0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

http://www.serenahotels.com/serenadaressalaam/default-en.html

Dec 1, 2008

KWA NINI MUDA UKUENDESHE?

Kwao hakuna kitu kinachoitwa muda.
Nilipoandika kuhusu mwili wa hisia, bwana Kitururu alikuja na hoja kwamba, ni vigumu sana kwetu kuuratibu mwili wa hisia kwa sababu ya ubize wa shuguli zetu za kila siku. Ukweli ni kwamba nilipinga hoja yake. Kwa nini?.
Kwa sababu wanaadamu wamejilundikia majukumu mengi kutokana na ushindani, kila mtu siku hizi anataka kushindana, katika kutafuta kuuridhisha mwili, ambao nao kamwe hauridhiki. Watu wanaishi kwa utashi na si kwa uhitaji, na ndio sababu ya tunashuhudia watu wakisingizia kuwa bize au kukimbizana na muda kutokana na mikanganyiko ya majukumu waliyojiwekea.

Kuna wakati niliwahi kusoma habari za watu wa imani ya Kihindu na wale wa imani ya Buddha, ambao kwao suala la muda au kuwa bize haliko, yaani hakuna kitu kinachoitwa muda kwenye maisha yao. Nami nakubaliana nao. Kuna wanaoamini kuwa muda ni pesa, au wanoamini kwamba muda una nguvu na unahitaji kutumiwa kwa njia ambayo inaonyesha kwamba unapewa heshima yake, ambayo ni lazima iwe kubwa kuliko binadamu mwenyewe.

Mtu asipokuwa makini anaweza kukubaliana kabisa na kauli au dhana hizi ambazo kwa nje zinaonekana zina uzito, wakati kwa ndani hazina kitu, ni tupu. Ni kauli au dhana ambazo zinaashiria kwamba, muda ulivumbuliwa na sio kwamba uliumbwa na binadamu.
Naamini unafahamu tofauti kati ya kuvumbua na kuumba. Kwa kawaida tunavumbua kitu ambacho ni cha kimaumbile na kilikuwepo siku zote, isipokuwa hakuna aliyekuwa amebaini kuwepo kwake. Kuumba ina maana ya kutengeneza kitu ambapo hapo awali hakikuwepo au kilikuwepo na kinatengenezwa tena na tena.
Binadamu alivumbua muda, kwani haukuwepo hapo awali. Mungu hakutengeneza kitu kinachoitwa sekunde, dakika, saa, siku, wiki, mwezi, mwaka, muongo, karne na vyote unavyovijua vyenye kupima muda. Mungu alitengeneza vile vitu ambavyo binadamu anadhani vilitengenezwa kwa sababu ya kupima muda. Wanatumia mzunguko wa dunia kwenye mhimili wake wa kulizunguka jua kama kipimo cha muda.

Lengo la mungu kufanya mizunguko hiyo haikuwa kupata muda, bali kitu kingine kabisa. Ndio maana suala la muda limeanza juzi tu, binadamu akiwa tayari ni mjanja. Kuna kuishi na kutenda yale ambayo mtu anaamini ndio yaliyomleta hapa duniani, lakini hakuna muda. Binadamu amevumbua muda kwa lengo la kujipa maradhi ya moyo, hofu na mashaka. Amevumbua muda katika hofu zake za kukabili kutokujua kwake amekuja hapa duniani kufanya nini. Kwa sababu ya muda anakwambia, “maisha ni mafupi sana”, au “ponda mali kufa kwaja”

Kama ukiweza kuishi bila kujali muda, unaweza kuanza kuhisi tofauti. Nikisema kuishi bila kujali muda, sina maana kwamba ukiambiwa umalize kazi uliopewa leo ukatae, hapana. Sisemi kwamba ukiambiwa mradi uliopewa ukamilike mwezi ujao, useme, “nitakamilisha siku yoyote’, hapana. Unapaswa kukumbuka kwamba ni wajibu wako kufanya kwa juhudi, kufanya kwa dhamira na kujitolea zaidi na zaidi, na sio juu yako kuendeshwa na muda wa mwisho uliopewa kukamilisha mradi huo (deadline)

Kama umefanya na imefikia mahali huwezi kukamilisha kwa kadiri ya muda uliojiwekea, au uliopewa, basi huna haja ya kujiuwa. Kama ni kazi yako, unajua namna ya kujiambia , na kama ni kazi ya mtu, ni suala la kujieleza na kujionesha ni kwa nini umeshindwa kwenda kwa mujibu wa ulivyotaka wewe. Kumbuka kwamba dunia hii imekuwepo na ilibeba watu, wanyama na mimea ya kila aina, lakini imepita yote. Hata kama utafanya usiku na mchana na asubuhi na jioni ili kuwahi muda usiishe, utaondoka nawe pia, ukiwa hujamaliza unayotaka kumaliza.


This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi