0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

http://www.serenahotels.com/serenadaressalaam/default-en.html

Jul 10, 2010

NENO MOJA LATOSHA KUVUNJA NDOA!

Kubishana sawa, lakini tuchunge kauli zetu!

Wote sisi, kama binadamu huwa tunashikwa na hasira kutoka muda fulani hadi mwingine, lakini kushikwa na hasira na kuziacha hasira hizo ziwaumize wale tunaodai kuwa tunawapenda ni jambo tofauti sana.

Tunapojikuta tunashindwa kuzuia kulipukwa na hasira dhidi ya wale tunaowapenda mara kwa mara, inapasa tujue pia kwamba tunaujeruhi uhusiano wetu na baadae tutauuwa kabisa.

Kuna wakati kwa sababu mbalimbali, baadhi yetu huwa tunajikuta tukitaka tu kuwakera wapenzi wetu kwa kuwapandishia kila wakati kwa milipuko ya hasira. Ni kama vile, bila kulipukwa na hasira hizo, maisha yetu yanakuwa yamepoteza maana.

Ni vigumu sana wakati mwingine kwa watu hawa kuacha tabia yao hiyo, lakini juhudi ya kujitoa ni muhimu sana. Ni muhimu sana kwa sababu, uhusiano mwingi umevunjika kutokana na hasira hizi za kila wakati, ambazo wala hazina msingi, bali zinatokana na mtu kujichukia mwenyewe.

Kutokana na hasira hizi, mara nyingi wapenzi hujikuta wakilazimika kubishana badala ya kujadili. Hawa watu wenye hasira hizi za hapa na pale, huwa siyo wasikilizaji, bali ni watu wa kulaumu, kujitetea, na kutaka kusikilizwa wao tu, kwa maana ya kushinda.

Katika uhusiano wa aina hii, hakuna uwezekano wa ustawi, bali uwezekano ni uhusiano kufa. Kwani ni mara chache ambapo huyu mpenzi mwenye hasira za mlipuko atakuwa tayari kusikiliza na kuelewa.

Jambo ambalo wapenzi wanapaswa kulifanya,. Bila kujali kama wana hasira sana au hasira nyingi, ni kujitahidi kuweka nguvu kwenye jambo wanalojadili. Watu wenye hasira za ziada, huwa hawana uwezo wa kuzingatia kile kinachojadiliwa.

Huwa na ugumu huo kwa sababu hasira za ziada huwasukuma kusema chochote ambacho kitawafanya washinde, ikiwemo kusingizia na kusema uongo. Lakini huwa wanabebwa na wimbi la hasira kiasi kwamba hawana muda wa kupima athari ya kile wanachosema.

Kuna haja ya kujua kwamba, neno moja tu la hasira, linatosha kuvunja uhusiano au ndoa. Kwa hiyo, ni muhimu sana kwa mtu mwenye hasira za mlipuko kujifunza kuzingatia jambo ambalo, yeye na mpenzi wake wanalijadili. Anapotoka nje ya mada, ni lazima ataropoka.

Kuna wanandoa wanabishana kuhusu shule ya mtoto kwa mfano, mwanandoa mwingine hana haja ya kusema, ‘unabisha kwa sababu hukusoma, ndilo tatizo la kuoa wanawake wasiosoma.’ Hapa ni kutoka nje ya mada kwa hasira za mlipuko.

Kumbuka pia kwamba, wanandoa au wapenzi ambao wanapobishana hawatoki nje ya kile wanachobishania na pia wanatumia nguvu ya hoja badala ya mihemko, huwa wanaelewana katika mambo mengi sana, huwa wanatatua migogoro mingi kwa amani na kuaminiana zaidi.

Kuna wakati kwa sababu ya hasira za mlipuko, mpenzi anaweza kutafuta kwa makusudi jambo ambalo litamuudhi mpenzi wake. Anaweza kumwambia, ‘sibishani na mwanamke mnene kama nguruwe.’ Au mwanamke akamwambia mpenzi au mumewe, ‘mbele ya wanaume nawe unajiita mwanaume.’

Kila mmoja wetu anajua ni maneno gani akisema yatamkera mwenzake. Nasema kila mpenzi anajua eneo nyeti la mpenzi wake, ambalo akiligusa anakuwa amemuuwa kisaikolojia. Kujua huku eneo hilo hakupaswi kutumiwa vibaya na wapenzi.

Kwenye uhusiano kuna kanuni ya, ‘usimtendee mwenzio yale ambayo hupendi kutendewa.’Wapenzi wanapoweza kila mmoja kufuata kanuni hii, uhusiano huwa mzuri sana.

Kuna wakati mpenzi anaweza kudhani kwamba wakati wa kubishana ndio wakati mzuri kwake ‘kumpasha’ mpenzi wake, ndiyo wakati mzuri wa kumuumiza kihisia. Hili ni kosa la karne kwa sababu wakati huu, ndio ambao mwanandoa au mpenzi anapopaswa kujilinda na kauli zake kuliko waati mwingine.

Maneno ndio silaha kwenye kubishana kumbuka. Kwa hiyo yanatumika vizuri au vibaya ni jambo la msingi sana. Maneno huumiza na kuvunja mifupa kuliko vyuma, anavyoweza kupigwa navyo mtu.

Mtu anapojifunza kubishana bila kutumia maneno ya kuumiza au kutoka nje ya mada inayojadiliwa, hujenga kujiamini, kwani mara nyingie hasira za ziada ni matokeo ya kutojiamini.

Inaonekana kuna aina ya maradhi ya kisaikolojia, ambapo mtu hujikuta hawezi kuishi maisha ya amani na mpenzi.

Akihisi amani ni kubwa, hutafuta njia ya kuiondoa ili ajisikie vizuri. Kwa hiyo, atazua jambo ambalo litazua ubishi ambao utamfanya aropoke.

Bado, hata mtu kama huyu anaweza kujisaidia kwa kuanza kujua kwamba ana udhaifu, kuukubali na kuanza kufanya kazi ili kuukabili.

6 comments:
Andika Maoni Maoni
  1. Mkuu hapo umenena, mambo ya kusubiri mtafaruku ndio umwage donge lako, kwa kweli hugeuka sumu kali badala ya kutatua mzozo

    ReplyDelete
  2. Mkuu hii mada ya leo ni kiboko kabisa. Watu wengi tunapaswa kusoma hapa na kujifunza mambo haya ya msingi sana.

    ReplyDelete
  3. ni mada nzuri sana na ya kufunza Asante kaka.

    ReplyDelete
  4. Hii mada imetulia kweli.
    lakini kaka Shabani pamoja na hilo la kubishana na kukwazana, pia kuna wanaume wana Ghubu kweli, unaweza kukuta mwanaume kila saa kulalamika, mara mbona chakula hakina chumvi, mara mbona watoto hawajaogeshwa, mara mbona nyumba ni chafu, mara mbona hiki au kile hakijafanyika........Mweh! yaani ni lawama mtindo mmoja...na kila kitu kitakosolewa.......

    Je hawa nao hawachangii kuvunjika kwa ndoa au mapenzi kupungua?

    Mie ninaye shoga yangu alikuwa amejifungua kwa operesheni..... lakini nilishangaa hata kabla hajapona mshono vizuri alikuwa anawajibika kufanya kila kitu mwenyewe.....hebu fikiri mtu ana watoto watatu chini ya miaka mitano na anawajibika kufanya shughuli zote za nyumbani peke yake na bado mume akirudi anaamrisha kila kitu afanyiwe! nguo afuliwe, anyooshewe, atekewe maji ya kuoga, apikiwe chai ya jioni, na shughuli nyingine zitakazojitokeza hususan wanapotokea wageni....cha kushangaza huyo mwanaume akirudi kutoka kazini, kama hatakuwa hasomi gazeti basi atakuwa anaangalia TV au kutoka kwa matembezi ya jioni.....Hivi huyu ni mawanaume wa aina gani?

    nilimsikitikia sana huyo shoga yangu, na kwa bahati mbaya alikuwa anaumia ndani kwa ndani kwani anamuogopa sana huyo mumewe....ambaye anatokea kule kwa akina NG'WANAMBITI

    ReplyDelete
  5. Bwana Kaluse. Asante sana kwa wema wako na maneno yako ya kutia moyo wakati ule wa msiba. Nimerudi kwenye chakula kitamu rasmi sasa. Tuko pamoja.

    Najitambulisha tu na nitarudi baadaye kuchangia mada hii nzuri.

    ReplyDelete
  6. Asante kwa mada nzuri iliyo ktk rugha nyepesi kiasi cha kueleweka vyema kwa msomaji! Kaka shabani mungu akujarie maisha marefu ili uzidi kuponya ndoa za watanzania bila malipo.

    ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi