0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

http://www.serenahotels.com/serenadaressalaam/default-en.html

Dec 26, 2009

ALIAMBIWA 'UTAKUFA' AKAFA KWELI

Veronica Guerin

KESI ILIYOZUA UTATA:

Ilikuwa ni tarehe Juni 26, 1996 Veronica Guerin alikuwa ndani ya gari lake aina ya Opel nyekundu akikatiza mitaa ya nje ya jiji la Dublin nchini Ireland, wakati akirejea nyumbani kwake baada ya pilikapilika za mchana kutwa akitafuta habari.

Huyu ni mwandishi wa habari za kiuchunguzi nchini Ireland ambaye alikuwa ni mwiba mchungu kwa wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya na wahalifu walishindikana.

Alipofika kwenye taa za kuongozea magari, Veronica alisimama, kisha akanyanyua simu yake ya mkononi na kumpigia rafiki yake mmoja ambaye ni Polisi. Hakupata majibu zaidi ya kujibiwa na sauti iliyorekodiwa kwenye simu ya mhusika ikimwelekeza aache ujumbe.

Wakati anaanza kuongea ili kuacha ujumbe kwenye simu ya rafikiye, hakujua kwamba kulikuwa na pikipiki iliyokuwa na watu wawili ikimfuata kwa nyuma ambayo ilisimama mita chache kutoka pale aliposimama.

Mtu yule akiwa amevaa kofia ya kuendeshea pikipiki alishuka kwenye pikipiki yake na kulisogelea gari la Veronica kisha akafyatua risasi tano kupitia dirisha la dereva ambapo zilimuua Veronica sawia.

Ni muda mfupi Veronica alikuwa hai akiongea na kucheka kwenye simu na muda huohuo anauawa kwa kupigwa risasi.

Ni tuklio ambalo lilichukua sekunde chache sana. Mwendesha pikipiki yule alitoweka na pikipiki yake, akitokomea kwenye viunga vya Dublin baada ya kufanya mauaji yale.

Kuuawa kwa Veronica kuliishtua jamii ya wa Irish ambayo pamoja na kushuhudia mauaji mbalimbali yanayoendeshwa na kundi la IRA, lakini mauaji ya watu ambao hawahusiki na masuala ya kisiasa yalikuwa ni adimu sana kutokea.

Ni jambo lisilokuwa na ubishi kabisa kwamba mauaji yale yalikuwa ni ya kupangwa na kufadhiliwa na wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevywa na wahalifu wakubwa ambao Veronica alikuwa akiwachunguza na kuandika habari zao.

Waziri mkuu wa wakati huo wa Ireland John Bruton aliahirisha kikao cha Bunge la nchi hiyo kwa ajili ya kuungana na familia ya Veronica Guerin katika msiba huo. Waziri mkuu huyo alisema katika taarifa yake, 'mtu fulani, mahali fulani anaamua kutoa roho ya mama huyu kwa sababu ya kuzuia habari za kihalifu zisitolewe hadharani, huu ni unyama.’

Salaam za rambirambi ziliendelea kutolewa kutoka kila mahali, Aengus Fanning mhariri wa gazeti la Sunday Independent gazeti ambalo Veronica Guerin alikuwa akiliandikia, katika taarifa yake alisema, ‘Veronica Guerin alikuwa ni mwandishi mahiri na jasiri ambaye sijapata kukutana na mwandishi wa aina yake katika maisha yangu.’

Mhariri huyo ambaye ndiye aliyekuwa bosi wa Veronica alitangaza hadharani kwamba gazeti la Sunday Independent litatoa zawadi ya kitita cha dola 150,000 kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa zitakazopelekea kukamatwa kwa muuaji.

Mazishi ya Veronica Guerin yalifanyika June 29, 1996, katika kanisa la Our Lady Queen of Heaven, ikiwa ni siku tatu baada ya kuuawa. Mazishi hayo yaliongozwa na baba askofu wa Dublin yalihudhuriwa na waombolezaji wapatao 1,000wakiwamo Rais wa Ireland, waziri mkuu pamoja na baadhi ya mawaziri na watu mashuhuri.

Siku mbili baadae nchi ya Ireland ilifanya kumbukumbu kwa wananchi wote nchi nzima kusimama kwa dakika moja, na Rais wa nchi hiyo alimtangaza Veronica Guerin, kuwa shujaa wa nchi hiyo.

Ili kujua sababu za Veronica kuuawa, na pia kujua muuaji aliyehusika na mauaji hayo, Polisi walianza kuchunguza taarifa alizokuwa akiziandika pamoja na wahusika, aliowahi kuwaandika. Veronica Guerin alianza kazi ya uandishi wa habari mnamo mwaka 1990 akiwa na umri wa miaka 30, na mama wa mtoto mmoja wa kiume aitwae Cathal aliyemzaa na mumewe aitwae Graha Turley.

Mnamo mwaka 1993 alipata bahati ambayo mwandishi yeyote angeota kuipata.

Katika kipindi hicho kuliibuka kashfa ambayo ilimhusu padri wa kikatoliki wa kanisa la Galway aitwae Eamonn Casey, ilipokuja kugundulika kwamba alikuwa na mtoto wa kiume wa umri wa ubarubaru aliyemzaa nchini Marekani.

Baada ya kashfa hiyo kuibuka, padri huyo alijiuzulu na kutoweka kusikojulikana, Veronica Guerin alichunguza na kugundua kwamba padri Eamonn Casey alikimbilia Amerika ya Kusini ambapo alimfuata na kufanya naye mahojiano yaliyokuja kutangazwa karibu dunia nzima yakiripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari .

Mahojiano hayo yalimfanya Veronica kuwa maarufu kwa muda mfupi mno. Miezi michache baadae Veronica alianza kuwindwa na vyombo vikubwa vya habari, kila chombo kikimhitaji kwa ajili ya kukiandikia habari.

Katika harakati hizo za kugombewa ni gazeti la Sunday Independent pekee ndilo lililofanikiwa kumnyakua mwanamama huyo.

Mtu wa kwanza kuanza kufuatiliwa na Veronica alikuwa ni Martin Cahill, ambaye alikuwa akijulikana kwa jina la utani kama Te General. Huyu alikuwa ni mtu hatari aliyekuwa akiogopwa sana katika jiji la Dublin kutokana na kufadhili magenge ya kihalifu.

Pia alikuwa ni mtu katili ambaye aliwahi kumpigilia misumari sakafuni askari kanzu mmoja aliyekuwa akimfuatilia na katika tukio lingine aliwahi kumchuna ngozi akiwa hai kibaraka mmoja wa polisi.

Veronica alimfuatilia The General kwa muda wa mwezi mmoja, hadi akakubali kufanya naye mahojiano, lakini kwa masharti kwamba, asirekodiwe kwenye kifaa cha kurekodi mahojiano, yaani kinasa sauti.

Katika mahojiano hayo The General alikanusha katukatu kushirikiana na magenge ya kihalifu. Miezi michache baada ya mahojiano yale, , mnamo mwezi agosti, 1994 The General aliuawa na muuaji wa IRA na sababu ya kuuawa ilitokana na kushirikiana kwake na wapiganaji wa kiprotestant walioko magharibi mwa Ireland. IRA ni kikundi cha kupigania uhuru wa Ireland kutoka uingereza.

Veronica aliliandika tukio la kuuawa kwa The General kama mpango maalum ulioandaliwa na IRA ili kuwazuia mabwana wakubwa hao kuhojiwa na vyombo vya habari, ingawa hakumtaja muuaji katika makala yake.

Wiki chache baada ya habari ile kutoka gazetini, Veronica alivamiwa na mtu mmoja mwenye silaha ambaye alifyatua risasi kupitia dirishani katika chumba cha kupumzikia, muda mfupi baada ya Veronica na mwanae aliyekuwa na umri wa miaka minne kuondoka pale sebuleni.

Tukio lile lilimtisha sana Veronica lakini alisema halitosababisha yeye kurudi nyuma.

Mtu wa pili kufuatiliwa na Veronica alikuwa rafiki wa karibu wa The General, ambaye si mwingine bali alikuwa ni John Traynor ambaye pia alijulikana kwa jina la The Coach.

Traynor alikuwa ni tapeli la kutupwa ambaye hata polisi waliamini kwamba ndiye aliyehusika na shambulio lililofanywa nyumbani kwa Veronica.

Pamoja na kujua kwamba Traynor ni mtu wa kuogopwa, lakini Veronica alimfuatilia na kufanya naye mahojiano mara mbili mwaka 1994.

Mnamo Januari 1995 Veronica aliandika makala iliyomwelezea Traynor kama mhalifu wa kuogopwa na ambaye amewahi kufadhili na kushiriki katika matukio ya kihalifu siku za nyuma.

Polisi hawakutilia maanani makala ile na walipuuza nakusema haina ushahidi wa kina wa kumhusisha Traynor na uhalifu uliotokea siku za nyuma…….

Wiki moja baada ya makala ile kutoka katika gazeti la Sunday Independent, Veronica alivamiwa na nyumbani kwake akiwa peke yake na mtu aliyeficha uso wake ili asitambulike.

Mtu yule alimshurutisha Veronica apige magoti chini na alimuelekeza bastola kisogoni na kuashiria kuifyatua lakini alisita na kumpiga Veronica risasi ya mguuni halafu akatoweka.

Veronica alifanikiwa kujiburuza na kuifikia simu na kuwapigia polisi kuwajulisha kuhusu uvamizi ule, Polisi walifika na kumkimbiza hospitalini. Veronica alitoka mwenyewe hospitalini bila kuruhusiwa na daktari, kwa kuwa alikuwa hajapona vizuri kiasi cha kushindwa kuendesha gari, mumewe Graham Turley alimchukua na kupita naye kwenye maeneo ya wahalifu aliowatuhumu kuhusika na tukio la kuvamia nyumbani kwake ili kuwaonesha kwamba ameponan na atarejea kazini kwake kama kawaida.

Ndani ya wiki moja tangu alipopigwa risasi, Veronica alirejea kwenye dawati lake la habari na kwenye toleo la gazeti la wiki iliyofuata aliandika kuhusu mkasa alioupata lakini aliwaonya maadui zake kwamba wasidhani ataacha kuandika habari zao.

Kwa maneno yake mwenyewe aliandika, 'nilisema na ninarudia tena, sidhani kama ninayo dhamira ya kuacha kuandika uozo wenu, ingawa bosi wangu amenipa chaguo la kubadilisha mwelekeo wa habari zangu, sitarajii kabisa kuacha na sitarajii kuanza kuandika habari za matamasha ya ulimbwende au kuandika habari za namna ya kutengeneza na kutunza bustani za maua.'
ITAENDELEA..............

2 comments:
Andika Maoni Maoni
  1. Naisubiri kwa hamu sehemu itakayofuata. Simulizi yenye kusisimua.

    ReplyDelete
  2. Huyu mwana mama alikuwa jasiri na alijitolea maisha yake kwa ajili ya kuitumikia jamii na kuwaumbua wahalifu, alikuwa jasiri na mwenye nia dhabiti MUNGU ailaze mahali pema peponi roho ya marehemu

    Nasubiri mwenddelezo wa makala haya.............

    ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi