0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Nov 11, 2008

UTAMBUZI NI NINI?Mimi nimejitambua, wewe je?

Haya wasomaji wa blog hii, leo nimerudi tena, baada ya ya pilika pilika za hapana pale ambazo zilinizuia hata kuweka mawili matatu katika blog hii ili tuendelee kujifunza maarifa haya ya utambuzi,

Leo sitaweka kile nilichopanga kukiweka katika muendelezo wa makala zangu na badala yake nimeona ni vyema nimjibu yule mdau wa Arusha, aliyetaka kujua sababu ya kuiita Blog yangu Utambuzi na Kujitambua.

Niliamua kuiita blog yangu hii Utambuzi na Kujitambua kwa sababu Blog hii itakuwa ikijihusisha na kuandika makala mbalimbali juu ya maarifa haya ya Utambuzi. Hii itawasaidia wale ambao bado hawajajitambua waweze kujitambua.

Je Utambuzi ni nini?

Chimbuko la maarifa haya ni bara la Asia. Ni maarifa ya siku nyingi sana.
Yana majina tofauti tofauti kutegemea na nchi au mahali ingawa kuna
vipengele ambavyo havitofautiani.

Kujitambua maana yake kukua kimwili, kiakili, kihisia na kiroho kwa njia
ambayo itakusaidia wewe na watu wanaokuzunguka. Ni kuachana na
mazoea, kuachana na akili ya kupewa (inayokuumiza au inayowaumiza
wengine), kuwa na akili yako (isiyokuumiza au isiyowaumiza wengine).
Kumbuka, tunapojifunza maarifa haya, hatuzungumzii dini wala sayansi,
tunazungumzia maarifa ambayo yako juu ya hivi. Ingawa kuna mahali
ambapo dini na sayansi inatumika kama rejea.

Tunajifunza Maarifa haya ya utambuzi ili:
· Yatusaidie kumudu kukabiliana na vikwazo na vurugu za maisha.
· Tuyaone maisha kwamba ni mepesi na siyo mzigo. Tuweze kuyaona
maisha katika upande wa pili.
· Tuwe na amani, furaha na ridhiko la kweli katika maisha.
· Tuweze kuishi katika maisha ya uhitaji na siyo utashi.
· Tuweze kufahamu kwamba sisi siyo huu mwili unaoonekana, na hivyo tuishi sisi kama sisi na siyo sisi kama mwili huu unaoonekana.
· Yatuwezeshe kumudu kufanya mambo kama sisi na siyo kama baba,
mama, shangazi, mjomba, jamii au watu wengine. Sisi ni kasuku au
roboti wa baba/mama au jamii. Jiulize kila unachofanya kama hufanyi
kile kile alichokuwa anafanya baba/mama au kama hufanyi kwa ajili ya
jamii.
· Tuweze kuishi maisha halisi kwani haya tunayoishi siyo halisi, ni
ya bandia.

Tunapata matatizo mengi kwa sababu tunaamini sisi ni huu mwili
unaoonekana, tumejifunga sana na huu mwili (tumekuwa wafungwa
wa mwili). Ndiyo maana unapofanya jambo baya unasingizia ibilisi.
Huyu ibilisi ni nani/nini?
Upo msemo unaosema kuwa “Ibilisi wa mtu ni mtu mwenyewe”
Kwa nini? Kwa sababu Ibilisi hawezi kutoka nje yako bali anatoka ndani yako, yaani kila mtu anao uwezo wa kudhibiti mambo mabaya dhidi yake.
Kwa hiyo ukitokewa na jambo baya umejitakia, hakuna wa kumlaumu bali ni wewe mwenyewe.

kwa kawaida mtoto anapozaliwa huwa hana utambuzi, hajui yeye ni
nani. Kitu cha kwanza anachokibaini ni vitu vingine (vya nje). macho
hufunuka kuangalia mbele, mikono hushika watu au vitu vingine,
masikio husikia watu au vitu vingine, ulimi huonja chakula na pua
hunusa watu au vitu vingine. Milango yote mitano ya maarifa
hufunguka, yote ikiwa inahusiana na vitu vya nje.

Mtu wa kwanza kumtambua ni mama yake na siyo yeye (hajijui).
Baadaye hutambua mwili wake (ambao pia ni nje yake). Mwili
huhusiana na dunia hii ya nje. Akiwa na njaa hulia ili anyonyeshwe
kuulisha mwili wake, akiumwa hivyo hivyo. Akishiba au kupona,
huusahau mwili wake, hana habari nao tena.

Mama huanza kumwambia yeye ni nani, huanza kumsifu au kumkaripia.
Akisifiwa wewe mtoto mzuri, hutabasamu na kujisikia vizuri, huhisi
kukubaliwa na kujiona mwenye thamani. Hapa ndipo choyo cha
kujipenda huanza (huzaliwa). Choyo (ubinafsi) ni ile tabia ya kutotaka
kutoa kitu kumpa mwingine (tabia ya kunyima). Hapa ndipo mtoto
huanza kujitambua kuwa yeye ingawa kujitambua huku ni taswira ya
kujitambua, siyo halisi.

Bado hajawa yeye halisi, anachojua ni wengine wanasema nini kuhusu yeye. Lakini kama hakuna anayemjali na kumuonyesha kwamba ana maana, ana thamani hapa napo choyo kingine cha kujipenda huzaliwa, lakini hiki ni choyo cha ubaya; visasi; huzuni; kukataliwa; kujihisi dhaifu, mnyonge na asiye na thamani.

Hivyo anaanza mama; baba; dada; wajomba; shangazi; msichana wa kazi;
majirani; walimu; marafiki n.k. wote humwambia yeye ni nani; Hapa
mtoto huchanganyikiwa kwani maoni kuhusu yeye ni nani huongezeka,
huwa tofauti na mengi zaidi kutegemea chanzo yalipotoka.

Kama mtoto angeishi peke yake bila kukutana na watu asingekuwa na choyo cha kujipenda zaidi lakini asingejitambua kikweli (yeye kikweli) angekuwa kama mnyama ambaye hana choyo cha kujipenda. Choyo cha kujipenda zaidi ni hitaji (hitaji la kijamii). Kila kitu kinatuambia sisi ni nani, siyo sisi kujiambia sisi ni nani, hatuwezi kujiambia sisi ni nani kwa sababu hatujui kwamba tupo.

Wahuni, marafiki, na majirani ndiyo wanaokuambia wewe ni nani, hivyo hatua kwa hatua kila mmoja anaboresha choyo chako cha kujipenda zaidi; kila mmoja anajaribu kukirekebisha na kukiboresha choyo chako ili usiwe tatizo kwa jamii. Hivyo wewe ni jamii na siyo wewe kwa sababu kuanzia mama; marafiki; walimu n.k; ndiyo waliokuambia wewe ni nani.

Umefungwa sana na jamii; kiasi kwamba kuwa wewe siyo jambo rahisi kiasi hicho. Unakula kwa sababu wengine wanakula; unavaa suti kwa kwa sababu wengine wanavaa; unakwenda kuzika kwa sababu wengine wanakwenda, unalia msibani kwa sababu wengine wanalia; unakwenda msikitini/ kanisani kwa sababu wengine wanakwenda- huwezi tena kuwa wewe kwa sababu ya hicho choyo.

Mfano: mtu akiua mtaani mtu mmoja anaitwa hatari sana; mwingine akaua vitani watu laki moja anaitwa shujaa. Jamii imekubali kuua vitani ni sahihi; mtaani siyo sahihi; jiulize swali hili ili uone jamii ilivyokufunga na hivyo ni ngumu kuwa wewe. Umekuwa jamii tangu kuzaliwa kwako. Kinachokubaliwa na jamii ndiyo sahihi hata kama kinanuka kiasi gani. Hicho ndicho unachotakiwa kuwa kwa sababu wewe ni jamii na siyo wewe.

Hutakiwi kuwa wewe, na ukiwa wewe jamii itakutema mara moja. Ukweli unatakiwa uwe nao wewe na siyo jamii. Lakini bahati mbaya hujawahi kuwa wewe, siku zote umekuwa jamii, hivyo unasikiliza Inasemaje kuhusu wewe na inakutaka uishi vipi. Ukiwa wewe jamii itaona umeasi au umekuwa kichaa.

Jamii haitaki ujitambue (ujue wewe ni nani). Ukijitambua utakoma kuwa jamii na jamii haiko tayari kukupoteza mtumwa wake. Jamii inakutumia kwa faida ya jamii. Ukiwa wewe jamii haiwezi kukutumia itakavyo. Ukifanya jambo zuri unapendwa na kusifiwa; na ukifanya jambo baya unachukiwa na kubezwa. Hii hujenga choyo cha kujipenda zaidi ambacho hutaka kushibishwa kila siku.

Mtu atajitahidi kufanya kile ambacho jamii inampangia ili kushibisha choyo alichopewa na jamii husika. Atataka gari na nyumba kwa sababu jamii imemwambia ni vya maana na vinampa thamani siyo kwa sababu yeye anavitaka. Atataka digrii, mke mzuri, utajiri, umaarufu yote ikiwa ni choyo alichopewa na jamii.

Kila siku tunatafuta sisi ni akina nani kupitia kwa watu wengine, wakituona kututambua, kutusifia ndipo tunahisi kuwa sisi. Jamii inayumba kila siku kuhusu kipi ni kipi na hivyo na sisi tunayumba kila siku kwa sababu sisi ni jamii. Kumbuka wakati unazaliwa ulishakuwa wewe na uwewe wako bado unao. Lakini kwa sababu umepewa uwewe mwingine na jamii ndiyo maana kuchanyikiwa na kujuta ni kwingi sana.

Ni hadi hapo utakapovua uwewe uliopewa na jamii na kubaki na uwewe uliozaliwa nao (kuwa wewe halisi), ndipo kuchanganyikiwa na kujuta kutaisha. Inawezekana!!!

Binadamu anahangaika sana na maisha. Anatafuta mambo ya nje
(gari, pesa, mke mzuri, mume anayejali, elimu n.k.) ili yampe
nafuu (furaha, amani na ridhiko). Lakini, anapoyapata anajikuta
hayampi nafuu badala yake yanampa maumivu.

Mambo ya nje hayawezi kutupa nafuu hadi tuingie ndani yetu (ni wapi huko?). Tutapata jibu kwa kadri tunavyoendelea kufuatilia Blog hii ili uweze kujifunza maarifa haya vizuri zaidi, na hatimaye tutajijua sisi kama sisi na siyo sisi kama mwili huu unaoonekana, hisia, mawazo (akili) au roho. Ni vema kutazama miili hiyo kwani ndiyo ambayo itatusaidia kujua hasa ni wapi tuendako kwenye maisha haya na pengine kujua maisha haya yana maana gani kwetu. Hii inaweza kutupunguzia mizunguko na mahangaiko ambayo kiukweli hayana maana.

Maarifa haya unaweza kuyapata katika madarasa yaliyoko Kimara Rombo upande wa kulia kama unaelekea Morogoro mji kasoro bahari, lipo jengo limeandikwa "FAJI Elimu ya Utambuzi inapatikana hapa" Zamani lilikuwa limeandikwa "Familia ya Jitambue"
Au unaweza kuwasiliana na mwezeshaji Dr. John Simbila kwa namba hii 0713 250701

No comments:
Andika Maoni Maoni

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi