Ipo tabia moja ambayo imeshamiri kwa upande wa kina dada au wanawake wengi ya kuwatelekeza watoto wao nyumbani kwa wazazi wao. Suala la kuwatunza hao watoto wenyewe kama wazazi huwa halipo, wakishazaa hujua jukumu lao limekwisha, hivyo majukumu yote ya kuwatunza na kuwalea watoto wao, huyaacha mikononi mwa wazazi wao.

Wanawake hawa hufanya hivyo kwa kisingizio kwamba, wanakwenda kutafuta fedha za matumizi kwa ajili ya watoto wao, kwa kuamini kwamba, wanapowaacha watoto hao nyumbani kwa wazazi wao (Kwa babu na bibi wa watoto), kazi yao ya utafutaji wa fedha huwa rahisi zaidi.



Ukweli ni kwamba, watoto waliotelekezwa na mama zao, huongeza mzigo mkubwa kwa wazee hao, ambao walio wengi tayari wameelemewa na mzigo wa hali ngumu ya kiuchumi. Akina dada wenye tabia hii huwa hawapo tayari kuwajibika wao binafsi, wala kuwawajibisha wanaume waliowapa mimba, kwa lengo la kutaka kuendelea na starehe zao bila bughudha ya watoto na wengine huona watoto kama mzigo utakaowazuia kufanya shughuli zao za kuwapatia kipato.




Kulingana na hali ngumu ya kimaisha na utegemezi waliyo nayo wazazi hawa wanaopelekewa mzigo wa watoto, hukubali kwa haraka kuishi na wajukuu zao, kwa lengo kusaidiwa na kunufaika kiuchumi, kutoka kwa hao watoto wao, pale watakapotumiwa misaada na fedha za matumizi kwa ajili ya wajukuu zao. 




Lakini kwa bahati mbaya sana baadhi ya wazazi hao hujikuta wakiumia kwa kukosa misaada hiyo toka kwa watoto wao kama walivyoahidiwa. Kwani wazazi wengine wenye hao watoto hutokomea kabisa mijini na kusahau watoto wao na wengine hujikuta wanarudi majumbani kwa wazazi wao na kuwa mzigo mwingine, kwa kuwa jitihada za kutafuta fedha za matumizi ya watoto wao zimeshindikana. 




Ipo mifano mingi ya watoto wanaotunzwa na babu na bibi zao, ambao wanaonekana kwa kila hali kukosa malezi bora na huduma muhimu za msingi, kutokana na wazazi wao kutotuma fedha kwa ajili ya matumizi ya watoto wao. Kina mama wenye tabia ya kutelekeza watoto wao kwa wazazi wao bila kutuma fedha za matumizi kama walivyoahidi, wanapaswa kuondokana na tabia hiyo mara moja. Si vyema kusukumia majukumu hayo mazito kwa wazazi wao ambao tayari wameshazeeka.