0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Jan 1, 2009

JE UNAYO MALENGO GANI MWAKA HUU WA 2009?

Ndugu wanablog wenzangu na wasomaji wa blog hii, napenda kuchukuwa nafasi hii kuwatakia heri ya mwaka mpya.

Leo ninayo mengi ya kuzungumza na ninyi juu ya huu mwaka tunaouanza leo hii.

Je umejiwekea malengo gani mwaka huu ?

Je ungependa kuona mabadiliko yakitokea katika maisha yako kwa ghafla? Ungependa kufikia malengo yako mara moja?

Najua ungependa kufikia malengo yako mara moja na si baadaye. Hiyo ni kwa sababu tumejengwa katika kufikiria kwamba tunaweza kupata vitu mara moja, tunapotaka. Utake, usitake, hivyo ndivyo tulivyojengwa, lakini siyo kwamba, ndivyo inavyotakiwa.

Unaweza kutuma ujumbe kwa mtu aliye mbali sana duniani, kutoka ulipo na ujumbe huo akaupata baada ya sekunde chache. Tunazo simu zinazotuma ujumbe wa maneno, simu za zinazoweza kutupatia mawasiliano mara moja na popote tulipo.

Vitu vingi vinazidi kuwa vya haraka siku hizi. Hata hivyo si kila kitu, kwani bado inahitajika miezi tisa kwa mwanamke kuweza kukaa na ujauzito kabla ya kujifungua. Baada ya kujifungua, mtoto huyo bado atahitaji angalau mwaka mmoja kabla ya kuanza kutembea mwenyewe na angalau miaka mingine miwili ili aweze kuongea bila matatizo.

Inahitajika miezi michache kwa mboga kama nyanya kukua kutoka mbegu mpaka kuwa tayari kuliwa. Wakati inawezekana ukawa na hamu ya kuona malengo yako yanatimia mara moja, ukweli ni kwamba hamu yako ya kuleta mabadiliko ya haraka yaweza kukuletea madhara zaidi kuliko faida.

Kwa nini? Kwa sababu unakosa subira na hivyo unafanya mambo yako kinyume na utaratibu wa maumbile. Ukosefu wa subira hutuma ujumbe hasi kwenye mawazo yako ya kina na wakati huohuo unakuwa unafanya mambo kwa kupingana na taratibu za maumbile.

Kwa kufanya hivyo hutumii kile kinachofahamika kama Nguvu ya Subira. Hii Nguvu ya Subira yaweza kupatikana kwa hatua mbalimbali, zikiongozwa na kufikiri kwako.

Wakati unapokosa subira katika kupata mafanikio, unachofanya ni kuisukuma nafsi yako mbali zaidi kutoka kwenye mafanikio. Wengi wetu hutaka vitu tunavyoamua kuvipata, tuvipate hapohapo, na pale tunapoamua kubadilika, ama kuboresha hali zetu, tunataka mabadiliko hayo yatokee mara moja ili tuweze kuanza kufurahia maisha yetu mapya na kuanza kufurahia mafanikio.

Lakini sisi ni sehemu ya maumbile na maumbile hayabadili vitu mara moja, hivyo mabadiliko ndani yetu nayo hayawezi kutokea mara moja. Mchakato unaweza kuanza mara moja, lakini mabadiliko kamili hayawezi kutokea mara moja.

Kwa vile sisi ni sehemu ya maumbile, ni lazima tufanye kazi kama maumbile yanavyotaka na kwa kufuata taratibu zake. Wanawake wamekuwa wakijifungua watoto tangu mwanzo wa dunia, na mpaka sasa bado wanahitaji miezi tisa ya kubeba mimba kabla ya kupata watoto.

Huenda tungependa haya kutokea mara moja, lakini tunatakiwa kuruhusu maumbile yafanye mambo kwa kufuata ratiba yake, hivyo tunakuwa na subira wakati linapokuja suala la kupata mtoto.

Linapokuja suala la kufikia malengo yako, mawazo yako ya kina, kama yalivyo maumbile, yanatakiwa kufanya kazi kwa kupitia mchakato na kukuruhusu kwenda kwa hatua kuelekea kwenye mafanikio ya malengo yako.

Ralph Waldo Emerson, mkongwe wa ufahamu, aliwahi kusema. Fuata mwenendo wa maumbile, siri yake ni subira. Subira hiyo yaweza kukufikisha kwenye maisha bora kama unajua jinsi ya kufanya kazi na Nguvu ya Subira na maumbile kwa pamoja.

Kwa nini subira ni ya lazima kwa mafanikio?

Muulize mfanyabiashara yoyote aliyefanikiwa ama yeyote aliyefanikiwa bila ujanjaujanja, atakwambia kwamba, hakufikia uamuzi mara moja. Huchukua muda mrefu wa utafiti, kufuatilia na kufikiria, wakisubiri hadi muda muafaka kufanya uamuzi.

Maumbile hufanya kazi kupitia mchakato maalum na yana uwezo mkubwa wa kusubiri.

Kwa mfano: Unataka kupanda mbegu, imwagilie maji, iache kwa muda, na utakapofikia muda muafaka, wakati kila kitu kiko sawa, mbegu hiyo itaanza kuota na baadaye mmea. Hii ni kwa mmea wowote utakaoupanda.

Hii hutokea tu wakati hali inapokuwa sawa, lakini kulikuwa na kazi iliyokuwa ikiendelea kufanywa kabla ya matokeo yote haya kuchukua nafasi yake.

Mbegu inatakiwa kupandwa, inatakiwa kutunzwa, inatakiwa kuachwa ili ianze kutoa mizizi michanga ardhini, na baadaye muda utakapofika mmea unaanza kujitokeza juu ya ardhi katika hali hasa iliyotarajiwa.

Bila kuweko kazi ya mwanzo ya kupanda na kumwagia maji mbegu, mmea usingetokeza juu ya ardhi, na hungeweza kuwa na bustani yako ya matunda ama maua ambayo huenda hivi sasa unakula matunda yake.

Kama unataka kufikia malengo yako, iko haja ya kuwa na subira ya aina hiyo. Hii haina maana kwamba ukae kitako na kusubiri kila kitu kiende kwa wakati wake. Badala yake unatakiwa kufanya kazi kwanza, kuweka msingi, kupanda mbegu, na kuhakikisha ardhi unayolima ni ya kufaa. Tayarisha na usubiri kwa kila hali kuwa sawa kabla ya kutoa maamuzi sahihi yatakayokusukuma kwenye mafanikio makubwa.

Kwa bahati mbaya, watu wengi hawako tayari kufuata mchakato huu na badala yake wanataka kwa siku moja kupata kila kitu katika maisha yao. Siyo wazuri kafuata taratibu zinazokubalika za vitu kubadilika, na hivyo hujikuta wakitaka vitu vibadilike mara moja na hivyo kuishia wakichanganyikiwa na kukata tamaa kutokana na mabadiliko haya ya ghafla kushindikana.

Moja kwa moja hiyo huwa haifanyi kazi. Wakati unapofanya kazi kinyume cha maumbile, unasukumwa nyuma zaidi.

Ikiwa unataka kufanikiwa, unatakiwa kuwa na subira kwa kiasi fulani. Fikiria kile unachotaka kufanikisha, fikiria kuhusu mabadiliko unayoyataka, anza mchakato wa kuleta mabadiliko haya kwa kujua kile unachotaka na kwa nini.

Pandikiza mbegu zako za mafanikio kwenye bustani ya akilini mwako. Kuwa na subira ukisubiri alama za nyakati za kukuruhusu kuendelea. Hakikisha mawazo yako ya kawaida na yale ya kina yanafanya kazi kwa pamoja ili kukusaidia kufikia malengo yako.

Wakati unapokosa subira, wakati unaposhindwa kuamini na kukubali kwamba mambo yatakuwa, huwa unapunguzwa kasi yako, kukwamishwa na hatimaye kuishia kwenye njia isiyo sahihi na baadaye unashangaa: ‘Nimefika vipi hapa?’

Kwa mfano, uko kwenye foleni ukisubiri kulipia kitu fulani, foleni ni ndefu, lakini kuna mtunza fedha mwingine ambaye naye ana foleni ndefu kama hiyo. Kama utachoka na kukasirika, haitakusaidia. Ikiwa utaamua kuhamia mstari mwingine, hiyo huenda ikakuchukua muda mrefu zaidi, kama utaacha na kuondoka, hutopata kile unachohitaji.

Unaweza kuamua kuondoka ukipanga kurudi foleni itakapopungua, lakini baadaye ama ukashindwa kurudi ama unaporudi ukakuta foleni ni ndefu maradufu ya ile ya kwanza na hivyo kuamua kuachana kabisa na zoezi hilo ulilotaka kulifanya, na hivyo kukosa kile ulichotaka.

Unapokosa subira unakasirika haraka, ukidhani mambo ni rahisi upande wa pili, lakini ukaondoka bila kupata kile unachotaka.

Kama ungekuwa na subira, ungeweza kufanya malipo yako na kuendelea na kile ulichotaka.

Usifikirie mambo ni mazuri upande wa pili, shughulika na kile ulichonacho na kile unachojua na hivyo kuwa na subira na utatoa maamuzi sahihi. Ukikimbilia Marekani kwa kudhani huko mafanikio yanakuja mara moja, utashangazwa. Utakaa huko kwa miaka kumi na ukirudi hapa nchini, utakuta uliyemwacha akiwa anafanya kile ulichoona hakilipi, akiwa mbali sana.

Ni vigumu mtu kuanza na kufanikiwa kupata fedha nyingi katika kipindi kifupi kama cha miezi mitatu, kwa sababu lazima zitakuwepo taratibu zinazohitaji kufanyika kama ilivyo kwa wakati wa kupanda mbegu.

Ikiwa utakuwa na subira na kungojea mchakato ufikie wakati wake, ni wazi utapata mamilioni ya fedha si kwa miezi mitatu tu, bali katika kipindi kirefu cha maisha yako, mpaka pale utakapokiuka mchakato wake.

Unaweza kujaribu kufanya mambo ya haraka kwa kujaribu mradi na hivyo kuwekeza kwenye miradi ya hatari na pengine kuishia kuingia kwenye uchezaji wa kamari na bahati nasibu, lakini ni wazi utapoteza fedha nyingi zaidi.

Hata unapoyatazama maisha ya binadamu, utakuta yanafanya kazi kwa kufuata utaratibu wa maumbile, utaratibu wa kusubiri.

Tunaanza tukiwa watoto wadogo, tunakuwa, na kuwa watu wazima na umri unazidi kupanda hadi kuzeeka, kama ilivyo kwa utaratibu wa maumbile. Mtu hawezi kuzaliwa leo na kufikia umri wa utu uzima ili aweze kuwahi nafasi fulani ya kazi ambayo hivi sasa iko wazi.

Mafanikio katika maisha huwa hayatokei kwa usiku mmoja. Kuanzisha biashara na kuifanya ifanikiwe kunahitaji subira. Kukosa subira katika biashara ni kualika janga.

Uhusiano nao huchukua muda kuujenga na kuuboresha, kukosa subira katika uhusiano ni njia fupi ya kuhitimisha uhusiano huo.

Kutafuta kazi sahihi kunahitaji subira na juhudi, kukosa subira katika kutafuta kazi ni njia rahisi ya kuikosa kazi hiyo.

Mambo yanaweza kutokea ghafla, lakini mafanikio yanahitaji subira. Kwa mfano, waweza ukakutana na mwenza wako hata leo, lakini mafanikio ya uhusiano wenu huo yatahitaji subira ili yaweze kukua na kufanikiwa.

Unaweza ukawa na wazo la biashara hata leo, lakini kwa biashara hiyo kuweza kukua hadi kufikia mafanikio kutategemea jinsi utakavyokuwa na subira si kwa kazi tu, bali pia kwa wafanyakazi wenzako na viongozi wako.

Ili kuanza kujenga msingi wa mafanikio yako leo, anza kupanda mbegu hivi sasa ili uweze kupata mafanikio yako hapo baadaye.

Mafanikio yatakuwa yako, wakati unapofanya kazi kwa nguvu ya subira na kufuata sheria za kawaida kabisa za maumbile. Ruhusu mawazo yako ya kina yakuongoze kuelekea kwa watu na hali ambazo zitakurusha kuelekea kwenye mafanikio.

Watu wawili waweza kuanza kufanya kazi kwenye kampuni moja, wote wakiwa wameanzia katika kiwango kimoja cha cheo kazini na wote wakiwa na matumaini ya kupata mafanikio makubwa hapo baadaye.

Mmoja siku zote anakuwa na subira, akiwa ni aina ya watu wavumilivu. Mwingine anaonekana kuwa na haraka, kila wakati akitaka kupata vitu kwa haraka, akionesha wazi kutokuwa na subira na kila wakati akitaka apate zaidi kwa haraka.

Baada ya mwaka mmoja tu, huyu wa pili akawa tayari anataka kupanda cheo na hivyo akaanza kutaka mshahara mkubwa na kupandishwa cheo huku akitishia kuacha kazi.

Miezi michache baadaye akaacha kazi na kumshawishi mwenzake achukue hatua kama hiyo, lakini mwenzake akaamua kubaki.

Kuanzia hapo akawa anahama kutoka ofisi moja hadi nyingine, akitafuta mshahara mkubwa zaidi na kama kuna mahali alipodumu kwa muda mrefu, basi si zaidi ya miaka miwili. Hatimaye mtu huyu anakuta jina lake likiwa limeharibika, kwani anakuwa amepitia sehemu nyingi mno kiasi cha kuwatia wasiwasi hata wale wanaotaka kumwajiri.

Hakuna mwajiri anayetaka kumwajiri mtu asiye na subira, mtu anayejua akimwajiri ataweza kuondoka wakati wowote, tena ghafla na kumsababisha atafute mtu mwingine bia kutarajia.

Wakati huyu mmoja akihamahama, yule aliyebaki na kampuni ya mwanzo atajikuta akiwa amepanda na kuwa katika ngazi ya juu, kwani hata mwajiri wake atakuwa anamwamini.

Nguvu ya subira ina uwezo wa ajabu na inaweza kukuletea mafanikio ambayo hata wewe hutoweza kuamini.

Ni nguvu hii utakayoweza kuitumia ili kupata kazi unayoitaka, kukutana na watu sahihi na hata kufanya kazi kwa kutumia nguvu hii ili kuwekeza katika sehemu sahihi.

Ikiwa utapanda mbegu na kukesha ukiisubiri iote, utakuwa kichaa, ikiwa utapanda mbegu na kuisahau ukidhani unaisubiria, itakufa na ikiwa utaipanda na kuiwekea jiwe juu yake, haitajitokeza nje ya ardhi. Lakini ikiwa utapanda mbegu na kufanya kazi ya kuimwagilia maji na kuitunza, itaota na kumea vizuri.

Hivi ndivyo nguvu ya subira inavyofanya kazi. Fanya kazi zako vizuri kabisa, kuwa na subira na uelewa kwamba vitu vitakuja wakati utakapokuwa muafaka. Kama unatafuta kazi mpya, fanya kila uwezalo kupata kazi hiyo. Lakini uwe na subira ukijua wakati utafika, nawe utaipata.

Kuna tofauti kati ya subira na kungoja. Kungoja si kusubiri. Kungoja ni kupoteza wakati. Kusubiri hakuna maana kuwa ni lazima ungojee.

Unaposubiri unafanya kile kinachohitajika ili kuboresha maisha yako huku ukielewa kwamba mabadiliko yatatokea wakati muafaka. Unajitayarisha huku akiamini kwamba mabadiliko yatakuja. Lakini unapongoja, unakaa ukiwa na matumaini ya kuboreka kwa hali yako, bila kufaya jitihada za kutosha.

Usikae chini na kungoja, ni wajinga tu wanaoweza kufanya hivyo.

Timiza sehemu yako ya subira kwa kufanya kazi na nguvu ya subira kwa kufanya kila unalohitajika kufanya ili kufanikiwa katika maisha yako, huku ukijua kwamba mambo yatakuwa mazuri na baadaye ujaribu vitu vinavyowezekana katika kufanikiwa. Ikiwa utaketi chini na kungoja, utajinyima nafasi hizo za kufanikiwa.

Unaweza kufurahia mfanikio yako na zaidi, kuelekeza mawazo yako ya kawaida na yale ya kina ili zikusaidie kujenga maisha unayoyataka.

Anza kufanya kazi kwa kutumia nguvu ya subira na utaanza kusonga mbele.

Nakutakia heri ya mwaka mpya.

2 comments:
Andika Maoni Maoni
  1. Hii kweli karibu mwaka 2009. duuh mkuu mada ya moto

    ReplyDelete
  2. mh mada ndefu ila ninajiuiza kidogo, eti mfanikio nini? koua mke mzuri? kufungua duka? kulewa sana? kunyoa panki? ku-blog? kuongea kiswanglish? kwenda ulaya? kuwa na utu? kujisikia? kujiona? kuokoka? kujigamba? au kupata digirii?

    ReplyDelete

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi