Mwaka 1976 nilianza masomo ya darasa la nne kwenye shule ya msingi Turiani. Kutoka shuleni hadi tulipokuwa tunaishi kwenye kambi za watumishi wa kiwanda cha sukari ni mbali sana, kiasi cha kilomita nane. Nilikuwa natoka asubuhi sana nyumbani nikiwa sijanywa chai na kurejea jioni.
Mwezi wa kwanza tangu kuanza masomo hali ilikuwa mbaya ingawa siyo sana. Kuna wakati nilikuwa ninalala na njaa, hasa zile siku ambazo shemeji yangu alikuwa akiingia usiku. Shemeji yangu alikuwa ni dereva wa magari ya kusomba miwa kutoka mashambani kwenda kiwandani. Kulikuwa na shifti mbili za kazi, usiku na mchana.
Shemeji yangu alikuwa ndiye mlinzi wangu kutoka katika shutuma, kashfa na mateso kutoka kwa dada yangu, ambaye marehemu mama alikuwa akimsema kwa uzuri siku zote. Kwa maana hiyo ni kwamba, nilikuwa nimeweza kwenda shule kwa sababu, shemeji yangu alikuwa upande wangu, niliweza kula na kulala kwa sababu ya shemeji yangu.
Huyu dada alikuwa na watoto wanne, mmoja wa kiume na watatu wa kike. Watoto watatu walikuwa walikuwa wannichukia na kunitendea kama kwamba nilikuwa nimeokotwa na kuletwa pale nyumbani kwao. Mmoja wa kike ambaye alikuwa darasa la pili, ndiye aliyekuwa ananijali na kunihurumia. Kama kweli watoto huchukuwa roho za wazazi wao kama watu wanavyosema, huyu alichukua roho ya baba yake.
Mwezi wa pili tangu kuanza shule, shemeji yangu alipatwa na malaria na kulazwa kwenye hospitali ya misheni inayoitwa Bwagala. Kwa wiki moja aliyolazwa, nilijua hasa maana ya roho mbaya. Ile siku alipolazwa sikula chakula na asubuhi yake nilikuta nguo zangu za shule zimeloweshwa na kutupwa nje. Dada yangu alinipiga sana, akidai kwamba mimi ni mchawi na ninaharibu bure pesa za mume wake, kwani sikuwa na uwezo wa kusoma.
Kama sio jirani mmoja ambaye namkumbuka kwa jina hadi sasa, Richard, kuingilia kipigo kile, naamini ningevunjwa mbavu au eneo fulani la mwili lingedhurika. Watoto wa dada mabo ni wapwa zangu walikuwa wakishangilia wakati napigwa na shule hawakwenda siku hiyo. Niliondoka hapo nyumbani baada ya kipigo hicho hadi hospitalini Bwagala. Nilikuwa mtu wa kwanza kuingia wodi ya wagonjwa siku ile.
Shemeji yangu aliponiona alijua kuna jambo. Sikutaka kumsimulia, lakini aliniomba nimwambie kumetokea kitu gani. Nilimsimulia. Alinitazama kwa muda mrefu sana kabla hajaniuliza, ‘lakini masomo unayaonaje?’ nilimwambia, ninaamini akiendelea kuwepo nitafaulu darasa la saba na kusoma zaidi. Alitabasamu na kuniambia ‘nitakuwepo na utafika mbali, mungu hawezi kukunyang’anya kila kitu.’
Nilimwona akigeukia upande wa pili wa kitanda chake na nina uhakika alilia. Aligeuka tena kunitazama kama baada ya dakika kumi. Aliingiza mkono wake mfukoni kwenye lile pajama la hospitalini alilokuwa amevaa na kutoa kitu. Alinyoosha mkono na kunipa. Zilikuwa ni hela. Sikumbuki zilikuwa ni kiasi gani, ingawa kwa kiwango cha sasa ninaweza kusema zilikuwa ni shilingi 2,000.
Nilisita kuzipokea, lakini macho yake yalinilazimisha kuzipokea. ‘Kafue hizo nguo zako, kesho uende shule. Kumbuka ukitoka shuleni pita pale midizini ule kabisa mghahawani, kabla hujaenda nyumbani. Usimwambie una hela au umekula.’ Aliniambia. Nilimtazama yule mtu pale kitandani na kuanza kulia. Nilishindawa hata kumwambia ‘asante,’ Nilikutana na dada yangu mlangoni wakati naondoka pale wodini. ‘Nyooo, mwanaharamu …..’ Nilimsikia akisema.
Kwa shida shida hivyohivyo nilimaliza darasa la nne na kuingia darasa la tano. Muhula wa kwanza na wa pili wa darasa la nne nilikuwa mtu wa kwanza darasani. Hii ilisaidia na kuniumiza pia. Nilianza kupata marafiki wa nje na nyumbani ambao walikuwa wakinisaidia nilipokuwa na shida kwa sababu walikuwa wakihitaji msaada wangu kimasomo. Lakini kwa nyumbani hali hiyo iliongeza chuki kutoka kwa dada na wapwa zangu. Ni kale kadogo tu, kalikokuwa kanaitwa Msekwa ndiko kalikokuwa kanafurahiya mafanikio yangu.
Shemeji aliamua kuwa na utaratibu wa kunipa senti kumi kila siku kwa ajili ya kula shuleni na ikawa ni siri yangu. Kuna wakati alikuwa akifika shuleni kuulizia maendeleo yangu, nadhani kwa makusudi ili waalimu wajue kwamba alikuwa na mtoto mwenye akili sana. Hii ilitokana na ukweli kwamba, hakuwa anaulizia matokeo ya watoto wake, ambao walikuwa wakishika namba za mwisho mwisho. Lakini bila shaka alikuw akitaka kunipa moyo, kunionesha kwamba kuna mtu anayenijali. Hii ilinipa nguvu sana na nilimchukulia kama baba yangu kabisa. Nilianza kuona uzito wa kumwita shemeji.
Lakini upande wa ndoa yake kulikuwa na tatizo. Kila siku kulikuwa na zogo kati ya shemeji na mkewe , yaani dada yangu. Jambo ambalo nilijifunza kwa shemeji ni subira na uvumilivu. Hakuwa akipenda sana kelele na kila zogo lilipoanza alikuwa akijibu kidogo na akiona dada haelewi alikuwa akijiondokea zake kunyoosha miguu kama alivyokuwa akiita mwenyewe. Kwa mara ya kwanza nilianza kuonja upendo wa mzazi wa kiume na kuonjeshwa roho mabaya inavyokuwa kwa mwanamke. Nilimshukuru mungu.
Lakini hali hiyo haikudumu. Nikiwa darasa la sita, jambo ambalo halikutegemewa na mtu lilitokea. Shemeji yangu alipata ajali ya gari wakati akitoka kusomba miwa. Gari lake lilimgonga mwendesha baiskeli na kumjeruhi sana. Kutokana na kosa hilo, alisimamishwa kazi, na baadae alifukuzwa. Kwa hiyo alitakiwa kuhama kwenye nyumba ile ya kampuni. Ilikuwa bahati kwamba wakati akiwa kazini alikuwa amejenga nyumba ya vyumba viwili iliyoezekwa kwa makuti kijijini Manyinga, umbali wa kilomita mbili kutoka kiwandani.
Ilibidi tuhamie hapo Manyinga. Alijitahidi kutafuta kazi kila mahali, lakini ilishindikana. Dada yangu alimwongezea machungu kwa kumsimanga. Nakumbuka siku moja walikuw2a wakigombana huko chumbani kwao usiku. Nilimsikia dada akimwambia shemeji kwamba, asipoangalia ataolewa. Alimwambia maneno hayo kwa kizigua.
Baada ya kauli hiyo sikusikia tena sauti ya shemeji na mimi binafsi niliumia kuliko hata yeye bila shaka. Asubuhi kabla sijaenda shuleni, shemeji aliniita na kuzungumza nami. ‘Nasafiri leo, usimwambie mtu. Nataka kwenda Moshio kwa kaka yangu, nikajaribu kama nitafanikiwa kupata kazi. Nina kaka yangu yuko kule TPC, nadhani atanisaidia.’ Halafu aliendelea. ‘Jitahidi, nikiwa kule nitajitahidi kuhakikisha kwamba unasoma hadi ufike Makerere.’ Alisema na kutabasamu. ‘Una akili sana na mungu amekupangia jambo kubwa maishani. Vumilia shida, kwa sababu zitakufundisha kuishi na kukabiliana na lolote baya maishani.’ Halafu akatoa shilingi 120 kutoka mfukoni na kunipa.
Niliondoka kwenda shule na inasikitisha kusema kwamba huo ulikuwa mwisho wa kuonana na shemji yangu nikiwa mtoto. Alipoondoka yale mateso yalianza na bila shaka yalikuwa makubwa kuliko mtu anavyoweza kufikiria. Ni mengi kiasi kwamba siwezi kuyaeleza yote. Lakini nayakumbuka yale makubwa ambayo pia ni mengi sana kiasi kwamba nikianza kuyasimulia nitakuchosha wewe msomaji. Lakini kubwa kuliko yote lilikuwa ni lile la kuunguzwa na kwa mafuta ya kula shavuni. Nasema kuwa hili ndilo kubwa zaidi kwa sababu ndilo lililobadili kabisa maisha yangu.
Hili lilitokea wakati niliwa darasa la saba, ikiwa ni miezi minne tu kabla ya kufanya mtihani wa mwisho.Nilikuwa na uhakika kwamba ningeweza kufaulu iwe au isiwe. Sikuw nauwezo wa kubahatisha kwa kweli. Nilikuwa ninayaelewa maisha. Nakumbuka baada ya shemeji kutoroka, dada yangu hakuwa na njia isipokuwa kuanza biashara ya maandazi na vitumbua. Mimi ndiye niliyekuwa naandaaa unga wa vitumbua na kukanda ule wa maandazi na pia kuchoma vitumbua na maandazi. Pamoja na kufanya kazi hizo kila siku sikuwa ninaruhusiwa kuonja hata kipande cha andazi wala kitumbua. Nilikuwa ninaondoka nyumbani asubuhi bila kunywa chai.
Siku ya tukio nilikuwa ndio namalizia kuchoma maandazi kwenye saa 12.30asubuhiili nijiandae kwenda shule. Mama alikuja na kukagua kazi. Aliona andazi moja likiwa limeungua. Alilichukuwa na kuniuliza, ‘Hivi mama yako ndiye ananunua unga huu unaouchezea?’ Nilitaka kujiteta lakini kabla sijafanya hivyo , nilihisi kitu fulani kikiparuza katika shavu langu. Ni mafuta ya moto! Dada alikuwa amechukuwa kijiko mcha mboga kilichokuwa hapo karibu na kuchota mafuta ya moto na kunimwagia. Halafu nilihisi maumivu ambayo ni vigumu kuyaelezea. Nilikurupuka kutoka pale na kutoka nje nikipiga kelele. Huko nje nilishika shavu langu na kutoka na ngozi. Nilikuwa nimeungua sana.
Kama vile kujihami dada yangu alitoka nje na kupiga kelele kwamba nimemwibia fedha zake zote za biashara. Majirani walikuja kuona kulikoni. Namkumbuka Mzee mmoja wa kichaga au kipare ambaye alikuwa na duka hapo kijijini, aliponiona alisema, ‘tumpeleke hospitalini, ameungua sana’ Wazo lake lilikubaliwa haraka na majirani wengine nilikimbizwa Bwagala Hospitalini.
Je wewe unaamini katika ndoto au maono? Mimi naamini kwa sababu nilishuhudia. Lakini kwanza ngoja niendelee na habari yangu hii yenye kufundisha.
Nilipelekwa hospitlini na wale wanakijiji. Dada na wanae hawakujali kabisa. Kale kabinti kake ka mwisho yaani Msekwa, kalilia sana kalipoona nimeunguzwa. Nakumbuka nilipolazwa hospitalini ndiko pekee kutoka nyumba ile kalikokuja kunitazama.
Nililazwa hospitalini kwa wiki mbili na wale wanakijiji walionipeleka hospitalini ndio waliochangishana na kunilipia gharama za kukaa hapo hospitalini. Nilitoka nikiwa na nafuu kubwa, ingawa shavu langu lilikuwa na alama kubwa ya kuunguzwa kule. Hata hivyo nilijua kwamba, hata baada ya kupona ningebaki na kovu hilo mileleNilipotoka hospitalini sikuweza kurejea kule kwa dada yangu na wale wanakijiji walionisaidia pia waliogopa kunipokea. Waliogopa kwa sababu dada yangu alikuwa akiwatisha kwamba nikifa watanila nyama. Ilibidi nifikirie namna mpya ya kuishi. Kumbuka wakati ule, tena vijijini, watu hawakuwa wanjua kitu kinachoitwa haki za binadamu, achilia mbali haki za mtoto. Watu walikuwa waoga kuingilia mambo ya familia za watu, hata kama mtu anakufa.
Unajua ni kwa nini nimekuuliza kuhusu maono? Ni hivi. Saiku ile nilipotoka hospitalini nililazimika kwenda kwenye mashamba yampunga ambapo niliomba kibarua cha kufukuza ndege kwa wenye mashamba hayo. Nakumbuka watoto wengi na watu wazima walikuwa wakifanya kibarua hicho. Kwa bahati nzuri mama mmoja aliniambia angenisaidia lakini malipo yangu ningepata baada ya mavuno. Aliniambia ningekula na kulala kwake hapo hapo shambani. Niliona kama vile nimepata dhahabu. Nilikubaliana naye.
Ilikuwa ni usiku wakati nikiwa bado sijapata usingizi vizuri, nilipokiona kitu hicho. Hapo kwenye kibanda cha shambani nilimokuwa, niliona kitu kama kivuli kidogo. Kivuli hicho kililkuwa mbele yangu. Kwa sababu ya giza sikujua kama ni kivuli cha mtu au hapana.
Niliogopa kupindukia na nilikuwa natetemeka pale kwenye godoro la sufi nilipokuwa nimelala. Halafu nilisikia kama sauti, ambayo sikujua kama inatoka kichwani mwangu au kwenye kile kivuli. Ilikuwa ikisema 'Muone tu mama mkubwa, ni lazima usome, ile sauti ilirudia tena na tena. Ilikuwa ni sauti niliyokuwa ninaifahamu.
Ilizidi kunisisitiza tena na tena. Nilishindwa kuvumilia ambapo nilipiga yowe kubwa na kuamka. Nilipapasa hapo chini na kuchukua kiberiti. Niliwasha kibatari huku mikono yangu ikitetemeka. Nilitazama mle kibandani na sikuona kitu. Nilikumbuka sauti ile kwa mbali sana. Ilikuw ni sauti ya mama yangu au mdogo wangu, sikuwa na uhakika sana.
Nilianza kufikiria kuhusu huyo mama mkubwa. Mimi sikuwa na mama mkubwa, sasa ni mama mkubwa yupi ambaye huenda sauti zile zilikuwa zikinielekeza kwake. Nilijiuliza karibu usiku mzima. Hatimaye kwa njia fulani ya ajabu nilikumbuka kwamba, wakati nikiwa nimelazwa pale hospitalini Bwagala, kulikuwa na watu waliokuwa wakimtaja mtu aliyeitwa mama mkubwa, ambaye wengine walisema ndiye mwenye hospitali ile.
Nilichukuliwa na usingizi kwenye saa kumi na nilishtushwa na mama mwenye shamba. Alikuwa akiniita huku akitukana kwani mpunga ulikuwa unashambuliwa na ndege. Nilitoka kibandani kwa kasi na kukutana naye mlangoni. ‘Samahani mama nimechelewa kuamka…’Hakusubiri nimalize kwani alinitaka niondoke pale shambani kwake saa ile ile. Niliondoka bila kuhitaji kujitetea, labda nilishazoeshwa kuishi kwa amri.
ITAENDELEA....................
DUH stori imenidaka hii !Mkuu uliyopitia ni makubwa!:-(
ReplyDeletePole sana Kaka.
ReplyDeleteUliyopitia kweli ni makubwa na ya kutisha.