0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

http://www.serenahotels.com/serenadaressalaam/default-en.html

Feb 11, 2009

HIVI HATUWEZI KUBADILIKA?

Wenzetu wamewezaje?
Ni nani atakaye kuja siku moja kuliona jambo hili, kuuona ukweli huu, kwamba nchi hii haina umaskini wa rasilimali, wala umasikini wa nguvu kazi, bali ina umasikini mkubwa wenye kutisha na kukera wa namna nzuri ya kufikiri. Kuna kukomboka kwingi katika kufikiri kiasi kwamba watu wa nchi hii wanaonekana kama kituko katika mitindo yao mingi ya kimaisha.

Ni kweli kwamba wananchi wengi wa nchi hii ni wapole, wanapenda amani na uaminifu, lakini ndani ya sura hiyo kumelala ujinga, kutojiamini, na hofu kuu iliyoambatana na kushindwa kwao kujijua. Wananchi wengi wakiwapo pia viongozi wamekuwa wanaishi kwa kufuata utaratibu maalumu ambao tunauita mazoea ya namna ya kufikiri.

Kuna kila kitu katika nchi hii, ambacho binadamu anakihitaji ili aweze kuishi katika ubora unaopimika. Kuna ardhi, maji ya kutosha, wanyama, madini, na nguvu kazi ya kutosha lakini kila siku hali ya mtanzania inazidi kudidimia, malalamiko yanazidi, kutoaminiana kunaongezeka na ulaghai unashamiri. Kila kunapokucha kinachoboreka ni njia bora za udanganyifu, ulaji rushwa na ubabaishaji. Kila jinsi umri unavyosogea ndivyo jinsi kufikiri vizuri kunavyo didimia kwenye tope la ufahamu.

Tunapenda sana kuishi katika dunia ambayo haipo tunapenda kuyatazama mambo au masuala mengi yanayotuhusu kimakengeza kana kwamba hayatuhusu sisi. Hali hii bila shaka ni matokeo ya kufikiri vibaya tuna maana ya kuyatazama mambo au kila hali kwa imani ya kushindwa, kuharibu na machungu. kuyatazama mambo ya kila hali katika majaribio kwamba yatajiendesha yenyewe na kufikia mafanikio bila juhudi wala maarifa yetu.

Ndiyo maana yanaibuka masuala kama ya RICHMOND na EPA kama ilivyokuwa NET GROUP. Kila mmoja anajitahidi kujaribu kujidanganya kwa kudhani kuwa kuna miujiza ambayo huja tu tukiwa tumelala na mambo kuwa sawa na hakuna haja kwetu kuutazama ukweli na kuufanyia kazi. Mambo yanapobadilika, kwa sababu tuna asili ya ubishi, bila kujali tunabisha, na kujikuta tukiingia kwenye kulumbana kwa kuhemkwa bila kutafakari kwa kina.

Hebu tujiulize kuhusu Air Tanzania (ATCL) ni kweli serikali ina haki ya kudai kwamba shirika hilo limeshindwa kazi? Hivi Serikali imeshindwa kuwatumia wataalamu wetu hapa nchini kulinusuru hili shirika?

Ukweli ni kwamba hali mbaya inayoyakabili haya mashirika yetu ya umma na mahali pengine ikiwemo kwenye shughuli zetu za binafsi hazitokani na uwezo wa kimapato uliomo humo au tulio nao bali zaidi kwa namna tuvyofikiri. Mazoea yalisha tujengea kufikiri kwa namna fulani kuhusu kazi na uwajibikaji. Tulishajengewa kufikiri ambako kunatusukuma kudhani kwamba kila wakati na katika kila kitu tunadanganywa na kuonewa bila kutazama ukweli.

Kikubwa ambacho serikali na wananchi wanapaswa kukifahamu ni kwamba tumeshatoka kwenye maisha ya miaka ya 1970 na tuko mahali pengine kabisa. Dunia imebadilika sana na inaanza kuingia mahali ambapo wale waliofikiri vizuri ndiyo pekee wenye nafasi ya kufikia mafanikio wanayoyataka. Kujidanganya kwa kudhani kwamba kutafuta huruma, kuviringa maneno kwa njia tamu kutasaidia katika kufikia mafanikio ni kupoteza muda wetu bure.

Kama hatuwezi kutimiza wajibu wetu ni ujinga mkubwa kutarajia kupata haki zetu, na kutumia mabavu kutatua matatizo yetu hutuingiza kwenye kiza kikubwa zaidi cha utambuzi ufahamu na hatima yake siku zote ni kukwama.

Ni vizuri kujiuliza kila wakati kama tunachodai ni haki yetu kweli au tunachowanyima wengine siyo haki yao kweli. Tukishindwa kujiuliza maswali ya namna hii tutakuwa hatujitendei haki kwasababu kila wakati tutahisi kuwa tumeibeba dunia na pia tutaweza kuhisi kwamba hatupendwi na kuheshimiwa. Muda wa kujidanganya umeshapita siku nyingi, hali halisi ndiyo muongozo wa maisha kwa sasa.

3 comments:
Andika Maoni Maoni
  1. Tukumbuke tu lakini kuwa hata ya wenzetu hayako perfect.

    Kumbuka Swissair ilikufa kutokana na Uswisi nchi ijulikanayo kwa kufanikisha ,kushindwa na Itali, Alitalia imewashinda Waitali hivi karibuni.

    Kwa hiyo sio kwamba natetea Ubovu wa Tanzania lakini kuna mambo ni magumu hasa kutokana na mfumo uliopo karibu dunia nzima ambao ni mbovu.

    Angalia tu akina Obama wanavyohaha na serikali ya Marekani kwa madeni kibao ingawa ndio nchi isemekayo ni tajiri kuliko vyote.

    Karibu mengine yote umesema Mkuu na nakubaliana nayo .

    Kweli tunahitaji mwamko mpya wa kufikiri katika kutatua matatizo yetu.Na hatuna wakumuachia kama tunataka kuwa huru na kujivuni ya kwetu.Wenzetu sasa hivi wameshastukia wamechemsha na wanaweka vichwa kushughulikia na sisi naona bado hata mafisadi wanatushinda: Kuna kipindi huwa siwashangai Wachina kwa kuamua kuwa wakikudaka umefisadi adhabu kifo.

    ReplyDelete
  2. Naomba nikunukuu:

    "Kuna kila kitu katika nchi hii, ambacho binadamu anakihitaji ili aweze kuishi katika ubora unaopimika. Kuna ardhi, maji ya kutosha, wanyama, madini, na nguvu kazi ya kutosha lakini kila siku hali ya mtanzania inazidi kudidimia, malalamiko yanazidi, kutoaminiana kunaongezeka na ulaghai unashamiri. Kila kunapokucha kinachoboreka ni njia bora za udanganyifu, ulaji rushwa na ubabaishaji. Kila jinsi umri unavyosogea ndivyo jinsi kufikiri vizuri kunavyo didimia kwenye tope la ufahamu".

    Matambuzi mtambuzi mtambuzi....

    Hebu kwanza niwaulize wanablog wenzangu, hivi hizi busara tunazoandika zinasomwa na wanasiasa wetu kweli?
    Jana nimemsikia Muheshimiwa saaana waziri mkuu Pinda akisema kuwa kuna haja ya vyuo vyetu kufundisha utaalamu wa kuingia mikataba ili tusije tukajikuta tumeuza nchi huko mbeleni, kwani mikataba mingi mibovu ilitokana na kutokuwa na utaalamu wa kusoma na kuichambua mikataba hiyo(Hili sidhani kama lina ukweli)

    Hebu naomba tujiulize, hivi tangu kipindi cha mikataba ya kina Sultani Mangungo wa Mvomero mpaka leo hatujajifunza mambo haya? Tulikuwa tunangoja nini?

    Nadhani pia kuna haja ya kufundishwa kwa elimu hii ya utambuzi huko mashuleni ili vijana wengi waweze kujitambua, kwani wakijitambua sidhani kama haya anayoyasema kaka Mtambuzi yanaweza kutokea.

    Ahsante kwa kutufumbua macho....

    ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi