili dhidi ya makosa waliyoyafanya.

“Kila mtu anayeizungumzia kesi hii anaihusisha na dini ya kishetani, hiyo si sahihi hata kidogo,” alikanusha wakili Eric Conn, na hakusita kusema hadharani kuw atatumia kifungu cha sheria kinachowatetea watu wenye matatizo ya kiakili dhidi ya makosa waliyoyafanya.

“Huwezi kuyatenganisha makosa haya na matatizo ya kiakili kwa sababu kulikuwa na nguvu isiyo ya kawaida iliyokuwa ikiwaendesha vijana hawa kufanya yale waliyoyafanya,” alisema wakili huyo.

Hata hivyo pamoja na Natasha kukatazwa kuongea na vyombo vya habariau mtu yeyote kuhusiana na kesi ile, hakuacha kuzungumza na vyombo hivyo kuhusiana na imani yao ya kishetani yeye na watuhumiwa wenzake.

“Kuna wakati najihisi kama nimerukwa na akili, lakini hapana, nadhani mimi sio mwendawazimu” alinukuliwa akisema Natasha.
Kwa mujibu wa rafiki zake Natasha alijulikana kama binti aliyekuwa na tabia ya kuongoza wanaume na tabia hiyo amekuwa nayo hata katika kikundi chao. Natasha alikanusha kwamba alikuwa ni kiongozi wa kundi lao.

“Mimi sikuwa na wafuasi na sisi sio wafuasi wa dini ya kishetani bali ni kikundi cha marafiki tulio na utashi w aina moja” alisema Natasha.
Akizungumzia juu ya minong’ono iliyoanza kuenea kwamba, yeye Natasha alikuwa na uhusiano maalum wa kusagana na mtuhumiwa mwenzie Karen Howell, lakini tuhuma hizo alizikanusha pia.

Akizungumza juu ya minong’ono hiyo, Natasha alisema, “Karen ni rafiki yangu wa karibu na sio urafiki wa kusagana. Kwa kawaida huwa tunabusiana lakini sio kama mnavyofikiria”

Natasha aliongeza kuwa alikuwa na mpango unaoratibiwa na shetani wa kuwaandaa vijana wote duniani ili waasi. Alidai kwamba vita ya mwisho ya Armageddon iko karibu kuanza lakini baba yao shetani hajawaambia tarehe maalum vita hiyo itakapoanza, na aliwaomba waandishi wa habari wawatangazie watoto wote ulimwenguni kusimamia haki na imani zao kwa kuzipigania kwa jinsi watakavyoweza. (Armageddon ni vita takatifu vilivyozungumziwa katika Biblia agano jipya itakavyopiganwa mwiso wa dunia kati ya wafuasi wa shetani na watakatifu kwa mujibu wa maandiko ndani ya Biblia)

Natasha aliongeza kusema kuwa anamwamini wakili wake Eric Conn na nguvu za shetani, “ naamini baba yangu shetani atanisaidia na kunilinda” alisema Natasha.


ITAENDELEA..............................

1 comment:
Andika Maoni Maoni
  1. Inasikitisha sana, na inahuzunisha.
    Bado najiuliza, hivi ni nani wa kulaumiwa hapa. ni hawa watoto, wazazi au jamii iliyowazunguka?

    ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi