0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

http://www.serenahotels.com/serenadaressalaam/default-en.html

Jan 31, 2009

TUNAPOKULA NA KUSAZA: JE JIRANI NAYE KALA?

Tujiulize kama nao wamekula

Kila mmoja wetu anajipenda na ni wazi wengi wetu kama sio karibu wote tunajipenda zaidi kuliko tunavyowapenda wengine, iwe ni ndugu, jirani, rafiki, au mpita njia. Tunaweza kujifanya kwamba tuna upendo mahali ambapo hakuna kujitolea au kujitoa muhanga, lakini unapofika wakati kama huo uongo hujitenga na ukweli unaosikitisha kudhihiri.

Wengi wetu tuna kwenda misikitini, makanisani, na hata jamatini na kwenye mahekalu au kutambika. Kote huko lugha ya upendo inazungumzwa sana. vitabu vyetu vitukufu vinatuambia kwamba ni jambo muafaka na heri zaidi kuwapenda jirani zetu kama sisi tunavyo jipenda mwenyewe. jirani zetu kwenye vitabu hivyo ina maana ya mtu yeyote ambaye uko naye katika kipindi husika. Hii ina maana kwamba tunashauriwa kumpenda kila mtu mahali popote tulipo na alipo.

Lakini jambo la ajabu na linalo sikitisha ni kwamba ni wachache sana kati yetu ambao wana upendo kwa watu wengine zaidi ya nafsi zao. Kila mmoja kati yetu anataka kuhakikisha kwamba amepata nafasi amefaidika yeye na kuridhisha nafsi yake kwa mapana yote ndipo amfikirie au kumkumbuka mwingine, kama hata hivyo itatokea kumfikiria au kumkumbuka huyo mwingine.

Sasa hivi tunaishi kwenye jamii ambayo ni sehema ya jamii ya dunia kwa kila kitu-utamaduni, tabia, maendeleo na mabadiliko ya kila siku ya mfumo wa habari na maarifa. Dunia nzima hivi sasa inaendelea kufanywa ndogo zaidi na athari za ubabe wa kibepari ambazo watu wa jamii kama hii yetu hawakuwa wanazitazama hata kwa miaka mia ijayo.

Leo hii Tanzania iliyokua ikiamini katika thamani ya mtu kwa utu wake na mchango wake kwa jamii imebadilika na kuanza kuamini katika mali kama kigezo mahususi cha kupimia utu wa mtu. Leo hii kila mmoja anajitahidi kwa njia yoyote apate mali ili kuhuisha thamani yake. Katika juhudi hizi wengi wetu tumejikuta tukitoka katika ubinadamu na kuingia kwenye hali ya unyama halisi.

Pengo kati ya wale walionacho na wasionacho linazidi kuwa kubwa kila kukicha. Walionacho kwa bahati mbaya wanazidi kujilimbikizia na kutapanya mali walizonazo kwa nia ya kufurahisha nafsi zao zaidi bila kujua kwamba pembeni kuna wengi ambao ndio waliowafanya wao kuwa nacho wakipiga mikambi ya kifo kwa njaa na maradhi.

Kila aliye nacho leo anajitahidi kushindana na mwingine kutokana na udhaifu wa nafsi. anataka kujenga nyumba ya ghorofa moja anataka kununua gari la milioni mia moja zuri zaidi ya lile la mwingine, anataka kusafiri ulaya kutalii kila baada ya mwezi mmoja, zaidi ya yule mwenzake anayekwenda kila baada ya miezi mitatu, anataka wanae wasome shule wanayosoma watoto wa Obama, zaidi ya yule mwingine ambaye wanawe wanasoma shule waliyosoma watoto wa
George Bush.

Hakuna kati ya wale walionacho ambaye ameshawahi kujiuliza kuhusu hali za wale ambao hata nauli ya daladala, mlo mmoja wa rahisi wa kutwa, panado ya kutuliza maumivu na ada zinawashinda. Hakuna anayejali hakuna anayejiuliza na hakuna anayebugudhiwa na hatima ya wanyonge hawa ambao ni ndugu zao, wazazi wao na hata watoto wao.

Imefika mahali ambapo sio dhambi hata kidogo kwetu kujiuliza kama kuna ridhiko la kweli la moyo kwetu sisi kufanya “matanuzi” yaliyopindukia wakati kuna wale waliotuzunguka ambao wangetamani kupata hata moja ya milioni kumi ya kile ulicho nacho waweze kuishi nao kama binadamu.

Inakuwaje basi tunathubutu kwenda kanisani au misikitini na kupiga goti au kusujudu tukimwomba Mungu mwenye upendo atupe nusura, wakati mioyo yetu ni migumu kiasi hicho!
Naona umefika wakati ambapo wale walionacho wanatakiwa wajiulize wanajisikia vipi kuona kwamba wamezungukwa na watu wenye dhika na mateso. Wanafaidi kitu gani katikati ya ulitima wa wengine? Je, kweli watayaita hayo walio nayo ni mafanikio, wakati wanajua wazi kabisa kwamba wangeweza kutoa hata moja kwa milioni ya kile walichonacho ili kuwasaidia wengine, lakini kamwe hawajawahi kufanya hivyo?

Ukiacha kushitakiwa na dhamira zao, ni lazima wajue kwamba upande wa mzani wa walionacho ukizidi kudondokea chini wakati wa wasionacho ukipanda juu, suala litakua sio mtu anavyojisikia moyoni, bali suala litakua “nikimbilie wapi niinusuru nafsi yangu?”
Kila uovu una malipo yake. Kukosa upendo kwa kutowajali wengine kuna malipo mabaya zaidi ya kiroho na kimwili na haya hulipwa hapa hapa duniani kwa mtindo ambao huwa haupendezi.

Tujifunze kujiuliza kila siku swali hili; mimi ninakula na kusaza, je jirani anauwezo wa kupata hata kile ninachosaza mimi? Kama huwezi, basi tujifunze kula kwa kadri yetu ili kile ambacho tungesaza tuwape wengine. Tujifunze kufurahi wengine wanapofanikiwa kama sisi na nzuri zaidi kama mafanikio yao yatakuwa tumeyachangia hata kwa kiasi kidogo.

4 comments:
Andika Maoni Maoni
  1. Kuna kale kamsemo ninakokasikia kakiimbwa saana kwenye reggae kasemacho "Hero to zero". Na hapa tumewaona wengi. Tumemuona Mobutu aliyekuwa anapiga mswaki kwenye sink lenye madini akifa mbali na kwake. Tumemuona Saddam aliyekuwa ana chumba cha dhahabu akimalizia siku za mwisho jela na kabla ya hapo akiwe kwenye shimo. Tumewaona kina Milosevich na maisha yalivyowageuka. Idd Amini alivyokimbia nchi akafia nje na wengine wengi. Sijisikii kugusa hali ya nyumbani maana huko nako ni kinyaa. Hawa hawana tofauti na tuwaonao sasa. Kuna mwisho na hauko mbali kwa wote watendao haya. Pengine na wengine watapuuzia fikra na mtazamo lakini twatambua kuwa mabadiliko yanakwenda kwa kasi na muda si mrefu utaona maisha bila ulichonacho yalivyo.
    Naamini umesema yote Kaka. Asante kwa somo zuri la kuanzia wikiendi.
    Blessings

    ReplyDelete
  2. Kaka Mubelwa, Makala hii niliiandaa wakati nilipoamua kutembelea kituo kimoja cha watoto yatima.
    Sikwenda kule kupeleka chochote bali nilikwenda kujifunza na kuona mazingira wanayoishi watoto hawa.
    Nilijifunza mambo mengi sana na ndipo nilipoamua kukaa chini na kuandika makala hii.
    Huu ndio mchango wangu katika kuikumbusha jamii kuhusu kundi hili la watu wasioweza kumudu hata mlo mmoja kwa siku, kundi ambalo linazidi kukua kila uchao.


    Ahsante kwa maoni yako.

    Blessings....

    ReplyDelete
  3. Unachokisema Kaluse ni sahihi kabisa.Tatizo kubwa jamii yetu naona inaishi kwa hofu kubwa ya kesho hali hii ndiyo ambayo inapelekea kuwe na kujilimbikizia mali,si chakula tu.Mara ngapi mtu ananunua nguo bila ya kuzivaa wakati anajua kuna mdugu yangu hana uwezo wa kuvaa nguo?Yaani tunalimbikiza kila kitu kwa hofu ya kesho.
    Ukweli ndugu zangu furaha ya ndani haitokani na kuwa na malimbikizo mengi ya mali,furaha ipo pale unapoona wengine wanafurahia maisha kutokana na wewe na wewe pia kutokufanya kwa kujionyesha kama tunavyoona watu wakienda kutembelea au kutoa msaada katika vituo vya watoto yatima wanataka waandishi wa habari waende ili waje waonekane kwenye luninga.
    Jamani tubadilike tuwe tunawakumbuka wenzetu walioko kwenye matatizo.

    ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi