0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

http://www.serenahotels.com/serenadaressalaam/default-en.html

Jun 21, 2009

MAJAMBAZI YALIPOTAKA KUNIULIA MWANANGU USIKU WA JANA

Abraham akitatafakari tukio la jana

Kuna wakati mambo mengine inabidi yatokee ili maisha yaendelee.
Katika kujifunza kwangu maarifa haya ya utambuzi nimegundua kwamba
Matukio yote tunayokutana nayo yanakuwa yanatufundisha jambo fulani muhimu maishani.
Kama ukianza kutazama matukio na matendo ya watu ambao unakutana nao kwenye maisha yako ya kila siku kwa kujiuliza kile unachojifunza kutoka katika matuki hayo utajikuta unaanza kuyatazama kwa jicho tofauti yale uliyokuwa ukiyaona hapo kabla kama maudhi au yenye kukatisha tamaa. Utaanza kuhisi ukipungukiwa na kiwango cha kukerwa, kuchanganywa na kubughudhiwa na vitendo na mapungufu ya wengine..
Hapa ninapoandika makala hii siamini kabisa kama niko hai mimi na familia yangu.
Usiku wa jana majira ya saa tisa za usiku tulivamliwa na Majambazi zaidi ya kumi wakiwa na silaha mbali mbali kama vile mapanga, marungu na Bastola .
Nyumba ninayoishi iko maeneo ya Tabata Bima na ni Non Crime area kwa maana kwamba hakuna uhalifu wa kutisha na tukio hili la jana limemuacha kila mtu mdomo wazi, kila mtu alikuwa akijiuliza KULIKONI JAMANI!!!!

Jana nlikuwa kazini na nilirudi nyumbani majira ya saa tatu za usiku nikiwa nimechoka ile mbaya, na hata mwanangu Abrahamu nilimkuta alikuwa hana furaha kabisa kama kawaida yake.
Nilipanda kitandani kulala sa nne na nusu usiku baada ya kupata mlo wa usiku.

kama unaamini katika maono, au njozi basi tukio hili nilifahamishwa kabla hata halijatokea

Ilikuwaje?

Ngoja niwasimulie. Katika hali ya kuashiria kuwa kuna jambo baya litatokea, nikaota ndoto ya kushangaza sana.
Niliota kwamba nilitoka kwenda katika kampuni fulani kufuatilia masoko na huko wakanipa kiasi kikubwa cha fedha ambacho kilikuwa na mchanagnyiko wa Dola za Kimarekani na za Shilingi za Kitanzania ambazo nilitakiwa kuziwasilisha kazini, kwani lilikuwa ni deni ambalo kampuni ninayofanyia inaidai kampuni hiyo.

Nilipewa lifti na mmoja wa wafanyakazi wa kampuni ile na alinishusha karibu na kazini kwangu, nilipovuka barabara, nikakutana na watu wawili wakiwa na bastola wakataka kuninyang'anya ule mkoba wenye hela, sasa nikawa navutana nao huku wapita njia wakipita bila hata kutoa msaada na walikuwa wakiona kila kitu, nikawa nawaonyesha ishara walinzi wa kampuni ninayofanyia kazi kuwa naibiwa lakini nao hawakunijali hata sikumbuki ile ndoto iliishaje nikastukia kishindo cha mlango ukivunjwa.
Nilipoamka nikajikuta nimewekewa bastola kichwani na mwanangu Abrahamu kashikwa kichwa chini miguu juu, huku wakitishia kuniua mimi na mwanangu pamoja na mke wangu, kama sitawapa pesa.
Mke wangu alizimia ghafla kwa hofu.

Nilinyanyuka huku nikipigwa na mapanga kwa ubapa mgongoni na kuwapa pochi iliyokuwa na kiasi cha shilingi elfu sabini.

Wakakataa wakidai kuwa hawawezi kuvunja nyumba kwa elfu sabini na nisiwatanie kwani taarifa walizonazo ni kwamba sisi wapangaji wa nyumba ile tuna hela sana na wakatishia kumkata kichwa mwanangu.

Kuona hivyo nikajua kuwa hawatanii kwani walikuwa ni wengi sana, nikawapa mkoba wangu mweusi uliokuwa na vijisenti vyangu vya akiba, hawakuridhika na kuanza kunipiga kwa ubapa wa panga nikawaambia kuwa kama wanataka kuniuwa basi wafanye hivyo kwani sina hela tena.

Basi wakachukua TV, Deki ya DVD, Mobile phone 3 na Music System, lakini walishindwa kubeba Computer yangu kwa madai kuwa itawapotezea muda kuchomoa nyaya, niliposikia hivyo nilishukuru sana kwani kile kitendea kazi changu kingechukuliwa, ningeadimika mtandaoni, na blog ya Utambuzi na Kujitambua ingesinzia kidogo.

Kumbe walianzia kwa wapangaji wenzangu. Nyumba yetu ina wapangaji wanne.
Baa day a kuchukua kile walichoamini kuwa kingewasaidia kusogeza maisha yao mbele walitoka na kutufungia mlango wa chumbani kwa nje ili tusitoke kuwasaidia wenzetu, kwani walikuwa wakiendelea kuvunja vyumba vingine.

Majambazi hayo yalitumia takribani nusu saa katika kuvunja na kuiba kisha yakatoweka.
Niliungana na wapangaji wenzangu pamoja na majirani waliojitokeza baada ya tukio lile kwenda kutoa taarifa kituo cha polisi kilichopo jirani, Pale kituoni tulishauriwa twende kituo cha polisi Buguruni kwani ndipo tunapoweza kufungua faili na kupewa RB.

Mpaka sasa Polisi bado wanaendelea na uchunguzi na watuhumiwa hawajatiwa mbaroni.
Hali ya familia yangu na ya familia za wapangaji wenzangu tulioibiwa pamoja bado ni tete na bado nina maumivu ya mapanga ya mgongoni.

Napenda kuchukua nafasi hii kumshukuru mungu muumba kwa kutuponya katika kadhia ile na kuepuka kifo, kwani roho zetu zilikuwa mikononi mwa majambazi hayo.
This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi