0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Jul 6, 2013

MIAKA MITATU YA NDOA, KIPIMO CHA NDOA KUENDELEA AU KUVUNJIKA...!Kuna msemo katika Kiswahili kwamba, kipya ni kinyemi. Msemo huu una maana kwamba, kitu kikiwa kipya huvutia sana na wakati mwingine inakuwa kama vile tunaamini kwamba, hatutaweza kamwe kupunguza hisia zetu dhidi ya kitu hicho. Lakini kadiri siku zinavyoenda, mazoea hutufikisha mahali ambapo hatuwezi tena kuendelea na kiwango kilekile cha kupenda.

Tunapooana, kwa sehemu kubwa ni kwa sababu tunapendana, yaani tumevutana. Katika hatua za awali, tunatokea kuoneshana upendo wa dhati sana. Mara nyingi hi inatokana na haja yetu kuwaonesha wenzetu kwamba, sisi ni watu wa upendo, sisi ni waadilifu na wema. Tunachotafuta ni kukubaliwa nao kwa sababu, wakati huo hamu yetu kwao ni kubwa.Kadiri tunavyokaa pamoja, ile hamu yetu kwao inapungua. Ni vigumu kukuta watu ambao wanaweza kudai kwamba, wameishi kwa muda mrefu na hamu ya kila mmoja kwa mwenzake iko palepale au imeongezeka. Kuna tofauti tu ya viwango vya kushuka kwa hamu, lakini huwa inashuka.


Lakini huku kushuka kwa hisia hakuna maana ya kushuka kwa upendo, hapana. Kushuka kwa hisia kuna maana ya akili na baadaye hisia, kujenga mazoea kiasi cha kumchukulia mwingine kwamba ni wa kawaida, pamoja na kumpenda kuliopo.


Kuna wakati wapenzi hulalamika kwamba, mwenzake alikuwa akipenda kukaa naye kwa muda mrefu, siku hizi hakai kwa muda mrefu tena. Kuna kulalamika kwingi hususan kwa wanawake kwamba, mwenzake haonyeshi ukaribu kama zamani na mengine ya aina hiyo, ingawa bado anaweza kukiri kwamba, anajua anapendwa na huyo mwenzake.


Wataalamu wanadai kwamba, ndoa inapofikia miaka mitatu, mara nyingi ndipo ambapo kama ni kuachana watu huachana au kama ni vurugu, zinakuwa zimefikia mahali pazuri hasa! Katika kipindi cha ile miaka mitatu ya kwanza, ndipo ambapo watu wamefahamiana vema na kama ndoa yao itakuwa ni ndoa ya vurugu, kufikia muda huo inakuwa imeshafahamika.
Ndoa nyingi za vurugu zinakuwa zimefahamika kwamba, ni za vurugu kwa kiwango gani kufikia miaka mitatu. Inaelezwa kwamba, katika mwaka wa tatu, mtu anaweza kabisa kutabiri kama ndoa itakuwa ya amani au vita na kama ni ya vita ni kwa kiasi gani. Kama ni ya vurugu kubwa, hata hivyo, mara nyingi haivuki miaka mitatu.

Kama ndoa imeweza kuvuka miaka mitatu, kwa kawaida kipimo kingine ni miaka mitano. Kwenye mwaka wa tano wa ndoa kuna kuachana na kuapizana kwingi pia. Ukichunguza kwa makini, utagundua kwamba wanandoa wengi hufurahishana na kuachana au kuapizana zaidi mwaka wa tatu na wa tano, tangu ndoa yao.


Hapa kwenye mwaka wa tano, ndipo ambapo wanandoa hujiuliza kama walifanya uamuzi sahihi, ndipo ambapo hutaka kujua kama waendelee na ndoa ngumu kama hiyo au hapana hujihoji kuhusu udhaifu wao (wale wenye hekima). Hapa unaweza kukuta mtu anabadilika tu na kuwa ama mkorofi sana au mwadilifu sana kwa ndoa yake.
Inaelezwa kwamba, baada ya hapo, yaani ukiona watu wamevuka mwaka wa tano salama, kimbuka kinaweza kutokea kwenye mwaka wa tisa. Kwenye mwaka wa saba yale ambayo yalikuwa ni siri ya wanandoa yanaweza kusemwa nje. Inawezekana mume alikuwa ni mzinzi mke akawa anaficha, mke hajui kutunza familia, mume akaficha, yote hayo yanaweza kusemwa hadharani au kwa watu wengine inapofikia mwaka wa tisa.

Kama wanandoa wakivuka salama au wakivuka pamoja na misukosuko yao kwenye mwaka wa tisa, hatua ya mwisho ni mwaka wa 13 wa ndoa. Hapa ndipo ambapo wanandoa wengi wanaamua kwamba, ngoja maisha yaende kama yalivyo au tufikie ukomo. Hebu jaribu kuvuta kumbukumbu na uone kama hakuna wanandoa wengi ambao unawajua, waliovunja ndoa zao kwenye mwaka wa 13! Kama sio mwaka wa 13 palepale inaweza kuwa mwaka wa 12 au wa 14 wa ndoa yao. Lakini kipimo mara nyingi ni mwaka wa 13.Ukiona ndoa imevuka hapo, watu wakiwa pamoja hata kama kuna vurugu za namna gani za kindoa, huenda wataishi hivyohivyo hadi kifo kiwatengenishe au mmoja amdhuru mwingine…….

No comments:
Andika Maoni Maoni

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi