0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

http://www.serenahotels.com/serenadaressalaam/default-en.html

Jul 7, 2013

ALINIPIGA KIDOGO TU, TENA MARA MBILI KWA MWEZI, KUNA WANAOPIGWA KILA SIKU...!


Tunajua wote kwamba, hutokea wanawake wakateswa sana kwenye uhusiano wao wa kindoa au kimapenzi na bado wakaendelea kukaa tu kwenye uhusiano huo. Inafikia hadi mtu anakufa huku akiona kabisa. Watu wengine huiita hali hii kuwa ni ujinga na wengine huita kulogwa au huelezea hali hii kwa njia ambayo haiwapi haki wanawake hao. Zipo sababu nyingi ambazo zinawafanya wanawake kuendelea kukaa kwenye ndoa ngumu, bila hata kufikiria kuondoka. Sababu nyingine zinaweza kuonekana kama kituko, lakini ndizo zinazowafanya wafie kwenye ndoa.

Kuna ile sababu kwamba, hawajui ukubwa wa kiwango cha mateso. Hii hutokana na kwamba, baada ya kuzoea mateso, mwanamke hufikia kuamini kwamba, hayo siyo mateso, bali ndivyo ndoa inavyotakiwa iwe. Kuna sababu ya kukosa marafiki, ndugu au jamaa wa karibu. Na kwa sababu hana watu wa aina hiyo, inakuwa vigumu kwake kuwa na mahali pa kukimbilia ili aweze kupata nafasi ya kujiandaa kuanza upya maisha. 


Kuna wanaoendelea kukaa kwa sababu dini zao zinawaambia, hawana budi kukaa, kwani wameshakuwa mwili mmoja na waume zao na hivyo hawawezi kuondoka. Wanafikiria iwapo wataamua kutoroka, viongozi wao wa dini watawaona vipi na waumini wenzao watachukuliaje jambo hilo. Kwa hiyo, wanaishi kwenye ndoa hizo kwa sababu ya dini, siyo kwa sababu yao binafsi. Halafu kuna suala la kupenda. Utegemezi wa kihisia huwa unaitwa kupenda. Kwa hiyo mwanamke anasema anampenda fulani kiasi kwamba, hawezi kumwacha, wakati ukweli ni kwamba, anamtegemea mwanaume huyo kihisia.Wanawake wanaoteswa kwenye ndoa, huwa wanajidanganya kwamba, watamudu siku moja kubadili tabia hiyo a waume zao kuwafuja. Wanajiambia kwamba, kutukanwa, kupigwa, kudhalilishwa, na matendo mengine, siyo hiari ya hao waume wao. 


Hivyo wanaamini kwamba, kuna siku watamudu kuwasaidia watoke kwenye tabia hizo. Lakini wakati mwingine wanaume hawa watesaji, huwa wanajidai kusema kwamba, wanafanya mambo hayo bila kujua sababu na kuna wakati wanasema wamelogwa.Hujawahi kuwaona wanawake wanaokwenda kwa waganga kutafuta dawa ili waume zao wasiwapige, ati kwa sababu vipigo vyao vinatokana na kuchananywa na uchawi wanaofanyiwa na wanawake zao wa nje? Mwanamke anaamini kabisa kwamba, mumewe hamjali na anamdhalilisha kwa sababu ya kulogwa!Mwanamke anaweza kujiambia kwamba, kwa sababu mume wake kuna wakati anamtendea wema, hata kama ni moja, basi anampenda na hayo mengine mabaya, yatakwisha au ni bahati mbaya. 


Mwanamke pia anaweza kufikiri kwamba, akijitahidi sana kumfurahisha mumewe, mume huyo atabadilka na kuwa na tabia nzuri. Hivyo hujipendekeza na mwanaume habadiliki na mateso yanaongezeka. Kuna wanaomudu kuishi kwenye uhusiano huu wa sababu, wamemudu kukandamiza, kupunguza ukubwa wa maumivu. Wanajiambia kwamba, wanavyotendewa siyo vibaya sana. Mwanamke anaweza kujiambia, ‘alinipiga kidogo tu, tena mara mbili kwa mwezi, kuna wanaopigwa kila siku.’ Huyu amehalalisha kipigo na mateso, hawezi kuondoka.


Kuna wanawake wanaoamini kwamba, ndoa inajengwa na kuimarishwa na mwanamke au kuvunjwa na mwanamke pia. Kuna andiko moja katika Biblia hutumiwa sana kuwatisha, linalosema, ‘Mwanamke m.p.u.m.b.a.v.u huivunja ndoa yake kwa mikono yake mwenyewe.’ Kwa hiyo wanapofikiria kuondoka, hufikiria kwamba, watu watajua na kumzonga au kumdharau kwa sababu ameshindwa kulinda ndoa. Wengine ni woga tu, kwamba, wakiondoka waume zao watawalipizia visasi au watawasumbua. kuna wakati waume wenyewe ndiyo wanaokuwa wamewatisha kwa kiwango hicho.

No comments:
Andika Maoni Maoni

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi