0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Nov 23, 2008

HIVI SISI NI NANI?

Sisi hatutakufa bali miili yetu ndiyo itakayokufa na kuzikwa mavumbini.
Nimekuwa na wakati mgumu kuweka mada zangu za namna ya kufikiri vizuri kwa sababu zimekuwa zikiacha maswali mengi kwa wasomaji wa blog hii ya Utambuzi.
Nadhani nilifanya makosa, kwa sababu tangu mwanzo sikuwahi kuweka msingi wa maarifa haya ya utambuzi kwa kuzungumzia kuwa sisi ni nani.
Kimsingi tukijua sisi ni nani nadhani mada zinazofuata hazitawapa shida wasomaji wablog hii.

Hivi sisi ni nani?

Ni kweli sisi ni hii miili inayoonekana (miili ya nyama)?, au ni majina yetu? Sura zetu? Makabila yetu? Akili zetu? Jinsia zetu? Hasira zetu?
Kwa kutaja hivi vyote, bado swali halijajibiwa.
Sisi tuna miili (inayoonekana), ambayo inatuwezesha kuishi kwenye maisha haya ya duniani, tuna mwili wa hisia, mwili wa akili na mwili wa roho (siyo dini). Kuna wakati mwingine, huwa tunajibainisha na miili minne. Lakini swali bado halijajibiwa.

Mwili unaoonekana:

hivi umeshawahi kujiuliza hata siku moja, ni kwa nini unavaa vizuri, unakula vizuri, unataka kujenga nyumba nzuri, kumiliki mali, kufanya starehe ili kuupa mwili raha au kuwa maarufu. Jibu ni kwamba unataka kuridhika. Ni kweli ukipata vitu hivyo vyote utaridhika? Jibu ni hapana. Je huoni kwamba, hii ni taarifa rasmi kwamba sisi siyo huu mwili?

Hebu tuangalie kwamba sisi tulitokana na nini?
Ulitoka kwa wazazi. Baba alitoa mbegu, ambazo kwa sehemu kubwa ni protini (chakula alacho). Kwa kufanya tendo la ndoa mara moja mwanamme hutoa cc 5 za manii (ujazo wa kijiko kimoja cha chai). Kila cc moja ina mbegu zipatazo milioni 120. Hivyo, cc 5 za manii, zina mbegu zipatazo milioni 600. Kati ya hizi, ni mbegu moja tu inayotakiwa kurutubisha yai ili azaliwe mtoto, ni ajabu eee!

Mbegu moja kati ya mbegu milioni 600. Ni uwiano mbaya sana kama siyo kituko. Kama wewe ni huu mwili, basi una bahati sana, kati ya watu milioni 600 aliowatoa baba ukabahatika wewe peke yako. Mama naye alitoa yai. Kila mwezi hutoa yai moja ambalo likirutubishwa anazaliwa mtoto.

Halafu mama naye hutoa yai moja kila mwezi, kwa mwaka mmoja hutoa mayai 12. kati ya haya ni mangapi hurutubishwa? Kumbuka, mbegu na yai vilitokana na vyakula ambavyo vilioteshwa au kupandwa kwenye udongo wenye rutuba (mbolea) na maji. Maji na mbolea vilitoka wapi? Ni mzunguko usio na mwisho wala mwanzo.

Binadamu hajui hata huo mwanzo halisi wa mwili wake, achilia mbali hisia zake, akili/mawazo yake na roho yake. Ngumu zaidi ni yeye mwenyewe ambaye ndiye mwenye kuitumia miili hiyo.

Dini zote zinasema baada ya kufa watakatifu watakaa milele peponi/mbinguni. Watenda dhambi/waovu watachomwa moto milele au watapelekwa jehanamu. Watu hawa wote (watakatifu na waovu) hawatatumia miili hii tuliyonayo. Watakuwa katika hali nyingine, pengine ni hali ile ile waliyokuwa nayo kabla hawajapata hii miili inayoonekana.

Milele maana yake hakuna mwisho. Kitu chochote kisicho na mwisho hakina mwanzo. Hivyo, binadamu hana mwanzo wala mwisho. Hebu jiulize, mwanzo wa kitu ni kizalisha au kizaliwa? Wewe siyo mwili kama unavyofikiri. Kama unaamini wewe ni mwili, basi una mwanzo na mwisho.

Na kama una mwanzo na mwisho, maisha hayana maana yoyote. Hii ni kwa sababu, dunia ina mamilioni ya miaka, wewe unaishi miaka 70 au 80 kama umejilinda sana. Huu pia ni uwiano mbaya sana- mamilioni ya miaka kwa miaka yako 70. Ni kweli MUNGU aumbe mtu kwa mfano wake, halafu aishi miaka 70, 10, au siku moja ndani ya miaka mamilioni ya dunia? Bila shaka angekuwa kituko.

Lakini pia, dini zinasema, mungu alimuumba binadamu kwa udongo kisha akampulizia pumzi akawa hai. Kuna dini zingine zinasema, sina uhakika kama zote zinasema hivi, wakati wa kuuzika mwili, yule anayeongoza mazishi utamsikia akisema, ulikuwa mavumbi na mavumbini utarudi. Je, wewe ni haya mavumbi (udongo) au ile pumzi aliyoipulizia mungu baada ya kuuumba huu mwili kwa kutumia udongo? Ni swali letu sote. Ili upate jibu, toka nje ya dini kwanza kwani ukiwa ndani hutaweza kupata jibu sahihi, jiulize haya maswali kana kwamba huna dini yoyote. Sisemi uache dini yako, la hasha!!!
Magonjwa: ukiumwa huwa unasemaje? Mwili wangu unauma, mkono wangu unauma, kichwa changu kinauma (changu nani?)
Lakini hata ukifa watu watasema: mwili wa marehemu utasafirishwa kwenda Arusha (mwenye huo mwili ni nani? Yuko wapi?). Kama mtu ni mwembamba, anakula mapochopocho lakini hanenepi, utamsikia akisema, mwili wangu hauna shukrani (wangu nani?).
Kuharibika kwa mimba: hebu jiulize, kwa nini mimba huwa zinaharibika? Unaweza kukadiria, kwa siku moja ni mimba ngapi huwa zinaharibika? Ukienda kumuuliza mtaalamu yoyote wa tiba, atakutajia sababu nyingi sana zinazopelekea mimba kuharibika, ikiwemo ile ya mimba kuharibika yenyewe au kuharibiwa kwa makusudi.

Lakini bado jibu halijajibiwa, kwa nini iharibike yenyewe au iharibiwe? Je kuharibu (kutoa) mimba kuna ubaya gani? Huo ubaya unaouona wewe, unafikiri huyo anayetoa hiyo
mimba anauona pia? Kama hauoni kwa nini?. Ni kweli kilicho kibaya/kizuri kwako na kwa wengine kiko hivyo? Kwa nini?. Jiulize tena.

Hivi kama kusingekuwa na kuharibika au kuharibiwa kwa
mimba dunia ingekuwaje? Bila shaka ingekuwa imemalizika kutokana na wingi wa watu. Nasema hivyo kwa sababu, ukiangalia idadi ya mimba zinazoharibika na zinazoharibiwa kwa siku moja zinaweza kuwa sawa au ni nyingi kuliko idadi ya watoto wanaozaliwa kwa siku moja. Lakini si mimba zote zinaweza kuharibika au kuharibiwa, kuna zingine huharibika kirahisi sana hata kama mwenye nayo ataitunza kama yai, kuna zingine huharibiwa kirahisi sana hata kwa kunywa dose ya kawaida ya dawa au kwa kufanya kazi nzito kidogo, unafikiri ni kwa nini?.

Mfano; mama anaweza akawa anafanya kazi nzito kila siku,
akanywa dawa za kila aina au akatumia kila njia kuharibu mimba aliyonayo ikiwemo ile ya kwenda kwa madaktari lakini mimba isiharibike, unafikiri ni kwa nini? Je, nikikuambia kwamba zile zinazoharibika hazijapata mtu wa kuutumia huo mwili utakubaliana na mimi? Pia nikikuambia kwamba zile zinazokataa kutoka tayari zimeshapata mwenyewe ambaye atautumia huo mwili, utakubaliana na mimi? Kama hukubaliani na mimi, una sababu za msingi za kutokukubali? Ukijiuliza kwa kina, hatimaye utapata jibu.

Jamii inasemaje kuhusu wewe/sisi ni nani?

Mwili ni nini? Je mwili una thamani gani kwetu? Hivi kama mwili ungekuwa na maana sana, ungekimbizwa mochuari na kuhifadhiwa ili usiharibike baada ya mtu kufa? Au ungepakwa asali au kuchomwa sindano ili usiharibike na kuleta usumbufu wa harufu na maradhi?

Mwili siyo mimi wala wewe. Mwili haujawahi kuwa mwenye mwili na hautakuja kuwa. Mwili ni kama tochi tu, ambayo umeiazima tu ili iweze kukusaidia kufika kijiji cha pili, kutokana na giza na njia ya uchochoro ambayo unatakiwa kuipita ili kufika kijiji hicho cha pili.

Mwili ni kifaa na siyo wewe, bali wewe unakitumia kifaa hicho. Binadamu anajibainisha kwenye maisha haya ya hapa duniani kupitia mwili wake, lakini yeye siyo mwili. Mwili ni ubainisho, ni chombo cha kutumika kwa kusudi la kidunia tu.

Baada ya muda mwili hukoma kuwepo, hujimaliza wenyewe au kumalizwa, ili binadamu amudu kuingia hatua nyingine ya maisha ambayo haitumii au haihitaji mwili. Tangu ulipozaliwa umeoneshwa na kufundishwa kwamba, wewe ni mwili kama njia zote.

Akili yako imeshika kutu kwa kuamini kwamba, mwili ni wewe na wewe ni mwili. Huna uwezo tena wa kuuona ukweli, kwa sababu vipimo vyako vyote kuhusu maisha vinaishia kwenye akili, ambayo nayo pia haikuhusu, siyo yako, umepachikwa tu.
Kwa ujinga huu wa kutojua mwili ni nini na sisi ni nani, ndipo ambapo tunaingia kwenye ujinga wa kuendeshwa na miili yetu, hisia zetu na akili. Kila mmoja anaamini kwamba, mwili wake ukipotea, ukishindwa kutumika, yaani akifa, basi huo ndiyo mwisho wake. Kama hiyo ni kweli, ina maana binadamu hana maana kabisa, ni upuuzi usofaa kuelezewa.

Yaani binadamu amekuwepo ili awepo kwa mwezi mmoja, miaka kumi, hamsini, sabini, tisini, au mia tu. Halafu baada ya hapo basi. Huu ni uongo mkubwa sana, unaoweza kukubaliwa na akili makapi ya kulishwa tu;Anayetafakari zaidi kidogo, atabaini kwamba, mwili ni mwili tu ni kasha tu.
Mwili ni kasha ambalo muda wake wa kutumika ukiisha mtumiaji au(wewe) analiacha kwa sababu haliwezi kukidhi kile anachokihitaji hapa duniani. Mtumiaji anachukua kingine ambacho kinakidhi wakati huo(baada ya kifo).

Kwa hiyo, binadamu hafi bali mwili ndiyo unaofikia ukomo wa muda wake wa matumizi kwa sababu mbalimbali. Anapokufa John au Hamisi, haina tofauti. Anapokufa mkulima hohehahe au tajiri kuliko wote duniani, pia haina tofauti. Wote wanapita kwenye hatua muhimu ya mabadiliko, ambapo wanaacha matumizi ya kifaa kilicho kuwa ndicho pekee kinachoweza kuwabainisha na wengine hapa duniani na kuchukua kingine ambacho hakiwezi kuwabainisha tena na wale wenye miili bado.

Anapokufa John au Hamisi, haijalishi kama amezikwa kwa dini jeneza la dhahabu na mizinga 100 au kwa masululu butu na kaniki. Kuzikwa ni utaratibu wa kimazoea wa kuhifadhi mwili ambao sasa ni mzoga tu,ili usisumbue watu wengine kwa harufu na maradhi. Kuzikwa haina maana kwamba, kunambadili aliyekuwa akitumia mwili huo(marehemu), la hasha.

Kama unadhani kwamba Mungu anahesabu umezikwa na dini gani, umezikwa na shehe au padri gani, ndiyo afanye uamuzi wa kukupokea mbinguni hapana, ujue unahitaji msaada wa haraka, kama siyo kupelekwa milembe.Ujue hujui chochote ingawa umekuwa ukijidanganya kwamba unajua. Mungu wa kweli hahangaiki na mzoga, bali sisi kwa ufinyu wetu ndiyo tunaodhani kwamba, mizoga au(maiti) hii ina maana.

Mungu Hayatazami mambo kama Abdallah Juma au John Maiko; Kwani kuzika hasa ni kitu gani. Hatuziki watu ili waende mbinguni. Kama ni hivyo, wanaoliwa na wanyama, kuungua na kuteketea kabisa, wao mbinguni hawatafika? Kama hawafika, watahukumiwa vipi siku ya mwisho? Mwili hautakiwi mbinguni, hauna kazi huko, kwani huko siyo makazi ya miili.

Mwili unafaa tu duniani. Kuna zile jamii ambapo mtu akifa mwili wake huchomwa moto na kuteketezwa kabisa unadhani hizi jamii hazimjui Mungu kama wewe unavyomjua? Zinamjua, tena vizuri zaidi yako. Lakini zimeng’amua kwamba, mwili ni kasha tu, likishindwa kufanya kazi, ni sawa na taka nyingine, hutupwa dampo na kuteketezwa kwa moto.

Mtu akishauacha mwili wake(kufa)hana tena uhusiano na mwili huo. Mtu huyo anakuwa ameingia kwenye awamu nyingine ya maisha ambayo haihitaji mwili na ambayo haihitaji kujua huo mwili.

Naona kwa leo niishie hapa nisije nikawachosha, kwani mada hii ni ndefu kidogo.
Bado nakaribisha maoni na maswali kwa wasomaji.

1 comment:
Andika Maoni Maoni
  1. asante kwa makala nzuri sisi ninini? lakini nina swali moja kwako. wakristo wanasema kwamba Yesu kristo alipaa mbinguni akiwa na mwili, je we unasemaje? kwa sababu umetuonyesha ni kwa kiasi gani mwili hutegemea vitu vya mavumbini au ardhini yaani mimea nafaka na maji.

    je tule nyama? mbona inaonekana sisi hatupaswi kula wanyama wenzetu?

    ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi