0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

http://www.serenahotels.com/serenadaressalaam/default-en.html

Jul 6, 2013

MWANAMKE: JE, BADO UNA HISIA ZA KUMPENDA MPENZI MLIYEACHANA...?


Kuondokana na hisia za mapenzi dhidi ya mpenzi uliyetokea kumpenda sana lakini mkaachana katika mazingira ambayo hukuyatarajia, si jambo rahisi na hasa kama wewe ndiye uliyeachwa. Unaweza kujiambia kwamba amekosea sana kukuacha na kamwe hatoweza kumpata mwanamke atakayempenda kama ulivyompenda wewe. Lakini kiukweli ndani ya moyo wako unampenda na kitendo cha kukuacha bado kinakuumiza na kukutesa. Inawezekana pia ukawa unatamani sana akurudie kwa sababu ulimpenda sana na unahisi upweke moyoni. Kwa mwanamke aliyeachwa, kuwaza hivyo ni jambo la kawaida kabisa, labda kama hukutokea kumpenda mwanaume huyo. Lakini kama miezi na miaka inapita na bado unaendelea kuwa na mawazo ya aina hiyo, basi hilo litakuwa ni tatizo, na hapa chini nitajaribu kueleza namna ya kuondokana na mawazo ya aina hiyo na kuendelea na maisha, kwani kuachwa na mpenzi sio mwisho wa dunia.



1.Unamuwaza muda wote 


Hili ni jambo la kawaida, lakini duh, kama unajikuta unamuwaza mpenzi aliyekuacha muda wote na kujikuta unashindwa kufanya mambo yako ya msingi kwa ustawi wa maisha yako, basi hilo ni tatizo ambalo linahitaji kupatiwa ufumbuzi. Ingawa waswahili husema “lisilo machoni, halipo moyoni,” lakini mimi nasema sio kila lisilo machoni halipo moyoni, kwa swala la mapenzi nadhani iko hivyo. Ukweli ni kwamba hujui yuko wapi, anafanya nini au yuko na nani na hapo ndipo utakapojikuta ukitafuta picha mlizopiga mkiwa pamoja wakati wa kilele cha mapenzi yenu, na wakati mwingine unaweza kusikia wimbo fulani ambao aliupenda sana ukakukumbusha tukio lililowakuta mkiwa pamoja ambalo linahusiana na wimbo huo. Kwa kifupi ni kwamba, ni jambo la kawaida sana kumkumbuka mpenzi mliyeachana mara kwa mara baada ya kuachana. Lakini kama mawazo hayo yanaonekana kukuumiza na kukupotezea muda basi jua kwamba, jambo hilo linaweza kukuletea matatizo makubwa sana kiafya.



Namna gani utaondokana na tatizo hili: Muda ni nyenzo muhimu sana katika kuponya. Kama unashindwa kupata suluhu ya namna ya kuondokana na mawazo ya huyo mpenzi mliyeachana naye, basi jipe muda, kwani kwa kujipa muda zaidi unajipa nafasi ya kuponya majeraha ambayo yanaonekana kukutesa. Kwa jinsi muda unavyochukua nafasi ndivyo unavyomudu kusahau na ndio maana waswahili husema yaliyopita si ndwele tugange yajayo

2.Unaogopa kumkubali mwanaume mwingine…


Mojawapo ya dalili za kuonyesha kwamba bado unamkumbuka mpenzi wako uliyeachana naye ni kitendo cha kuogopa kuwa na mtoko na mwanaume mwingine. Unachofanya na labda hukijui ni kulinganisha wanaume wanaokuomba mtoko na huyo mpenzi wako, na mara nyingi kinachotokea ni kwamba kila mwanaume unayekutana naye anakuwa na tofauti kubwa na mpenzi uliyeacha naye na hapo ndipo unapojikuta ukishindwa kukubali kutoka naye. Jambo usilolijua ni kwamba sifa za huyo mpenzi wako uliyeachana naye unaziweka juu sana kiasi kwamba kila mwanaume unayekutana naye unashindwa kumpa nafasi kwani unajaribu kumfanya huyo mpenzi wako mliyeachana naye kama vile ni mtu asiye na kasoro kabisa jambo ambalo si kweli.



Namna ya kuondokana na tatizo hilo: Usilazimishe. Kama huko tayari kutoka na mwanaume mwingine, basi jipe muda kwani ukilazimisha, hutakuwa unamtendea haki huyo mpenzi mpya kwa sababu kuna uwezekano mkubwa wa kugombana mapema mno kutokana na kujaribu kwako kutaka kumbadilisha afanane na mpenzi mliyeachana naye. Na kama ikitokea uhusiano wenu ukavunjika mapema, itakuumiza zaidi. Hata hivyo naomba kutahadharisha kwamba kuwa na mtoko na mwanaume haina maana ya kuingia katika mahusiano. Wakati mwingie kuwa na mtoko na mwanaume na kujirusha katika klabu mbalimbali za starehe inasaidia sana kuharakisha kukuondoa katika maumivu ya kuachana na mpenzi wako wa zamani. 


3. Unaumia sana baada ya kumuona akiwa na mpenzi mwingine….

Inaumiza sana baada ya kugundua kwamba mpenzi wako kapata mpenzi mwingine nakuendela na maisha muda mfupi tu baada ya kuachana kwenu. Yaani wakati wewe bado unauguza vidonda vya kuachana na mpenzi wako, yeye zamaaani keshakusahau na kusonga mbele na maisha huku akiwa na mpenzi mpya. Hii inauma sana na ni sawa na kukupiga kofi la usoni.Iwapo umeachana na mpenzi wako halafu inatokea unamkuta akiwa na mpenzi mwingine na hali hiyo ikawa haikushtui wala kukukera basi jua kwamba, jambo hilo limeshapita na umemudu kuondokana nalo. Lakini kama ukikutana na mpenzi mliyeachana akiwa na mwanamke mwingine na jambo hilo likakuumiza kihisia na kuhisi wivu basi ujue kwamba, bado unampenda mpenzi huyo na bado hujamudu kumuondoa mawazoni mwako.



Namna ya kuondokana na tatizo hilo: Endelea na maisha na huhitaji kujiumiza kwa kumuwaza sana, haitakusasidia kumrudisha. Ni kweli kwamba, kitendo cha kumuona akiwa na mwanamke mwingine kinakera na kinaumiza hisia, lakini kumbuka kwamba huna jinsi, maji yameshamwagika. Jaribu kuutumia muda wako mwingi na marafiki au familia yako na jichanganye na marafiki wenye upendo ambao watakufariji na kukutoa katika simanzi ya kujeruhiwa kihisia.


4. Bado unatembelea maeneo mliyokuwa mkitoka pamoja…


Kama unajikuta bado unatembelea katika maeneo mliyokuwa mkitoka pamoja wakati wa kilele cha mapenzi yenu, inaweza ikawa ni kwenye Mghahawa, ukumbi senema, au klabu ya usiku, basi inawezekana bila kujijua unajikuta ukipenda kutembelea katika maeneo hayo ukitarajia kuonana naye. Lakini inawezekana ukawa unatembelea maeneo hayo ukiwa na dhamira ya kuonana naye. Unaweza kujipamba hasa na lebasi za ulimbwende na mavazi ya thamani na kwenda katika maeneo hayo kwa lengo la kutaka akuone jinsi ulivyo mzuri na ulivyopendeza ili akurudie. Kama unajikuta ukifanya hivyo, basi jua kwamba hujaondokana na jakamoyo la kuachwa na kama akikuona asipoonyesha kujali wala kuvutiwa na wewe, utaumia zaidi.



Namna ya kuondokana na tatizo hilo: Acha ujinga mwanamke. Fanya kinyume chake na badilisha maeneo ya kutembelea na punguza mitoko kwa kadiri uwezavyo kama unayo dhamira hasa ya kumuondoa katika mawazo yako. Iwapo marafiki zako unaotoka nao wanasisitiza kwenda katika maeneo ambayo mlikuwa mkitoka na huyo mpenzi wako na unahisi unaweza kukutana naye, kutokana na yeye kupenda sana kutembelea maeneo hayo, basi ni vyema usitishe huo mtoko.



5. Unafanya vibweka katika mitandao ya kijamii......


Hii mara nyingi hufanywa na mabinti wa siku hizi wanaotumia mitandao ya kijamii kama Facebook, twitter nk. Mabinti wa siku hizi hutumia sana mitandao ya kijamii katika kuwasiliana na kuweka picha za matukio yanayowahusu. Iwapo inatokea unatumia mbinu mbalimbali za kuweka picha zako katika mitandao ya kijamii ambazo zinaamsha hisia za mapenzi kwa nia ya kumvuta mpenzi wako ili akurudie, unaweza kujisikia vibaya na labda kuumia kihisia kama itatokea hataguswa na picha hizo. 



Namna ya kuondokana na tatizo hilo: Usiwe mtoto mdogo. Kumbuka kwamba kuendelea kumkumbuka mpenzi mliyechana ni jambo lenye kuumiza sana. Ukweli ni kwamba itakuwa ni ujinga kufanya mbinu hizo za kitoto kutumia mitandao ya kijamii kutaka kumvuta mpenzi mliyeachana, kwani kitendo hicho kitakufanya azidi kukudharau na kukuponda. Jaribu kwa juhudi kubwa kutoyapa uzito mawazo yoyote yatakayokukumbusha mapenzi yenu na mpenzi mliyeachana naye. Kwani kuendelea kuyapa uzito mawazo hayo, ndio sababu ya wewe kusumbuka sana kwa mbinu mbalimbali kutaka mrudiane. Iwapo utafanikiwa kuyazika mawazo yote kuhusu huyo mpenzi mliyeachana, hakika utamudu kusonga mbele kwa ustawi wa maisha yako……………….



MZAHA NA KUCHEKESHA HUDUMISHA UHUSIANO KWA WANANDOA...!

Mzaha na Kuchekesha hudumisha uhusiano kwa wanandoa………!


Kucheka mara kwa mara kutakuondolea msongo wa mawazo na mifadhaiko; pia kutakufanya kulala usingizi mnono na kufurahia maisha yako. Uchekeshaji ni kitu muhimu sana na ndio maana viongozi wakuu, waalimu na washauri nasaha wengi ni wachekeshaji katika mazungumzo yao.


Mara nyingi ninapozungumzia au kujadili kuhusu kucheka, huwa najiuliza, hivi ni ndoa ngapi ambapo wanandoa wake hucheka na vicheko hivyo hutoka kwa wenzao? Nalijua jibu, lakini silipendi, ingawa siwezi kuubadili ukweli. Kama kuna ndoa kumi, basi ni ndoa mbili tu ambapo wanandoa wake hupeana afya kupitia kuchekeshana.

Kwenye ndoa nyingi, utakuta mke au mume amenuna muda wote. Hata mwenzake anapojaribu kumchekesha ili kufanya hali iwe na mwelekeo wa amani na upendo, ni kazi bure. Mke au mume huyu anapokuwa nje na nyumbani kwake, ni mchekaji mzuri sana tena wa vichekesho vya kawaida mno!

Nimebaini kwamba, ndoa inapokuwa na vichekesho yaani mzaha na utani usioumiza, humfanya kila mwanandoa kutamani kuwa nyumbani kwake, humfanya kila mwanandoa kuhisi haja ya ukaribu wa mwenzake. Lakini kubwa zaidi ni kwamba, mwanandoa hujenga afya yake ya akili, mwili na hisia kupitia kicheko.

Mara nyingi nikitazama zile sinema za dhati zilizobuniwa na wataalamu wanaojua Nyanja nyingi za kimaisha, huwa ninaona kicheko kikitumiwa sana kuelezea au kuonesha kama ndoa ni ya amani au vurugu. Kama ndoa ni ya amani, ni wazi utaona wanandoa wakitaniana na kufurahia sana utani. Huu siyo ukweli wa kisinema, bali ndio ukweli halisi.

Ndoa bora huweza kupimwa kwa kiwango cha utani kati ya wanandoa. Hebu jaribu kufikiri kwa hatua, halafu ujiulize, ni ndoa ngapi ngumu unazifahamu (pengine ikiwemo yako). Halafu jiulize, huwa unakuta wanandoa hao wakitaniana mara ngapi, kama imeshatokea ukawa karibu nao? Utapata jibu kirahisi sana. Hujawahi, na kama umewahi, basi ni kwa tukio maalumu au tukio la makusudi la wanandoa hao,kukuonesha wewe kwamba, wanandoa hao wako katika amani. 

Ukweli unaendelea kubaki kwamba,kama wanandoa wanajua kuchekeshana, tena kwa makusudi, vurugu ndogondogo huwa zinafutwa kirahisi sana. Ni lazima zifutwe kwa sababu, hatimaye kila jambo huingizwa kwenye mzaha na kuvurugiwa humo.

Wataalamu wanasema, mahali popote ambapo watu wana dhati sana ya mambo (serious), hapo kuna maumivu mengi. Kuna nyumba ambazo kila jambo linajadiliwa na kuzungumzwa kwa sauti kavu na imara ya dhati – hakuna mzaha hata chembe. Mke na mume wako pamoja tangu asubuhi, lakini hakuna hata mmoja ambaye amemfanya mwenzake akacheka. Kama yupo anayejaribu , atakutana na kizuizi cha, ‘si wakati wa mzaha huu.’

Napenda kukushauri kwamba, hebu kuanzia hivi sasa anza kufanya mzaha mdogomdogo kwa mwenzako, lakini wenye nguvu ya kuchekesha. Kama naye alikuwa hajui utamu wa kuchekesha, ataujulia kwako na huenda naye akaanza kufanya mzaha. Lakini mnaweza kwa pamoja kuamua kuanza kuyageuza maumivu mengi kuwa mzaha na vichekesho. Hili linawezekana.

MALEZI YA WENETU YANAPOKUWA YA LAANA...!


Wataalamu wamethibitisha hivi sasa kwamba, familia ambazo wazazi ni walevi kwa mfano, au ni wavuta bangi, ni rahisi sana kwao kuwarithisha watoto wao kuliko watu wanavyofikiria. Jambo ambalo halipendezi katika matokeo ya tafiti nyingi kuhusu hali hii ni ule ukweli kwamba, badhi ya tabia mbaya hujitokeza wakati watoto wa familia yenye ‘laana’ fulani wakiwa barubaru, (miaka 13 hadi 19) au huweza kujitokeza ukubwani. Kwa nini nimesema halipendezi? Subiri nitakwambia.


Tabia walizozitaja wataalamu hao ambazo ni kama laana kwa familia kwa sababu hurithiwa kirahisi na watu wa familia husika ni pamoja na kupigana, kuiba, kukosa uzingativu au utulivu wa mahali pamoja au kukosa uwezo wa kuheshimu sheria au kuheshimu watu walioko madarakani.



Katika jarida la Abnormal Child Psychology la hivi karibuni limebainisha kwamba, ni mara chache kukuta mtoto hajaathiriwa na tabia za wazazi wake ambazo hujitokeza sana katika familia. Kwa mfano kati a watoto watano wa wazazi walevi, anaweza kupona mtoto mmoja tu. Labda tu kama mzazi mmoja anapinga ulevi na ndiye mwenye nguvu kwa watoto. Kwa nini nilisema pale awali kwamba, yale ni matokeo yasiyopendeza? Nadhani unakumbuka. Basi nilikuwa na maana hii:


Mwanamke: Hebu fikiria kwamba, umepata mchumba, handsome boy, ana fedha zake na amesoma madarasa ya kutosha. Anataka kuwa na uhusiano nawe, tena pengine uhusiano wa kudumu yaani kuoana. Je utaangalia tu uzuri, elimu na fedha zake au utakwenda mbali zaidi?

Mwanaume: hebu chukulia kwamba, umekutana na msichana, jicho-jicho, guu-guu, kalio-kalio na anajua mahaba, halafu amekubali kuwa mpenzi wako, nawe umebabaika unataka haraka sana muitwe mke na mume. Je unajitendea haki kuishia kwenye guu-guu tu au unapaswa kwenda mbali zaidi?


Kwa kawaida familia anayotoka mtu ina mchango mkubwa sana kuhusiana na tabia za mtu huyo. Anaweza asioneshe tabia hizo wazi na hata akizionesha kwa kiasi fulani unaweza kushindwa kujua kwamba, ni tabia ambazo hawezi kujiepusha nazo, kwani ni za familia kwa sababu hujui familia yake. Kwa hiyo badala ya kuishia kwenye guu-guu au jicho-jicho na kuishia kwenye u-handsome, elimu au fedha, inabidi uende mbali zaidi. Kama kweli unataka kuwa na familia bora na imara, inabidi uende mbali zaidi pale unaposema umempenda fulani.



Usipoenda mbali utampata handsome ambaye amerithi kupiga mke, amerithi ulevi, amerithi ghubu na mengine yanayofanana na hayo. Kwa kuwa umempenda utakaa kwenye ndoa ya mateso na vipigo, ambapo watoto wenu nao watakuwa ni wa kupiga wake au kupigwa na waume zao na kuwavumilia. Hapo mtakuwa mnaendeleza familia ya laana. Mila na desturi zetu zilikuwa zinahimiza kwamba, kabla ya vijana hawajaamua kuwa pamoja, ilikuwa ni lazima wazazi kujua kuhusu familia ya mwingine. Hata kama haina maana kuwa mmoja akijua mwenzake familia yake ina laana ya kupiga, aachane naye, hapana. Kwa kujua, anaweza kuwa kwenye nafasi ya kujua namna anavyoweza kumsaidia mwenzake kuchana na tabia hiyo au kujisaidia kuepuka vipigo kwa maana ya kuchukua tahadhari.

Wazazi wetu zamani hawakuwa wajinga walipokuwa wanachunguza familia ya mahali binti yao anapotaka kuolewa au kijana wao anapotaka kuoa. Walikuwa hawajui somo linaloitwa saikolojia, lakini walikuwa wakijua kwamba, tabia mbaya au nzuri zinawezsa kuwa zinatembea katika familia. Ni jambo la kusikitisha kukuta binti anajua vizuri familia ya mpenzi wake kwamba, baba wa mpenzi wake huwa anampiga sana mkewe, mbaya zaidi, inawezekana ameshaanza kuona dalili za mkono mwepesi wa kupiga kwa huyu mpenzi wake. Lakini bado anang’ang’ania kuingia kwenye ndoa na mpenzi huyu mkorofi. Huu ni ujinga….


Ukweli ni kwamba ukienda kuoa kwa wapewa na watoa talaka, jiandae kwa kutoa au kupewa talaka. Huna haja ya kujidanganya kwamba, utaweza kubadili tabia hii kirahisi kama unayeoana naye anayo kutoka katika familia yake……….. 

MIAKA MITATU YA NDOA, KIPIMO CHA NDOA KUENDELEA AU KUVUNJIKA...!



Kuna msemo katika Kiswahili kwamba, kipya ni kinyemi. Msemo huu una maana kwamba, kitu kikiwa kipya huvutia sana na wakati mwingine inakuwa kama vile tunaamini kwamba, hatutaweza kamwe kupunguza hisia zetu dhidi ya kitu hicho. Lakini kadiri siku zinavyoenda, mazoea hutufikisha mahali ambapo hatuwezi tena kuendelea na kiwango kilekile cha kupenda.

Tunapooana, kwa sehemu kubwa ni kwa sababu tunapendana, yaani tumevutana. Katika hatua za awali, tunatokea kuoneshana upendo wa dhati sana. Mara nyingi hi inatokana na haja yetu kuwaonesha wenzetu kwamba, sisi ni watu wa upendo, sisi ni waadilifu na wema. Tunachotafuta ni kukubaliwa nao kwa sababu, wakati huo hamu yetu kwao ni kubwa.



Kadiri tunavyokaa pamoja, ile hamu yetu kwao inapungua. Ni vigumu kukuta watu ambao wanaweza kudai kwamba, wameishi kwa muda mrefu na hamu ya kila mmoja kwa mwenzake iko palepale au imeongezeka. Kuna tofauti tu ya viwango vya kushuka kwa hamu, lakini huwa inashuka.


Lakini huku kushuka kwa hisia hakuna maana ya kushuka kwa upendo, hapana. Kushuka kwa hisia kuna maana ya akili na baadaye hisia, kujenga mazoea kiasi cha kumchukulia mwingine kwamba ni wa kawaida, pamoja na kumpenda kuliopo.


Kuna wakati wapenzi hulalamika kwamba, mwenzake alikuwa akipenda kukaa naye kwa muda mrefu, siku hizi hakai kwa muda mrefu tena. Kuna kulalamika kwingi hususan kwa wanawake kwamba, mwenzake haonyeshi ukaribu kama zamani na mengine ya aina hiyo, ingawa bado anaweza kukiri kwamba, anajua anapendwa na huyo mwenzake.


Wataalamu wanadai kwamba, ndoa inapofikia miaka mitatu, mara nyingi ndipo ambapo kama ni kuachana watu huachana au kama ni vurugu, zinakuwa zimefikia mahali pazuri hasa! Katika kipindi cha ile miaka mitatu ya kwanza, ndipo ambapo watu wamefahamiana vema na kama ndoa yao itakuwa ni ndoa ya vurugu, kufikia muda huo inakuwa imeshafahamika.




Ndoa nyingi za vurugu zinakuwa zimefahamika kwamba, ni za vurugu kwa kiwango gani kufikia miaka mitatu. Inaelezwa kwamba, katika mwaka wa tatu, mtu anaweza kabisa kutabiri kama ndoa itakuwa ya amani au vita na kama ni ya vita ni kwa kiasi gani. Kama ni ya vurugu kubwa, hata hivyo, mara nyingi haivuki miaka mitatu.

Kama ndoa imeweza kuvuka miaka mitatu, kwa kawaida kipimo kingine ni miaka mitano. Kwenye mwaka wa tano wa ndoa kuna kuachana na kuapizana kwingi pia. Ukichunguza kwa makini, utagundua kwamba wanandoa wengi hufurahishana na kuachana au kuapizana zaidi mwaka wa tatu na wa tano, tangu ndoa yao.


Hapa kwenye mwaka wa tano, ndipo ambapo wanandoa hujiuliza kama walifanya uamuzi sahihi, ndipo ambapo hutaka kujua kama waendelee na ndoa ngumu kama hiyo au hapana hujihoji kuhusu udhaifu wao (wale wenye hekima). Hapa unaweza kukuta mtu anabadilika tu na kuwa ama mkorofi sana au mwadilifu sana kwa ndoa yake.




Inaelezwa kwamba, baada ya hapo, yaani ukiona watu wamevuka mwaka wa tano salama, kimbuka kinaweza kutokea kwenye mwaka wa tisa. Kwenye mwaka wa saba yale ambayo yalikuwa ni siri ya wanandoa yanaweza kusemwa nje. Inawezekana mume alikuwa ni mzinzi mke akawa anaficha, mke hajui kutunza familia, mume akaficha, yote hayo yanaweza kusemwa hadharani au kwa watu wengine inapofikia mwaka wa tisa.

Kama wanandoa wakivuka salama au wakivuka pamoja na misukosuko yao kwenye mwaka wa tisa, hatua ya mwisho ni mwaka wa 13 wa ndoa. Hapa ndipo ambapo wanandoa wengi wanaamua kwamba, ngoja maisha yaende kama yalivyo au tufikie ukomo. Hebu jaribu kuvuta kumbukumbu na uone kama hakuna wanandoa wengi ambao unawajua, waliovunja ndoa zao kwenye mwaka wa 13! Kama sio mwaka wa 13 palepale inaweza kuwa mwaka wa 12 au wa 14 wa ndoa yao. Lakini kipimo mara nyingi ni mwaka wa 13.



Ukiona ndoa imevuka hapo, watu wakiwa pamoja hata kama kuna vurugu za namna gani za kindoa, huenda wataishi hivyohivyo hadi kifo kiwatengenishe au mmoja amdhuru mwingine…….
This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi