0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

http://www.serenahotels.com/serenadaressalaam/default-en.html

Sep 26, 2009

MASAIBU YALIYONIKUTA USIKU WA JANA!

Ilikuwa ni kazi kweli kweli, lakini yote yalikuwa ni majaaliwa

Kuna wakati Rais wa awamu ya pili ndugu Ali Hassan Mwinyi aliwahi kusema kuwa moto mkubwa huanzishwa na cheche, akimaanisha kuwa jambo lolote kubwa linaweza kuanzishwa na jambo dogo sana.

Jana wakati narudi kutoka katika mihangaiko yangu majira ya saa tatu usiku nilipata mkasa ambao mpaka leo hata sijui ilikuwaje, nilipanda basi la kuelekea Buguruni pale maeneo ya Posta majira ya sa tatu usiku hivi. Tulipofika Maeneo ya Kariakoo walipanda abiria wengine watatu lakini walionekana kuwa wamelewa sana. Wakati tukiendelea na safari mara ukazuka mzozo kati ya mmoja wa wale abiria waliolewa na abiria mwingine, kisa huyo abiria mwingine kakanyagwa na yule mlevi.

Vikazuka vita vya maneno, ilianza taratibu hivi, lakini kwa jinsi basi lilivyokuwa likiendelea na safari na ndivyo wimbo wa matusi kati ya abiria hao ulivyozidi kupamba moto, kutahamaki wakaanza kutupiana matusi ya nguoni na ya kudhalilisha sana haya yakilenga kuwadhalilisha wazazi wa kike, naamini mmeelewa mpaka hapo namaanisha nini.

Nilianza kuhisi shari mapema kabisa lakini sikuwa na jinsi nilikaa siti ya mwisho, kwani kama ningekaa karibu na mlango ningeshuka, lakini basi lilijaa na hapakuwa na njia ya kupita.
Vita ile ya matusi na ilianza kuwa kuwahusisha abiria wengine ambao walikerwa na matusi ya wale abiria walevi, ghafla wakaanza kupigana huku basi likiendelea kwenda kwa kasi. Mara zikazua kelele za abiria wengine wakimtaka dereva asimamishe basi ili watu washuke kwenye basi ili kuepuka ule ugomvi ambao sasa uligeuka kuwa ugomvi wa kupigana zilizidi mle ndani ya basi.

Dereva alisimamissha basi na kwa kuwa walikuwa wamengushana sakafuni kwenye basi ilibidi tupite juu ya viti ili kuelekea mlangoni, nilipoukaribia mlango abiria mmoja akamuamrisha dereva apeleka basi kituo cha Polisi pale Buguruni, nilikuwa bado sijateremka, ghafla basi likaondolewa kwa kasi ajabu, abiria mmoja akanisukuma na kujikuta niko chini kwenye lami na niliona tairi la nyuma la lile basi likipita usawa wa uso wangu, kutahamaki nikasikia sauti ya gari lingine likifunga breki za ghafla, nilipogeuka niliona gari dogo likiwa usawa wa pale nilipoangukia, nilijizoa pale na kujisogeza kando ya barabara, huku wapita njia wakinizunguka kutaka kujua kama nimeumia au la, ili wanikimbize hospitali. Nilijichunguza na kuona kuwa nina michubuko kidogo katika mikono yangu kutokana na kuangukia kwenye lami, lakini nilihisi mkono wangu wa kulia ukiuma kwa mbali, niliyapuuzia yale maumivu na hata niliposhauriwa niepekwe hospitali nilikataa kwani hata basi lenyewe lilishatokomea kusikijulikana.

Nilipanda basi lingine na kurudi nyumbani kwangu, nilipolala, ndio nikanza kusikia mausmivu makali ya mkono wangu wa kulia, na sikulala pamoja na kumeza vidonge vya kutuliza maumivu. Alifajiri na mapema niliwahi hospitalini na baada ya kupigwa X-Ray ikaonekana kuwa mkono wangu umeteguka kwenye kiungo. Nikatibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani.

Bado najiuliza, hivi ilikuwaje, kwa nini wale abiria ambao hawakulewa hawakuwapuuza wale abiria waliolewa na kuwaona kama wajinga hivi ili kuepusha shari? kwa nini walishindwa kuwavumilia kwa dakika chache ambapo kila mtu angeshuka kwenye basi na kuelekea nyumbani kwake?

Ni kitu gani wangepoteza kwa kuwapuuza walevi wale? Hivi kama lile gari lingenikanyaga ni nani angelaumiwa, ni wale abiria walevi au dereva? Na lile gari dogo je? kama dereva asingefunga breki ingekuwaje?

Pamoja na kuwa mkono wangu wa kulia umefungwa bendeji na hauna kazi lakini kwa kutumia mkono mmoja wa kushoto nimemudu kuwapasha yaliyonikuta jana
.
This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi