Mnaweza kufikia umri huu bila mtoto na ndoa ikaendelea kuwa ya upendo.......
Inaelezwa kwamba wanawake huwa wanavurugikiwa sana kiakili pale wanapogundua kwamba hawana kizazi au hawawezi kupata watoto.
Kuna ukweli kwamba mwanaume kama mwanamke huwa anasikitishwa na kukosa mtoto katika ndoa lakini kwa bahati mbaya tafiti mbalimbali zinaonyesha kwamba mwanamke huathirika zaidi kwa kujaribu kwake kuikataa hali hiyo. Wanawake huchukulia suala la kukosa mtoto au watoto kama ndio mwisho wa maisha yao.
Sio kwamba wanaume hawaumii kwa tukio kama hilo, la hasha huumia sana, lakini kinachotokea ni kwamba wao hulichukulia kwa uzito wa kawaida na hii husaidia kupandisha kiwango cha uwezekano kwao kupata ufumbuzi au suluhu ya tatizo hilo.
Wanawake mara nyingi wamekuwa wakihesabiwa kama ndio chanzo cha matatizo ya ndoa zisizo na watoto na kwa bahati mbaya wanawake wameonekana kwa kiasi kikubwa kuamini lawama hizo. Jambo hili huenda ndilo ambalo linawafanya wanawake kukosa raha kabisa pale wanapokuwa hawana watoto ukilinganisha na wanaume. Wanawake huogopa kwamba kwa kukosekana watoto ndani ya ndoa waume zao wanaweza kuchukua uamuzi wa kuoa wake wengine na kuwaacha wao au wao kuwa wake wakubwa wasio na thamani.
Hii ni njia ambayo imekuwa ikitumika sana katika mila karibu zote za Kiafrika. Lakini jambo kama hili halipaswi kuogopwa sana na mwanamke kwa sababu mume anayeamua kwenda kuoa mke mwingine kwa sababu mkewe wa awali hakubahatika kupata mtoto, huyo ni mwanaume asiye na upendo. Kwa nini basi mwanamke asione hiyo ni nafuu kwake ya kuachana na mtu ambaye alikuwa akiishi naye bila upendo.
Kwanza siku za nyuma wakati wa ujima mwanamke angeweza kulalamika sana kukosa mtoto, kwani mtoto alikuwa ni rasilimali. Lakini siku hizi mtoto ni sehemu ya ukamilisho wa jukumu la kimaumbile la mtu kulea kama alivyolelewa. Kama mwanamke anajikuta hana mtoto anaweza kwenda kuchukuwa mtoto kwenye nyumba za watoto yatima au kuomba ustawi wa jamii ili apewe mtoto aliyetupwa au kutelekezwa na wazazi. Huyu naye ni mtoto sawa au kumzidi yule wa kumzaa kama atapata malezi mema.
Imefika wakati ambapo inabidi wanawake wajue kwamba kukosa mtoto au watoto siyo mwisho wa dunia na wala haiwapunguzii hata chembe ya utu wao.
No comments:
Andika Maoni Maoni