0715 72 92 92

SHABAN KALUSE

Kwa Matangazo na mambo mbalimbali & Wasiliana Nami

http://www.serenahotels.com/serenadaressalaam/default-en.html

Mar 19, 2009

KAMA KIFO HUJA HIVI, BASI KIFO NI KITAMU. SEHEMU YA MWISHO.

Sioni sababu ya kukihofia kifo tena

Habari hii niliiandika wiki iliyopita na niliahidi kuimalizia wiki hii. Huu ni mkasa wa kweli ambao unasimuliwa na muhusika mwenyewe, mwanafunzi mwenzetu katika madarasa ya Utambuzi pale Kimara Rombo.
Fuatana nami ili kumalizia mkasa huu....
Ghafla yule daktari akatamka kwa sauti kama anapiga kelele “ Taifodi” na mimi kwa kasi ya ajabu nikiwa katika umbile lile lile la upepo nikaingia katika mwili wangu kwa kupitia sikio langu la kulia na mara nikahisi mwili wangu ukiunguzwa na moto mkali ambao sijui ulitoka wapi, mara nikastuka na kuamka, na kuwaacha watu wote pale ndani akiwepo mama yangu wakishangaa, wote walikuwa wameduwaa.

Nilianza kumnanga yule daktari kwa maneno ya kejeli. Kwani ile ilikuwa ni mara ya pili naenda katika hospitali ile na kumkuta daktari yule yule lakini alikuwa akidai kuwa siumwi, na akanishauri kuwa nitafute boyfriend, sijui alikuwa na maana gani?
Nilisema maneno mengi ya kumdhihaki na kumuuliza “Sasa umeamini kuwa kweli naumwa?”
Hakujibu kitu kwani alionesha kushikwa na tahayari na uso wake ulikuwa umesawajika.

Vipimo vilionesha kuwa nilikuwa na taifodi ambayo kwa mujibu wa daktari yule ilikuwa imefikia katika hatua ambayo hawaamini kuwa ningeweza kuwa hai.

Tatizo langu lilianza mwaka 1994, nilipofunga choo kwa takriban mwezi na nusu na kila nikienda pale hospitalini nilikuwa nadai kuwa naumwa tumbo, kwani niliona aibu kusema ukweli kwa kudhani kufunga choo ni ugonjwa wa aibu ambao haupaswi kusemwa.

Yule daktari aliniambia nilale kitandani, naamini wasichana wengi watakubaliana na mimi kuwa kitendo cha kuambiwa ulale kitandani na daktari kilikuwa kinaashiria nini , hasa kama unadai kuwa unasumbuliwa na tumbo.

Nilikuwa na mtazamo hasi juu ya madaktari kuhusiana na na kitendo cha kuambiwa nilale kitandani kwani kuna wakati niliwahi kusimuliwa kuwa daktari akikwambia kuwa ulale kitandani kisha akavaa gloves basi anataka kuingiza mkono wake kwenye uke ili kupima au kuchukuwa vipimo.

Hivyo kitendo cha kuambiwa nilale kitandani na daktari nilikuwa najiwa na picha ya kufanyiwa kitendo hicho. Pia niliwahi kuambiwa kuwa ugonjwa wa kufunga choo niliokuwa nao, matibabu yake yalikuwa ni kipigwa bomba. Hilo nalo lilinitisha na ndio sababu nilikuwa nauficha ugonjwa huo uliokuwa ukinisumbua.

Nakumbuka tatizo langu lilifikia katika hatua mbaya siku nikiwa kazini.
Nilikuwa nauza duka la madawa mjini, na siku hiyo nilikuwa napanga dawa kwenye makabati mara kijana mmoja mtumiaji wa madawa ya kulevya, maarufu kama Teja, alikuwa akihitaji bomba la sindano, nadhani alikuwa akienda kujidunga sindano ya madawa ya kulevya.

Nilichukuwa hela aliyokuwa nayo mkononi na kumpa lile bomba la sindano, basi kile kitendo cha kumpa lile bomba nikajiona nikianza kutetemeka na huku jasho likinitoka, mara nikastukia nikipiga kelele nikanguka na kupoteza fahamu.

Nilipostuka nilikuwa nimelazwa hospitalini pale magomeni, nilipojikagua nikaona nimetundikiwa dripu lenye maji ya njano, moja kwa moja nikajua nimewekewa dripu la kwinini.

Nilipata hofu sana kwani mimi sipatani na kwinini na dawa aina ya salfa na niliwahi kuonywa na daktari kwamba nisitumie kabisa hizo dawa kwa kuwa zinaniletea Mzio (Allergy). Ilikuwa nikitumia dawa hizo navimba mwili mzima na kutokwa na vidonda mwili mzima.

Nilitamani kulichomoa lile dripu lakini sikuwa na nguvu ya kufanya hivyo, mara daktari akatokea, alipofika pale kitandani nilipolala nilimuomba atoe ile dripu na kumweleza kuwa ile sio dawa kwangu bali ni sumu itakayoniuwa.

Yule daktari alinijibu kuwa hawezi kutoa ile dripu kwa kuwa nimepimwa na kugundulika kuwa nina malaria.
Wakati naendelea kubishana na yule daktari, mama yangu na dada yangu walifika pale na kumuomba yule daktari atoe lile dripu, hiyo ilikuwa ni baada ya kumuelewesha kuwa nilikuwa niko sahihi na sio kwamba malaria ilikuwa imepanda kichwani, kama alivyokuwa akidai.

Nilirudishwa nyumbani, huku nikiwa na siri yangu moyoni kuhusu ule ugonjwa wangu wa kufunga choo kwa muda mrefu. Hata hivyo sikuunganisha tukio la kuanguka kwangu ghafla pale kazini na ule ugonjwa wa kufunga choo.

Nilipofika nyumbani mama alinitengenezea supu ya mboga mboga na kunipa ili niweze kurejesha nguvu kwani niliishiwa na nguvu kabisa.

Nilipomaliza kunywa ile supu nikajipumzisha kwenye pale sebuleni na ndipo ile hali ya kufa ganzi kuanzia kwenye unyayo iliponianza.

Nakumbuka nilipokuwa nirudi nyumbani baada ya kutoka hospitalini nilimwambia mama yangu kuwa nataka kusali na kuna kitu kilikuwa kinaniongoza kwenda kutafuta nyumba ya kusali.

Wakati huo ilikuwa ni saa nne za usiku, nilijikuta nikielekea kwenye nyumba moja ya jirani yetu mmoja Msabato na huku mama, dada na kaka yangu wakinifuata kwa nyuma, kwani waliamini kabisa kuwa nimechanganyikiwa au nilikuwa na mapepo.

Nilipofika pale nilimkuta yule mama akiwa ndio anafanya usafi, baada ya kumaliza kupika keki, kwani yule mama alikuwa ni mpishi wa keki pale mtaani. Nilipofika nilimwambia tena kwa amri, “Njoo hapa uniombee sasa hivi” nilikuwa naongea kwa sauti yenye mamlaka kama vile namuamrisha mtoto mdogo, ingawa nilihisi kuwa nilikuwa naongea kwa sauti kubwa lakini baadae nilisimuliwa kuwa sauti yangu ilikuwa ni ndogo sana.

Yule mama alibaki ameduwaa, mara mwanae aliyekuwa na umri wa miaka mitano hivi alifika na kunishika kichwa, wakati huo nilikuwa nimekaa chini pale sebuleni kwao, yule mtoto alinishika kichwa na kuniombea kwa kusema, “Baba mungu mponye dada Eggy kwa jina la Yesu, amen” alipomaliza, ule moto ulionichoma pale hospitalini, ulinichoma tena na nikahisi kuwa mwepesi kama vile nilikuwa nimeutuwa mzigo mzito.
Baadae yule mama alikuja tukaomba kwa pamoja.

Kuanzia hapo nikapewa Biblia na kupewa muongozo wa imani.
This Blog Designed by DonSoo, Contact 0656212326.DonSoo
Kaa Karibu na Mimi