0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

Nov 7, 2008

HIVI NI MPAKA THAMANI ZETU ZIONEKANE MAHALI PENGINE?


Juzi nilitembelewa na rafiki yangu mmoja aitwae Mkude (Sio jina lake halisi) ambaye miaka ya tisini niliwahi kuishi nae jirani huko maeneo ya Mwananyamala, hapa jijini Dar Es Salaam.

Rafiki yangu huyu alikuja kunitaka ushauri juu ya mtihani uliokuwa umemkabili kuhusiana na uamuzi ambao alitakiwa kuuchukuwa.

Kwa kifupi alinifahamisha kuwa amepata kazi mahali pengine kwa ahadi ya kulipwa mshahara mara tatu zaidi ya mshahara aliokuwa akilipwa na mwajiri wake wa sasa.

Tatizo ni kwamba mwajiri wake wa sasa nae amekubali kumuongezea mshahara mara nne zaidi ya mshahara aliokuwa akimlipa.

Sasa hakujua achukuwe uamuzi gani kwani kule alikopata kazi walishakubaliana kila kitu na alishasaini mkataba wa ajira, na huku kwa mwajiri wake wa sasa ambapo amefanya kazi kwa zaidi ya maiaka 15, amemuomba abatilishe uamuzi wake kwa ahadi kwamba atamuongezea mshahara mara nne ya mshahara anaomlipa ikiambatana na marupurupu mengine.

Ukweli ni kwamba rafiki yangu huyu ametoka mbali sana na mwajiri wake huyu ambaye anamiliki kampuni ya uchapishaji wa vitabu na majarida.

Awali alianza kazi kama msaidizi wa ofisi wengi huita mesenja, lakini wakati mwingine alikuwa akihitajika kusaidia kazi za uchapaji kama kazi zikiwa zimezidi.

Kutokana na uchapakazi wake baadae akahamishiwa kwenye kazi za uchapaji na nafasi ya uhudumu wa ofisi akaajiriwa mtu mwingine kuchukuwa nafasi yake hiyo.

Rafiki yangu hakuishia hapo kwani alikuwa ni mtundu na mwenye bidii sana na anaependa kujituma, akajifunza ufundi wa kuzitengeneza zile mashine.

Ilikuwa ni kawaida yake kila mafundi wakuzifanyia matengenezo zile mashine wakiitwa pindi zikiharibika au zikihitaji matengenezo ya kawaida yeye huwa nao karibu akijifunza bila wao kujua.

Haikupita muda matunda yakaonekana, ikawa kila mashine zikipata matatizo madogo madogo yeye anakuwa anazitengeneza, hivyo wale mafundi wakawa hawaitwi mara kwa mara kama zamani.

Ingawa mwanzoni mwajiri wake alikuwa hamuamini, lakini ikatokea siku moja walikuwa na kazi moja muhimu sana ambayo ilikuwa ikihitajika haraka.

Wakati kazi ikiendea, ile machine pekee iliyokuwa ikitegemewa katika kazi ile ikaharibika.
Kwa kuwa mashine yenyewe ilikuwa imenunuliwa karibuni, japo ilikuwa imetumika huko ilikotoka mwajiri wake hakutaka aiguse, hivyo aliwaita mafundi wake aliokuwa akiwaamini ili waje waifanyie matengenezo kazi iendelee.

Wale mafundi walipofika waliifungua ile mashine na kuanza kuifanyia matengenezo.
Baada ya kuhangaika nayo kwa takribani masaa nane mashine haikutengemaa, wakadai kuwa kuna kifaa kimoja ambacho walikitoa na kumpa mwajiri wake na kumwambia kuwa ndicho kilichoharibika.

Kilichomchanganya mwajiri wake ni ile kuambiwa kuwa kifaa hicho hakipatikani nchini labda mpaka Nairobi nchini Kenya.

Baada ya kutoa maelezo yale mafundi wale wakaondoka zao, na kumuacha mwajiri wake akiwa amechanganyikiwa.

Ikabidi mwajiri wake aanze kuwasiliana na Viwanda vingine vya uchapaji ili ikiwezekana kazi ile ihamishiwe kwenye kiwanda kingine.

Rafiki yangu huyu aliporudi nyumbani hakulala alikuwa akiwaza juu ya ile mashine, na ilipofika asubuhi aliwahi kazini mapema zaidi, alipofika alikwenda kwenye ile mashine na kuifungua, na kwa kuwa mwajiri wake alikuwa hajafika aliweza kuisoma kwa makini bila bughudha ingawa msimamizi mkuu wa kiwanda kile alionesha wasiwasi kidogo.

Haikumchukuwa muda mrefu kugundua tatizo, na kulirekebisha na hivyo mashine ikaanza kufanya kazi kama kawaida.

Mwajiri wake alipofika alishangaa kukuta kazi ikiendelea kama kawaida na alipouliza ndipo alipojulishwa na msimamizi mkuu kwamba Mkude ndiye aliyeitengeneza.

Mwajiri wake hakuamini alikwenda kuichunguza ile mashine pamoja na kumuuliza maswali kadhaa Mkude na baada ya kugundua kuwa inafanya kazi vizuri aliridhika.
Kuanzia hapo ikawa wale mafundi hawaitwi tena kuzifanyia matengenezo zile mashine, na kazi hiyo akawa anaifanya Mkude.

Tukio hilo lilitokea miaka kumi iliyopita lakini kwa mujibu wa Mkude aliwahi kuongezwa mshahara si zaidi ya mara mbili tena kwa kiwango kidogo sana, na hata akijaribu kumuomba mwajiri wake, amuongezee mshahara, alikataliwa na hata wakati mwingine kutishiwa kufukuzwa kazi kwa kuonekana msumbufu, kwa kifupi thamani yake haikuonekana.

Hata hivyo Mkude hakuridhika na kiwango cha taaluma ile alichojifunzia pale pale kazini kwake
hivyo kwa kujinyima sana aliamua kujiunga na masomo ya jioni katika chuo cha nufundi VETA na kufanikiwa kupata cheti chake cha ufundi wa ofisi mashine daraja la kwanza (Grade 1)

Hata alipowasilisha vyeti vyake kwa mwajiri wake ili japo aongezewe mshahara, mwajiri huyo alikataa kumuongeza, kwa madai kuwa kiwanda hakina tija.

Hatimaye Mkude akaona matangazo ya nafasi za kazi katika kampuni moja ambayo ndio kwanza inafunguliwa na baada ya kutuma maombi yake aliitwa na kufanya usaili, ambapo alifaulu vizuri na kupewa ajira kwa mkataba wa mshahara mnono.

Sasa rafiki yangu Mkude, kashikwa na kigugumizi cha kufanya maamuzi, Je abaki na mwajiri wake wa sasa kwa ahadi ya kuongezewa mshahara mara nne zaidi ya mshahara wa awali au ajiondokee na kwenda kwenye kampuni mpya kwa mshahara mara tatu zaidi ya mshahara aliokuwa akilipwa na mwajiri wake wa sasa?

Naamini wapo baadhi ya wenzetu ambao wamewahi kupatwa na mtihani kama huu wa Mkude. Labda nikuulize wewe msomaji wa blog hii, kuwa Je kama ingekuwa ni wewe Mkude ungechukuwa uamuzi gani?

Ukweli ni kwamba wapo baadhi ya waajiri wamekuwa ni wachoyo wa fadhila au sijui niseme, wana roho mbaya. Hivi kweli mtu anajua kabisa kuhusu utendaji wako wa kazi na anajua umuhimu wako katika kampuni, lakini kwa makusudi kabisa anashindwa kukuongeza mshahara au hata kukupa bonansi kulingana na jitihada zako kazini.

Wakati mwingine hata mfanyakazi anapokuwa ameokoa mamilioni ya fedha katika kampuni, muajiri anashindwa hata kutoa bahashishi kwa mfanyakazi husika au hata kutoa ahsante tu.

Kwa mfano kama tulivyoona katika swala hili la Mkude, aliokoa fedha za kampuni kwa kutengeneza ile mashine, ambayo kama tulivyoona kuwa ingemlazimu mwajiri si tu kuingia gharama ya kuagiza kipuri kutoka Nairobi nchini Kenya bali pia kazi ile ingekwenda kufanywa kwenye kampuni nyingine kwa sababu ilikuwa ni ya haraka, lakini Mwajiri hakuonesha shukurani hata kidogo.

Katika kitabu chao cha Suceeding in the World of Work, waandishi Grady Kimbrell na Ben Vineyard, wanashauri kuwa pamoja na kuwa mwajiri mara nyingi anategemea mfanyakazi alete tija katika kampuni lakini ni vyema mwajiri huyo akaonesha shukrani kwa yule mfanyakazi anayefanya vizuri zaidi ya wenzake.

Wataalamu hao wanabainisha kuwa hata ile kuweka picha ya mfanyakazi kwenye ubao wa matangazo na kutangaza kuwa ni mfanykazi bora wa mwezi na kueleza mchango wake katika kampuni, inatosha kabisa kuongeza ushindani miongoni mwa wafanyakzi wenyewe na kuongeza tija katika kampuni husika, na hii haihitaji gharama yoyote.

Lakini waajiri wengi hawaoni umuhimu wa kufanya hivyo, badala yake huwabana wafanyakazi kimaslahi ili kujitengenezea faida maradufu.

Sasa itokee mfanyakazi huyo huyo kama ilivyotokea kwa mkude apate kazi katika kampuni nyingine kwa mshahara mara dufu zaidi ya mshahara wa kampuni anayofanyia kazi, hapo ndipo mfanyakazi huyo atabembelezwa ili abaki kwa ahadi kibao ikiwepo hata kupandishwa cheo.

Hii ina maana gani? Hii ni sawa na kukupa ujumbe kuwa katika miaka yote uliyokuwa ukifanya kazi katika kampuni hiyo ulikuwa unapunjwa mshahara, tena kwa makusudi!

Hivi ni mpaka mfanyakazi aamue kuacha kazi au apate kazi mahali pengine kwa mshahara mnono ndipo uongozi wa kampuni ambayo mfanyakazi huyo alijitolea maisha yake yote kuitumikia kwa uaminifu na kujituma ndio uone umuhimu wa kumuongeza mshahara?

Ina maana thamani ya mfanyakazi huyo ilikuwa haionekani mpaka ionekane mahali pengine?
Mimi naamini kuwa ni mwenda wazimu pekee anayeweza kubaki kwenye kampuni ya namna hii.
Kwa nini waajiri wasitambue mchango wa wafanyakazi wenye vipaji na juhudi binafsi, na kuwalipa mishahara kulingana na thamani zao?
Kwa nini iwe ni mpaka mfanyakazi aamue kuacha kazi ndipo apandishiwe mshahara au kupandishwa cheo?

Kwa mtaji huu wa kutokujali maslahi ya wafanyakazi hata kwa kile kidogo wanachostahili ni kuwapelekea kuwa wadandiaji wa ajira kwa kutoka kampuni moja hadi nyingine.

Hii ina athiri sana katika kufikia malengo yao na kutokuaminiwa hapo baadae watapokuwa wanaomba kazi mahali pengine.

kwa nini? Kwa sababu kama inatokea mfanyakazi CV yake inonyesha kuwa kwa muda wa miaka mitatu tu ameshafanya kazi katika kampuni si chini ya tano, unadhani ni mwajiri gani anaweza kuajiri mfanyakazi wa aina hii?
Ni lazima atahisi kwamba ipo siku na yeye atabwagiwa manyanga iwapo atatokea mwajiri mwingine atakayepanda dau.

Haihitaji kutumia akili za mwanasayansi wa kutengeneza Roket ili kufikia uamuzi.

Je, wewe msomaji wa blog hii una maoni gani?
Toa mchango wako.

No comments:
Andika Maoni Maoni

This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi